Jumatatu, 24 Oktoba 2011

SIMU YA MKONONI ILIMPONZA GADDAFFI NA KUFANYA NATO WAJUE KAJIFICHA WAPI?

Katika muda wote wa vita nchini Libya, Gaddafi alijitahidi kutoacha alama yoyote ambayo ingepelekea ajulikane sehemu aliyokuwa amejificha.

Kosa kubwa sana ambalo lilipelekea kifo chake alilifanya siku moja kabla ya kukamatwa kwake na baadae kuuliwa.

Gaddafi baada ya kuzidiwa na mashambulizi ya majeshi ya baraza la mpito na yale ya NATO, Gaddafi alitumia simu ya satelite kuwapigia wafuasi wake kusini mwa Libya akiwaomba wamtumie wanajeshi 12,000 ili kumsaidia kupigana vita na ndipo NATO ilipoidaka simu hiyo na kugundua sehemu ambayo Gaddafi alikuwa amejificha.

Baada ya kugundua amegundulika sehemu aliyokuwa amejificha, Gaddafi akiwa na msafara wa magari 80 alijaribu kutoroka mji wa Sirte lakini alikumbana na mashambulizi ya angani ya NATO ambayo yalitumia ndege za kivita za Ufaransa za Mirage 2000D pamoja na ndege za kivita za Marekani ambazo hazibebi mtu zinazoitwa, Predator.

Wakati huo huo, majeshi ya NTC yalitaarifiwa sehemu alipo Gaddafi na hivyo kupelekea Gaddafi awe kwenye mashambulizi makali ya angani na ardhini.

Gaddafi alilazimika kurudi kwenye mji wa Sirte ambako baadae alikutwa akiwa amejificha chini ya mfereji wa maji taka akiwa anavuja damu usoni.

Kijana mwenye umri wa miaka 21, Mohammed al-Bibi ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumuona Gaddafi akiwa amejificha kwenye mfereji wa maji taka. Mohamed alimtaarifu kamanda wa kikosi chake ambaye aliwaongoza wenzake kumtia mikononi Gaddafi. Tangu wakati huo, Mohamed amekuwa akionekana kama shujaa wa Libya.

Gaddafi alijisalimisha mwenyewe kwa waasi huku akiwaomba wasimuue huku akiwaambia "Haya mnayonifanyia ni haramu, mnatenda dhambi".

Hali hiyo ilipelekea baadhi ya wanajeshi wa NTC wamtandike na viatu usoni huku mwingine akiiba pete yake ya ndoa na mkewe iliyokuwa na maandishi "Safia 1970".

Baada ya purukushani ya kumtembeza mtaani, Gaddafi aliuliwa na mwili wake ulionekana baadae ukiwa na majeraha ya risasi kichwani na tumboni.

Baada ya habari za kukamatwa na kuuliwa kwa Gaddafi kusambaa duniani, mtoto wa kike wa Gaddafi, Aisha Gaddafi mwenye umri wa miaka 34 alijaribu kumpigia baba yake simu mara kadhaa lakini simu hiyo ilipokelewa na wanajeshi wa NTC.

Ripoti za televisheni nchini Jordan na Dubai zilisema kuwa Aisha aliwavurumishia matusi waasi kwenye simu akiwaita "Panya" jina ambalo baba yake alipenda kuwaita waasi wakati wote wa vita vya kuipindua serikali yake.

Wakati huohuo, familia ya Gaddafi imetaka ikabidhiwe mwili wake ili iweze kumuandalia mazishi ya heshima.

Wakati huohuo pia, majeshi ya NATO yametangaza kuwa yatasitisha harakati zao za kivita nchini Libya ifikapo oktoba 31


Marehemu Kanali Gaddaffi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni