Jumanne, 4 Oktoba 2011

VITA KUU YA DUNIA NA VUGUVUGU LA UHURU WA TANGANYIKA.

Askari wa Tanganyika waliopigana vita vya kwanza vya dunia, wakati huo Tanganyika ikiwa chini ya Mjerumani




Na Lawrence Kilimwiko
BAADA ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia, huku takriban watu milioni 56 wakiwa wamegeuka makaburi, juhudi kubwa ilielekezwa katika kujenga amani na kuzuia vianzio ambavyo vingepelekea kuzuka upya vita.

Moja ya mambo ambayo hapana shaka yangelipelekea dunia kurudi katika vita, ilikuwa ni suala la ukoloni na makoloni. Hii ni pamoja na kwamba licha ya kumalizika kwa vita, mataifa ya ulaya bado yalipenda kung’ang’ania makoloni yake barani Afrika , Asia na Amerika ya Kusini.
Na kwa kuwa yalikuwa yako taabani baada ya kugharamia vita, yaliekeza nguvu zake katika kuyakamua makoloni ili yaweze kujijenga upya. Mbinu zilizotumika katika kurekebisha uchumi ulioparaganyika kutokana na vita, ikawa ni  kuimarisha unyonyaji kwenye makoloni.
Ukatili mkubwa ukatumika katika kuhakikisha kuwa makoloni haya yanazalisha ziada. Sheria kandamizi zisizojali ubinadamu zikatungwa kwa mijali ya kufanikisha azma ya kufufua uchumi wa ulaya chini ya usimamizi wa askari.
Kwa sababu hiyo, wananchi wa asili katika makoloni haya walijikuta katika mateso makubwa ambayo dawa pekee ilikuwa ni kuuasi utawala wa kikoloni kwa gharama zo zote.
Wakati huo huo. ilitokea kwamba Amerika,  taifa  ambalo halikuathirika na vita liliibuka kuwa lenye nguvu na ushawishi mkubwa kuliko yote duniani. Itakumbukwa kwamba, wakati vita vikipiganwa, Amerika ilipata faida kubwa kutengeneza silaha pamoja na vyakula na kuziuzia nchi zilizokuwa vitani kwani vita vya panzi ni furaha kwa kunguru.
Kwa mtindo huo, wakati mataifa mengine yote yakiwa taabani, Amerika ilikuwa inaelea kwenye lindi la utajiri  usio kifani.
Amerika ikatumia fursa hiyo, kuandaa mkakati wa amani duniani ikiwa ni pamoja na kusimamia uundwaji wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani,maarufu kama IMF na pia kuhakikisha kuwa sarafu ya Amerika , yaani Dola, ndiyo inayokuwa kigezo cha kubadilisha sarafu zingine katika biashara ya kimataifa.
Kama hiyo haitoshi, Amerika ikahakikisha kwamba makao makuu ya Umoja wa Mataifa na yale ya  Benki ya Dunia na IMF yote yanakuwa nchini Amerika. Zaidi ya hapo, taifa hilo lenye nguvu duniani, likahakikisha kuwa, wakati wote Rais wa Benki ya Dunia atakuwa ni raia wa nchi hiyo ilhali Mkurugenzi  wa IMF atoka katika bara la Ulaya.Kwa njia hii, mfumo mzima wa uchumi  wa dunia na biashara vikasimikwa kukidhi matakwa ya America.

Baada ya mkakati huo kukamilika, ndipo Amerika ilipobuni mpango kabambe wa kufufua uchumi wan chi za Ulaya uliojulikana kama Mpango wa Kufufua Uchumi Marshall au The Marshall Plan kwa kimombo.
 Madhumuni ya mpango huu, ilikuwa ni kuzisaidia nchi za bara la Ulaya ziweze kufufua uchumi wake hasa kwa kukarabati miundo mbinu, viwanda, huduma za kijamii na kununua mali ghafi.
Amerika ilijua wazi kuwa ilikuwa muhimu kwa nchi za ulaya kuimarika kiuchumi ili  iweze kufanya nazo biashara kwani biashara siku zote ni ya pande mbili.
Kukamilika kwa haya yote, kulitoa fursa kwa Amerika kusimamia kile kilichokuwa kimekusudiwa, ambacho ni kuwa na ushawishi mkubwa katika mambo yote katika anga za kimataifa. Ili amani iweze kujengeka duniani, Amerika ikitumia turufu ya kuwa ndiyo taifa lenye nguvu na kwa kupitia mgongo wa Umoja wa Mataifa, ikaja na mpango wa kuzitaka nchi za  Ulaya zenye makoloni kokote duniani kuyapatia uhuru kwani hiyo ni moja ya malengo ya Umoja wa Mataifa.
Ukweli ni kwamba, kile ambacho Amerika ilikuwa imedhamiria ilikuwa ni kuona kuwa  makoloni haya yanakuwa maeneo huru kwa ajili ya biashara hasa upatikanaji wa mali ghafi kwa viwanda vyake. Itakumbukwa kuwa, mpaka wakati huo, Amerika haikuwa na makoloni. Isitoshe baada ya vita, nchi za Ulaya zenye makoloni zilijielekeza huko kwa ajili ya kufufua uchumi wao.
Kwa kujikinga katika mwavuli wa Umoja wa Mataifa suala la kuyachia makoloni ukuru wake ikiwa ni ajenda ya umoja huu.
Ikatokea pia kwamba katika makoloni hayo, hasa kupitia askari waliorejea kutoka vitani kukaibuka wimbi kubwa la vuguvugu la kutaka uhuru wa kujitawala.
Mapinduzi ya huko Urusi na China na baadaye kupatikana kwa uhuru kwa India na Pakistan, kikawa ni kichocheo tosha kwa makoloni kudai uhuru.
Simulizi zinaeleza jinsi askari waliorejea kutoka vitani walivyoeleza mambo mapya waliyoyaona katika nchi za India, Burma, Ceylon, Pakistan na kwingineko wakiwa vitani. Wakasimulia kuhusu vuguvugu la mabadiliko yaliyokuwa yakiendelea huko.
Cha kuchekesha ,waligundua pia kuwa wakati wakiwa vitani walikuwa wakifunzwa uzalendo na utii kwa utawala wa malkia, ni utawala huo huo wa malkia ndiyo uliokuwa kiini cha ukatili waliokuwa wakifanyiwa katika nchi zao za asili. Hii ikachochea uasi.
Lakini askari hawa, pia walisimulia woga wa mtu mweupe vitani. Kwamba pamoja na ubabe aliokuwa anawafanyia wana wa Tanganyika, kwenye vita alikuwa si lo lote.  Wakasimulia jinsi wazungu walivyouliwa na mbu kwenye mahandaki na pia walivyokuwa waoga kwenye uwanja wa mapambano. Udhaifu mkubwa  waliouonyesha katika kukabiliana na adui ukawapa nguvu wazalendo.
Ushuhuda wa aina hii ukawajaza ujasiri wa kujiamini  wakijua kuwa kama hata mtu mweupe alikuwa anapigika, kwa nini wasimfurushe kutoka nchini mwao.
Elimu hii mpya, ikawa kichocheo kipya katika vuguvugu la kudai uhuru wa kujitawala kwa kutumia fursa zilizoletwa na mabadiliko baada ya vita vya dunia.
Nchini Tanganyika, Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kiliweza mara mbili kupelekea ujumbe wake huko New York, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kudai uhuru wa Tanganyika.
Ni dhahiri kama Amerika isingekuwa na ushawishi mkubwa wa kuona kuwa makoloni yanaachiwa kuwa huru, vita vingelizuka katika sehemu nyingi. Haishangazi kwamba , kwa nchi zile ambazo zilijaribu kung’ang’ania makoloni, zilijikuta katika vita, safari  ikipiganwa kati  watawala na watawaliwa.
Vita katika makoloni ya Ureno yalikuwa ni matokeo ya taifa hilo maskini kukataa kuyachia makoloni yake huko Angola, Msumbiji, Cape Verde na Guinea Bissau.
Hii pia ndiyo maana nchi nyingi hasa barani Afrika, ziliweza kupata uhuru  kwa pamoja , wakati mwingine kwa siku moja. Hii ilitokana na ukweli kwamba, pamoja na harakati za wazalendo kudai uhuru, kulikuwa na msukumo mkubwa  uliofanywa na Amerika kupitia mwavuli wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, mataifa ya Ulaya yalichofanya kabla ya kuyaachia makoloni yake uhuru, ilikuwa kwanza, ni kuimarisha mifumo ya kiuchumi ambayo ingewahakikishia kuwa wanaendelea kuzinyonya nchi hizi licha ya uhuru wao.
Mbinu zilizotumika zikiwa ni kuingia katika mikataba ya kibiashara lenye lengo la kuhakikisha rasilimali zote zinaelekezwa kwao kwanza. Na hili likafanyika kirahisi kwa vile mifumo ya elimu, miundo mbinu na hata sarafu zilizokuwa zinatumika zilikuwa ni zile mama wa ukoloni.
Ni dhahiri vuguvugu la uhuru wa Tanganyika lingekuwa lilichukua sura nyingine kama kusingezuka vita vya dunia vilivyopelekea kwanza, Ujerumani kunyang’anywa mamlaka ya kuitawala Tanganyika, na pili Mwingereza asingekabidhiwa udhamini tu wa Tanganyika na Umoja wa Mataifa.

Chanzo; Gazeti la Mwananchi 4.10.2011

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni