Ijumaa, 14 Oktoba 2011

TAKUKURU YABAINISHA UPUNGUFU KATIKA UGAWAJI VOCHA ZA PEMBEJEO.


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mbeya imetaja upungufu ilioubaini baada ya kufuatilia shughuli nzima ya ugawaji wa pembejeo za ruzuku kwa msimu wa kilimo uliopita.

Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Daniel Mtuka alisema hayo katika kikao chake na waandishi wa habari na kutaja upungufu uliobainika kuwa ni pamoja na baadhi ya wataalamu wakiwemo maofisa kilimo wilaya kulipwa kupitia dhana ya kujitolea.

Mtuka alisema kutokana na hali hiyo, ilikuwa rahisi mno kwa wataalamu na wajumbe wa Kamati kurubuniwa kwa kuwa wakati wakifanya shughuli hiyo, wanakuwa wakikabiliwa na changamoto nyingine ikiwemo za kushughulikia mahitaji ya familia zao.

“Utakuta mtu anajitolea kufanya shughuli hiyo inayogharimu fedha nyingi lakini nyumbani kwake wakati huo huo ana matatizo na pengine ya magonjwa na inakuwa rahisi kurubuniwa,” alisema.
Credits; Mwananchi Gazeti 


Kasoro nyingine zilizotajwa ni mawakala kutokuwa na mikataba na wengi wao kutokuwa na maduka ya pembejeo, huku walionayo wakiwa na maeneo tofauti na yale waliyoomba kutoa huduma.

Alisema pia imebainika kuwa elimu ya kutosha haikutolewa kwa wadau wote wa shughuli hiyo
kuanzia ngazi ya utawala hadi wakulima ambao walipaswa wapewe uelewa wa kutosha.

Elimu iliyopaswa kutolewa kwa mujibu wa Mtuka ni kuhusu ukweli kuwa pembejeo hizo hazitolewi kama zawadi kwao bali ni lengo la Serikali kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo.

Mbali na kasoro hizo, Mtuka alisema mbali na vyombo vya Dola kutopewa ushirikiano wa kutosha katika kufuatilia shughuli hiyo, pia havikupewa mwongozo maalumu ambao ungeviwezesha kutambua wakati wa kuanza ufuatiliaji.

Alisema ni vema Serikali ifuatilie kasoro hizo na kuzifanyia kazi iwapo inataka kazi hiyo iwe na tija ama sivyo wajanja wachache wataendelea kunufaika kwa kuwarubuni wahusika na kukwamisha lengo husika

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni