Jumanne, 11 Oktoba 2011

JAMBAZI MSAFIRI ILOMO AKAMATWA NA MALI KIBAO HUKO IRINGA.



NewsImages/5998010.jpg
Baadhi ya mali zilizopatikana nyumbani kwa jambazi Msafiri Ilomo. Picha na Francis Godwin, Iringa
Hili sio ghala la kuhifadhia mali za duka lolote lile nchini bali ni nyumba ambayo jambazi sugu wa mkoani Iringa alikuwa akificha mali alizozipora toka kwa wananchi aliowaua kwa kutumia nondo au kuwajeruhi vibaya kwa nondo.
Jambazi Msafiri Ilomo pamoja na kundi la majambazi wenzake sugu wa mkoani Iringa, walikuwa wakiwatesa wananchi kwa kuvamia nyumba zao na kuwajeruhi kwa nondo kama sio kuwaua kabisa.

Katika matukio yao ya ujambazi, Msafiri na wenzake walipora mali na kuzificha kwenye nyumba yao ya udongo kwenye eneo la Kigamboni kata ya Mwangata.

Mali nyingi zilizofichwa na Msafiri kwenye shimo ambapo juu yake alilima bustani ili isijulikane.



Mali nyingi zaidi zilifichwa chini ya ardhi kwenye shimo kubwa lililochimbwa mbele ya nyumba hiyo ambapo kwa juu shimo hilo lilifunikwa na kuwekwa matuta na kuonekana kama vile ni bustani ya mboga mboga.

Msafiri na wenzake walikuwa hawachagui ni nani wamuibie au waibe sehemu gani. Mali zilizokutwa kwenye nyumba yao ziliibwa toka kwa wananchi na hata misikitini na makanisani.
Jambazi Msafiri katika pozi.


Mali zilizokutwa kwenye nyumba hiyo ni pamoja na TV, DVD, nguo, vyombo, magodoro, baiskeli, sofa, masanduku ya nguo, vitanda, mabati, simu za modeli mbalimbali, visu, CD na pia vyombo vya makanisani na misikitini.

Wananchi wa kata ya Kigamboni walikuwa wakiishi kwa hofu ya majambazi hao ambao hadi sasa wameishawaua jumla ya wananchi wawili na kuwajeruhi kwa ncndo watu wengi.

Siku za mwizi zilitimia 40 juzi baada ya majambazi hao kufeli jaribio lao la kumpora mali kijana mmoja wa kata hiyo ambaye alipiga kelele kali baada ya kunusurika kutandikwa na nondo. Kelele zake ziliwavuta wananchi ambao waliwakimbiza majambazi hao ambao walimbilia kwenye nyumba ya Msafiri.

Wananchi walipoingia ndani ya nyumba hiyo walipigwa na butwaa kukuta mali mbali mbali zikiwa zimezagaa kila kona. Hata hivyo majambazi hayo yalifanikiwa kutoroka na kutokomea vichakani.

Mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi alifika kwenye eneo la tukio na kushuhudia wingi wa mali zilizokutwa ndani ya nyumba hiyo na aliamuru nyumba hiyo ivunjwe pindi polisi watakapomaliza taratibu zao kwakuwa nyumba hiyo ilikuwa imejengwa kinyume cha sheria na ilikuwa imeishapigwa X.

Jambazi Msafiri alikamatwa na kwa bahati nzuri alikubali kuwaonyesha polisi sehemu ya siri waliyokuwa wakificha mali hizo ambayo ilikuwa ni shimo lililokuwa chini ya bustani iliyokuwa mbele ya nyumba hiyo.

Mali zilizopatikana chini ya shimo hilo zilizidi kuwashtua wananchi kutokana na wingi wake. Mali zote zilizopatikana kwenye nyumba hiyo zilichukuliwa na kupelekwa kwenye kituo cha polisi kwa utambuzi zaidi.

Taarifa zaidi zilisema kuwa mwezi uliopita Msafiri alifiwa na mtoto wake lakini alifanya msiba huo kuwa wa wasiri ambapo mazishi yalifanyika nyumbani kwa wazazi wake kwa kuhofia watu wangegundua mali zilizopo kwenye nyumba hiyo iwapo msiba ungefanyika hapo.

Taarifa zaidi ziliongeza kuwa jambazi Msafiri alitoka jela kwa msamaha wa rais lakini hadi sasa ameishafanya matukio mengi ya kikatili katika kupora mali za wananchi.

Polisi mkoani Iringa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo lililowagusa wakazi wengi wa mkoani humo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni