Jumamosi, 8 Oktoba 2011

MBUNGE WA MBALALI AMEKAMATWA NA POLISI.


MBUNGE wa Mbarali (CCM), Modestus Kilufi amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kumtishia maisha mtendaji wa kata moja katika jimbo lake.Akizungumza kwa simu jana akiwa chini ya ulinzi wa polisi, mbunge huyo alisema alikamatwa akiwa jimboni kwake Mbarali na kusafirishwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya Mjini.

Mh.Modestus Kilufi

“Nimekamatwa na polisi. Wamekuja polisi wengi wakiwa na silaha na gari. Nilikuwa Mbarali na sasa wananipeleka Mbeya Mjini,” alisema Kilufi na kuongeza:

“Nimewauliza tatizo ni nini wakasema eti nimemtishia Ofisa Mtendaji wa Kata na nilipowauliza kwa nini hawakunipigia simu kwamba nahitajika kituoni hawakutaka kunisikiliza,” alisema.

Alisema anashangaa polisi hao kutompigia simu na kumweleza kuwa anatafutwa ili afike mwenyewe kwa kuwa yeye ni kiongozi na badala yake kwenda kumkamata Mbarali ili wampeleke Mbeya Mjini.

“Hayo ndiyo yamenikuta. Huyo mtu wanayesema nimemtishia maisha sijawahi hata kukutana naye tangu nimetoka bungeni, kwa sasa tupo maeneo ya Uyole ndiyo tunaelekea Mbeya Mjini, wako askari kama wanne, watano hivi, ngoja tukasikie kitakachotokea huko,” alisema mbunge huyo jana saa 11.45 jioni kupitia simu yake ya mkononi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Anaclet Malindisa alithibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo. Hata hivyo,  alisema ni mapema kueleza sababu za kukamatwa kwake hadi hapo mawasiliano yatakapofanyika.
Chanzo; Mwananchi Gazeti.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni