Alhamisi, 27 Oktoba 2011

MWEKEZAJI ATOROKA NA BILIONI 1.8 ZA LAPF.

MFUKO wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) umewachefua wabunge baada ya kubainika kupoteza Sh bilioni 1.8 kwa kukodisha hoteli ya Millenium Tower kwa kampuni ya kigeni ambayo hata anuani yake haijulikani.

Mwekezaji huyo kampuni ya GK Hotel and Resort, ambaye ametoweka bila kulipa fedha hizo, amebainika kuwa licha ya kukodishiwa hoteli, alipewa mkopo wa Sh milioni 500 za mtaji wa kuanzishia hoteli hiyo na LAPF.

Jengo la Millenium Tower linalomilikiwa na LAPF lililopo Kijitonyama.

Katika makubaliano yao, mwekezaji huyo aliahidi kurudisha mkopo na riba ya Sh milioni 721 ambazo nazo hakuzilipa hadi mkataba wake ulipovunjwa. Kana kwamba haitoshi, mwekezaji huyo hakulipa pango kwa kipindi chote ambacho aliendesha hoteli hiyo na hadi anaondoka, alikuwa anadaiwa Sh bilioni 1.1.

Fedha zote ambazo mwekezaji huyo anadaiwa na LAPF ni Sh bilioni 1.8 na sasa hivi mfuko huo unahaha kumpata huku akiwa ameshaondoka nchini na kurudi kwao Afrika Kusini.

Lakini LAPF jana ilikiri mbele ya Kamati ya Bunge, kuwa imeshindwa kupata anuani anazotumia Afrika Kusini.

Kashfa hiyo iliibuka wakati wa kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na mbunge wa kwanza kuibua suala hilo, Esther Bulaya, alisema ana uhakika kuwa baada ya deni hilo, bodi ya wadhamini ya mfuko huo, imeamua kulifuta.

Mbunge huyo pia alikwenda mbali na kudai kuwa anatambua mwekezaji huyo ni kiini macho bali kashfa ni mpango maridadi ulioandaliwa miongoni mwa vigogo wa LAPF ambao wanatumia fedha za wanachama kwa manufaa binafsi.

“Hizi ni fedha za wananchi, hatuwezi kukaa kimya katika suala hili.”

Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Sanga Eliud, katika kujibu hoja ya Mbunge huyo, alikiri kuwa mwekezaji huyo ametoweka nchini na sasa hivi wanafanya juhudi za kumtafuta Afrika Kusini ili wamfungulie kesi nchini.

Alisema kwa vile Mfuko umeshindwa kumpata, wameomba msaada ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia ubalozi wa Tanzania Afrika Kusini, ili watafute anuani ya mwekezaji huyo.

Mwanasheria wa LAPF Fidelis Rutakyamirwa, alipotakiwa na Kamati hiyo aeleze kilichopo, alisema baada ya LAPF kuvunja mkataba na mwekezaji, wawekezaji walikimbilia mahakamani wakitumia kampuni ya uwakili ya Mkono Advocates; lakini hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa baadaye kwa mwekezaji kuomba usuluhishi nje ya mahakama.

Baada ya kesi hiyo kufutwa, aliondoka. “Tunachofanya sasa tunaendelea kuitafuta kampuni hiyo Afrika Kusini, jitihada hizo bado hazijaa matunda licha ya kumtumia balozi wetu huko.”

Mwanasheria huyo alisema baada ya jitihada hizo kushindikana, sasa hivi wamewatumia Mkono Advocates ambao wamesaidia kuwapatia mawasiliano ya kampuni ya African Style ambao wana uhusiano naye kibiashara.

Baada ya hoja hizo, Mbunge wa Magomeni, Muhamad Amour Chomboh, alimhoji mwanasheria huyo: “Je una muda gani wa kazi hapo LAPF?” Akajibiwa “miaka mitatu.” Chomboh alihoji tena: “Wakati uongozi unaingia mkataba na mwekezaji huyo ulikuwapo?” Akajibiwa “Sikuwapo.”

Mbunge huyo alimgeukia Mkurugenzi na kumhoji kama alikuwapo wakati wa kutiliana saini mikataba hiyo? Akajibiwa: “Sikuwapo na wala Mwenyekiti wa Bodi hakuwapo.”
“Hili jambo linatia uchungu sana, yaani mnamkodisha mtu mwekezaji hamjui katoka wapi na wala hamjui hali yake ya kifedha!” Alishangaa Chomboh.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Esther Matiko alimhoji Mwanasheria wa LAPF: “Yaani mwanasheria unaongea kwa ujasiri haya mambo ya aibu hapa, hivi mnawezaje kuingia mkataba na mwekezaji wakati hamjui hata anuani yake?”

Swali hilo halikujibiwa na mwanasheria bali na Eliud ambaye aliingilia kati na kusema kilichofanywa na menejimenti yake ni kuchukua uamuzi mgumu wa kumwondoa na sasa wanafanya jitihada ili kumpata arudishwe nchini ashitakiwe.

Chomboh alihoji tena: “Hivi Mkurugenzi aliyeingia mkataba na mwekezaji huyo yuko wapi? Alijibiwa na Mkurugenzi kuwa “Kwa bahati mbaya alishafariki dunia.”

Licha ya madudu hayo ya awali, pia Kamati hiyo ilibaini kuwa mwekezaji wa sasa hivi kampuni ya Peacock ambayo iliingia baada ya mwekezaji wa awali kufukuzwa licha ya kuwa na miaka minne tangu aichukue hoteli hiyo, nayo inadaiwa zaidi ya Sh milioni 300 kama pango na haijalipa.

Lakini pia wabunge walitaka wapelekewe taratibu zilizotumika kuipangaisha kampuni hiyo, kwani kuna habari kuwa LAPF hawakufuata taratibu za zabuni.

Baada ya majadiliano hayo Kamati ya Bunge haikutaka kuendelea na kikao na Mfuko huo na wakawarudisha hadi watakapoandaa taarifa ya kina kuhusu mkataba, mkopo na mawasiliano yanayofanywa na GK Hotel & Resources.

Pia Kamati ilitaka kuona taratibu zilizotumika kuwaingiza Peacock na kwa nini mwekezaji huyo hataki kulipa deni la Sh milioni 351. Kamati hiyo ilitoa muda hadi Jumatatu Mfuko uwe umeshawasilisha maelezo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni