Jumanne, 4 Oktoba 2011

TAIFA STARS YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI MBELE YA ALGERIA.

Matumaini ya Tanzania kupata nafasi ya kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwakani yamezidi kuwa finyu kufuatia sare ya bao 1-1 na Algeria katika mechi iliyochezwa jijini Dar esa Salaam.

Timu zote mbili, Tanzania na Algeria zote zimejiweka kwenye wakati mgumu wa kusonga mbele kwani kila moja ina pointi tano wakati Morocco na Jamhuri ya Kati zina pointi saba saba kila moja.

Taifa Stars(picha ya maktaba)
Tanzania inashika nafasi ya tatu kutokana na tofauti kubwa ya magoli ya kufunga kulinganisha na Algeria.

Tanzania ilikuwa na uwezo wa kuifunga Algeria ambayo ilicheza kwa kujihami zaidi lakini washambuliaji wa Taifa Stars hawakuwa makini walipokuwa kwenye lango la Algeria na kupelekea kuzipoteza nafasi tatu za magoli ya waziwazi.

Taifa Stars ndiyo iliyoanza kuliona lango la Algeria kwenye dakika ya 22 kwa goli safi la Mbwana Samata ambaye aliunganisha vyema krosi iliyomiminwa na Nizar Khalfan.

Furaha ya Watanzania iliharibika kwenye kipindi cha pili pale Hameur Bouazza alipoisawazishia Algeria kwenye dakika ya 57 kufuatia makosa ya mabeki wa Taifa Stars.

Tanzania imebakiza mechi ngumu dhidi ya vinara wa kundi D, Morocco na mechi hiyo itachezwa nchini Morocco.

Katika muendelezo wa mechi za kundi hilo, Morocco itacheza leo jumapili na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kati huku timu hizo zikiingia uwanjani zikiwa na matumaini makubwa ya kupata tiketi ya kushiriki fainali ya mataifa ya Afrika ambapo mechi zake zitachezwa kwenye nchi za Gabon na Equatorial Guinea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni