Jumamosi, 1 Oktoba 2011

MAAFISA ARDHI NDIO CHANZO CHA MIGOGORO ARDHI.

 
Picture
Mh. Ole Medeye.

Migogoro mingi ya ardhi inayotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi inasababishwa na maafisa ardhi wanaouza ardhi mara mbili kwa watu tofauti, jambo ambalo limesababisha wananchi kugombana na kuchukiana.  Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye kwenye mkutano wa wadau wa ardhi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Ole Madeye alisema kuwa maafisa hao wamekuwa na tabia ya kupenda fedha huku wakijua kuwa wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao na kusababisha chuki kati yao kitendo ambacho kinachochea migogoro hiyo, jambo ambalo ni hatari na kwamba jamii inapaswa kupiga vita tabia hiyo.

“Maafisa ardhi wasio waadilifu ni hatari, kwa sababu wanachangia kuwepo kwa migogoo ya ardhi kwenye maeneo yao, jambo ambalo ni hatari katika jamii inayowazaunguka, na kwamba inachangia serikali kuonekana imeshindwa kazi, kutokana na hali hiyo tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria,”alisema Ole Medeye.

Aliongeza, ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali, hivyo basi kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji, lakini baadhi ya maafisa hao wanashindwa kufanya hivyo badala yake wanaweka tamaa ya fedha mbele, ni tatizo kubwa.  Alisema atakayeshindwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na serikali ajiondoe mwenyewe kabla ya kuondolewa kwa sababu wanarudisha nyuma maendeleo ya wananchi katika eneo husika  na kwamba wanachochea migogoro hiyo.

Alisema, kutokana na hali hiyo maafisa hao wanapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza matatizo yaliyojitokeza ambayo yamesababisha wananchi kuijengea chuki serikali na kuonekana imeshindwa kuwajibika kwa ajili ya watu wachache.

Ole Medeye alisema, ’mteja ni mfalme’, hivyo basi wateja wa maafisa ardhi ni wananchi, kutokana na hali hiyo wanapaswa kuwashirikisha kwa kila hatua inayofikiwa,ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha, na kuwaeleza mchakato mzima wa kuendeleza ardhi au kutafuta wawekezaji ili waweze kuelewa jambo ambalo naamini linaweza kupunguza migogoro hiyo.

Hata hivyo, Ole Medeye mpaka sasa baadhi ya maafisa hao hawana takwimu sahihi za viwanja wanavyomiliki na kwamba takwimu watakazozitoa katika kipindi hiki siyo za ukweli, hii inatokana na uzembe katika kutimiza wajibu wao, kutokana na hali hiyo wanapaswa kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kubaini viwanja vilivyopimwa, vilivyouzwa pamoja na viwanja vinavyotakiwa kupimwa ili waweze kukusanya kodi ipasavyo.

“Maafisa hawa hawana takwimu sahihi ya viwanja wanavyovimiliki, hii inatokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo, jambo ambalo limesababisha kupotea kwa kodi ya ardhi, kutokana na hali hiyo wanapaswa kubadilika ili tuweze kukusanya mapato yetu stahiki,” aliongeza. Alibainisha, ikiwa watafanya hivyo, wataweza kushirikiana na wananchi ili kuondoa migogoro hiyo pamoja na kufuata taratibu zinazotakiwa katika kuendeleza kazi zao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni