Jumanne, 25 Oktoba 2011

MWILI WA GADDAFI UMEZIKWA KWA SIRI JANGWANI

Kanali Gaddafi 'azikwa' kisiri Libya

Mazishi ya kanali Muammar Gaddafi, mwanae Mutassim na waziri wa ulinzi yamefanyika katika sehemu ya siri leo alfajiri.
Msemaji mmoja wa baraza la kitaifa la mpito (NTC) ameiambia BBC kuwa miili ya watu hao watatu imezikwa baada ya utata kuhusu pale watakapo zikwa.
mwili wa kanali Gaddafi
Gaddafi amezikwa

Jamaa wa kabila la Kanali Gaddafi waliomba wapewe mwili wa kiongozi huyo ili wauzike mjini Sirte, alipozaliwa lakini inasemekana kuwa viongozi wa baraza la kitaifa la mpito walipinga ombi hilo.
Taarifa zingine zinamnukuu msemaji wa NTC Ibrahim Beitalmal akisema jamaa wachache wa familia ya Gaddafi walishiriki katika mazishi hayo na dua zilisomwa kulingana na utaratibu wa Kiislamu.
Baadhi ya watu mjini Misrata wanasema miili ya watu hao watatu iliondolewa usiku kutoka sehemu ilipohifadhiwa katika harakati za kupanga mazishi hayo.
Raia wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la Misrata kujionea mwili wa kiongozi huyo ili kuthibitisha ukweli kuwa ameuawa.
Viongozi wa NTC walikuwa wanahofia kuwa huenda Kanali Gaddafi akizikwa katika sehemu iliyowazi, kaburi lake huenda likabadilishwa kuwa pahali patakatifu na wafuasi wake.
Pamoja na hilo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza uchunguzi ufanyike kubainisha jinsi alivyouawa kanali Gaddafi, kwani picha za awali zilionyesha kuwa alikamatwa akiwa hai.
Kiongozi wa NTC Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuwa uchunguzi utafanyika kuhusu hilo. Hata hivyo, kuna wale wanaohoji ikiwa kweli uchunguzi huo utakuwa wa wazi ikiwa mashirika ya kujitegemea hayata husishwa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni