Jumatano, 12 Oktoba 2011

POLISI WAFUNGUA MADUKA YENYE MSAMAHA WA KODI KAMA YALE YA JW


Mkuu wa Jeshi la Polisi, Saidi Mwema.


Kilio cha polisi chaanza kusikika

Na Florah Temba, Moshi

SERIKALI imeondoa kodi kwenye baadhi ya bidhaa za ujenzi kwa askari polisi ili kuwawezesha kujenga nyumba kwa gharama nafuu kulingana na vipato vyao.Hatua hiyo imechukuliwa
siku chache baada ya Kambi ya Upinzani Bungeni kulia na serikali kuhusu huduma duni inazotoa kwa askari polisi, hatua iliyotafsiriwa kuwa kambi hiyo ilikuwa inawachochea askari hao kugoma.

Hayo yalibainishwa jana na Kamishna ya Idara ya Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Patrick Kassera wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa udhibiti na uendeshaji wa maduka ya bidhaa zenye msamaha wa kodi kwa Jeshi la Polisi iliyofanyika katika Chuo cha Polisi Moshi(CCP).

Bw. Kassera alisema msamaha huo wa kodi kwa maduka ya jeshi ni mwendelezo wa msamaha ambao ulikuwepo kwa muda mrefu wa vinywaji vya bia na soda ambao ulikuwa kwa lengo la kuwapa askari motisha ya kufanya kazi.

Alisema msamaha wa sasa unalengo la kumnufaisha askari zaidi na kumuongezea uwezo wa kununua bidhaa muhimu zinazohitajika.

“Kwa kuzingatia hali halisi ya kazi za askari, ambapo muda mwingi anakuwa kazini na hivyo hana muda wa kufanya kazi nyingine ya kumuongezea kipato, ili kujiendeleza ikilinganishwa na watumishi wengine wa umma," alisema na kuongeza;

"Serikali imeondoa kodi kwenye baadhi ya bidhaa za ujenzi vinavyouzwa kwenye maduka hayo ya polisi ili askari waweze kujenga nyumba kwa gharama nafuu.”

Kamishna alitumia nafasi hiyo kuwataka askari kuhakikisha wanatumia fursa hiyo vizuri.

Alisema hatarajii kusikia ofisa yeyote amechukua bidhaa na kupeleka nje au kwa ndugu yake, kwani kufanya hivyo ni kukiuka matakwa na kusudio la serikali.

Kwa mujibu wa kamishana huyo misamaha ya kodi imekuwa ikipunguzia serikali mapato yake na kupunguza uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.

Msamaha wa kodi uliotolewa safari hii ni kwa askari wote bila kubagua kwa kuangalia cheo, hivyo ni wajibu wa wasimamizi wakuu kuhakikisha kila askari anafaidika na msamaha huo.

Awali, akitoa taarifa ya mafunzo Kamishna wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali wa Jeshi la Polisi, Bw. Clodwin Mtweve alisema, mafunzo hayo ni muhimu ili kuwajengea uwezo maofisa wanadhimu wa mikoa na wenyeviti wa kamati za kantini.

Wakati wa Bunge la Bejeti Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Bw. Godbless Lema alitoa lawama mbalimbali wa serikali kwa kushindwa kupatia mishahara ya kukidhi mahitaji yao wala kuwajengea nyumba, hatua inayosababisha wengi wao, hasa wa vyeo vya chini kuishi uraiani au katika nyumba zisizolingana na majukumu yao.

Chanzo; Gazeti la Majira

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni