Ijumaa, 21 Oktoba 2011

YANGA YAPANDA NGAZI MOJA KUELEKEA KILELENI.

 Image






YANGA ya Dar es Salaam imezidi kunogesha mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuifunga Toto African mabao 4-2.

Kutokana na matokeo ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga sasa imefikisha pointi 18 na kupanda kutoka nafasi ya nne hadi ya tatu kwenye msimamo.

Azam FC iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu imeshuka kwa ngazi moja, ambapo Azam pia ina pointi 18, lakini inazidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga ipo mbele mchezo mmoja zaidi ya Azam.

JKT Oljoro inaendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19, huku Simba yenyewe ikiongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 24, ambapo zote zimecheza mechi kumi.

Katika mchezo wa jana, Yanga ambayo ina udugu wa kihistoria na Toto African ya Mwanza
ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao hayo yalifungwa na Haruna Niyonzima dakika ya nane, Kenneth Asamoah dakika ya 12 na Jerry Tegete dakika ya 21 yote yakifungwa kwa mashuti.

Toto iliyokuwa ikionekana kuzidiwa kipindi cha kwanza ilicharuka dakika za mwisho na kupata
bao dakika ya 82 mfungaji akiwa Mohammed Soud.

Wakati mashabiki wakiamini mchezo huo ungemalizika kwa matokeo hayo ya mabao 3-1, Asamoah aliongezea Yanga bao la nne dakika ya 85 kabla ya Soud naye kupachika la pili dakika
ya 89.

Yanga ingeweza kupata mabao mengi zaidi lakini umaliziaji haukuwa mzuri kwa kushindwa
kulenga lango kila walipokaribia golini.

Hali hiyo pia iliikumba Toto Africans ambayo kwa nyakati tofauti wachezaji wake Soud,
Phabian James na Bakari Kigodeko walishikwa na kigugumizi cha miguu walipomkaribia kipa
Yaw Berko
.

Wakati huohuo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria kesho kinatarajia
kumpa tuzo aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Imani Madega kutokana na mchango wake katika michezo.

Kwa mujibu wa Madega, Kitivo hicho cha Sheria, ambacho kinatimiza miaka 50 tangu
kuanzishwa kwake, kimepanga kutoa tuzo kwa wanafunzi waliosoma katika chuo hicho, ambao
wameshiriki katika maendeleo mbalimbali ya jamii.

Madega licha ya kuwa Mwenyekiti Yanga, pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (Corefa) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Akizungumzia kuhusu tuzo, Madega alisema amefarijika na hatua hiyo kwa kuwa hiyo ni
heshima kwake kwa kuwa wamepita wanafunzi wengi chuoni hapo lakini ni wachache ndiyo
watakaopokea tuzo hizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni