Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MAKALA. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MAKALA. Onyesha machapisho yote

Jumatano, 23 Mei 2012

MBOWE AKANA KUWAFUNDISHA UCHAWI AKINA NASSARI, MBILINYI NA WENZIE!!!!!!!

Mbowe, je Nassari na wenzake si kama watoto wanaofundishwa uchawi?

 DR. WILBROAD SLAA KATIBU MKUU WA CHADEMA



 MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA FREEMAN MBOWE

 GORDON KALULUNGA

MAJUMA kadhaa yaliyopita Tanzania na Dunia kwa ujumla imeduwazwa na ujasiri wa Mbunge kijana wa Jimbo la Arumeru Mashariki Nassari Joshua (Chadema) pale alipotamka kuwa yeye na chama chake wana mipango ya kujitenga na kuunda Taifa lao.

Taarifa hii licha ya kuwaudhi watanzania wengi wakiwemo viongozi wa chama hicho cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hasa Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe, lakini vijana wenzake ambao ambao wanajiita ‘’Makamanda’’ walinyosha vidole juu na kushangilia kana kwamba ni jambo jema sana kwa mustakabali wao na vizazi vyao.

Kutokana na matamshi ya Mbunge huyo maarufu kwa jina la ‘’Mheshimiwa’’, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa aliinuka na kukanusha vikali matamshi hayo huku akisema kuwa huo si msimamo wa chama hicho jambo ambalo kwa wazalendo walimsifu Mbowe kwa ujasiri wa kusimamia misimamo ya chama chake.

Miongoni mwa matamshi anayotuhumiwa kuyasema Nassari ni kumpiga marufuku Mkuu wa Nchi kukanyaga Arumeru na Kanda ya Ziwa, eti kwa kuwa maeneo hayo ni ya Chadema na wakati wowote watatangaza Rais wao kama ilivyokuwa Sudani Kusini. 
Mengine ni kumhusisha mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani na masuala ya uteuzi wa viongozi wa nchi unaofanywa na baba yake.


Baada ya kutoa matashi hayo jukwaani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisimama na kusema kuwa matamshi hayo si ya Chadema bali ni ya vijana hao wenye damu ya moto wa gesi na ni kauli zao binafsi na yeye haziungi mkono.

Hongera sana Freeman Mbowe kwa msimamo huo kuutangaza hadharani ili jamii iendelee kukiamini chama hicho cha siasa kuwa kinajali pia maslahi ya nchi kwa ujumla na hii kwangu ni mara ya pili kukusikia ukikanusha matamshi ya wabunge wa chama chako ikiwemo kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi(Sugu) alipotamka kuwa viongozi wote wa Serikali wanatakiwa kupopolewa mawe.

Natoa hongera kwa Freeman Mbowe kwasababu ya uwezo wako wa kujenga hoja za kitaifa kwa mustakabali wa Tanzania yetu na wala si chama chako au familia yako au kutafuta sifa ya kushangiliwa kwa kunyooshewa vidole juu ya anga kama ilivyo alama ya chama hicho na vingine duniani.

Lakini mbali na kukupongeza Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuna jambo linanitatiza kidogo labda kupitia makala haya nikitoa hoja naweza kupata ufafanuzi kuhusu kauli za wabunge wa chama chako, je kweli hakuna vikao rasmi ama visivyo rasmi ambavyo chama chako kinapanga mambo haya?

Hainiingii akilini kuwa chama chako na wabunge wa chama hicho huwa hamyazungumzi haya wanayoyaropoka majukwaani mengine katika majukwaa ambayo mnakuwa wote baada ya kutoka katika vikao vya ndani, je kweli vijana wako hao wanajianzia tu?

Mbowe hivi kweli unataka kuwaaminisha watanzania kuwa chama hiki cha siasa kikipata ridhaa kutoka kwa wananchi kuongoza dora katika chaguzi zijazo hawa ndiyo watakuwa Mawaziri au wakuu wa mikoa Tanzania?

Nina mengi ya kukuuliza lakini naona una majukumu mengi ya chama na kitaifa sijui kama waweza kujibu maswali haya ambayo wengine watayatafsiri kuwa ni maswali magumu kiuhalisia lakini ni maswali mepesi kisiasa.

Ninachoweza kukiamini ni kwamba kwa sababu mikutano ya hadhara hasa mnapokuwepo ninyi viongozi wa kitaifa kwa kila chama cha siasa hapa nchini Tanzania ni kwamba kwa sababu kunakuwa na vikao vya ndani na mmnajipanga kuwa nani akaseme nini na nani anaweza katika masuala yepi basi nalazimika kuamini kuwa yawezekana uliamua kumgeuka kijana wako baada ya kuona ametoboa alidari ya siri za vikao vyenu.

Naamini hivyo kwasababu Mbunge huyu kijana sidhani kuwa alikuwa amelewa alipokuwa amepanda jukwaani siku chache baada ya umma wa watanzania kupitia wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kumpa ridhaa ya kuwa mtumwa wao katika jimbo hilo.

Mbunge huyu namfananisha na mtoto mdogo ambaye huwa anafundishwa uchawi bila kupewa miiko ya wapi anaweza kuyasema masuala hayo ya kishirikina.

Ndiyo, Nassari ni sawa na mtoto ambaye anafundishwa ushirikina kwa sababu mifano hiyo ipo katika jamii zetu ambapo tumeshuhudia mahala pengi watoto wakitamka kuwa wanaruka na Bibi zao au wazazi wao huku wakifanya masuala ya kishirikina na wanapobainika kuwa wameanza kutoa siri hiyo wale wanaowafundisha huwa wanaiaminisha jamii kuwa watoto wao wanaropoka.

Nalazimika kueleza mfano huu ambao wengi wetu ni mashuhuda na ninaamini mfano huu inashabiiana sana na mfano wa matamshi ya Mbunge Nassari na Mbowe ambapo Nassari alisema kuwa chama chao kinataka kufanya hivyo, lakini Mbowe anasema kuwa huo si msimamo wa chama bali na wa vijana kana akina Nassari na chama chake hakihusiki..’’kufundishwa ushirikina na kuropoka’’ kisha mfundishaji anasema mtoto anaropoka.

Nieleweke wazi kuwa katika makala haya sielekezi moja kwa moja kidole kwa Mbowe na viongozi wenzake kuwa huo ni moja ya mipango ya chama chake. La hasha! Bali ni mtazamo mpana ambao kwa pamoja yatupasa tujiulize kuwa Je ni kweli Nassari aliropoka kuhusu kujitenga na kutamka Rais wa kanda ya Kaskazini?

Kama ni kweli kutoka katika sakafu ya moyo wa Mbowe na viongozi wakubwa wa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kuwa huo si msimamo wao na wala ule uhamasishaji wa Mbunge wa Mbeya mjini kuwa viongozi wa Serikali na familia zao wapigwe mawe, basi nakushauri Mbowe usiwashirikishe katika mambo makubwa vijana wako.

Kati ya vijana ambao nawashauri Chadema wasiwashirikishe katika vikao vikubwa ni pamoja na Mbunge Nassari Joshua, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), John Heche, Diwani wa zamani wa CCM Sombetini ambaye hivi karibuni alihamia Chadema, Alphonce Mawazo na Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Ally Bananga ambaye pia amejiunga Chadema.

Nashauri hivyo kwasababu yawezekana watu hawa bado vifua vyao havijakomaa kutunza mambo makubwa mnayoyapanga sawa na mtoto anayefundishwa uchawi na wazazi au walezi wake kisha dakika kadhaa anamwaga hadharani kwasababu hawawezi kuhimili na kudhani kuwa wakitamka hivyo hadharani basi wataonekana kuwa wamekomaa kisiasa huku wao mategemeo makubwa ni kupigiwa makofi.

Freeman Mbowe hivi kweli hakuna kikao chochote cha siri au cha dhahili ambacho chama chako kilikaa na kupanga mipango hiyo ya kihaini? Au ukweli wako unabaki pale pale kuwa Nassari aliropoka!!

Na kama Nassari aliropoka je unalijua kundi lake ndani ya chama chako kuwa yupo na nani nyuma yake ambao wana mipango ya namna hiyo? Na je unatambua kuwa tetesi nyingi za Tanzania mwisho wake unakuwa kweli? Basi Mwenyekiti kama haya ni magumu kiuhalisia hebu toa ufafanuzi vema kwa umma wa Watanzania hata kisiasa kuwa Nassari ameropoka na wala hakufundishwa ‘’uchawi’’ kama wanavyofanya watoto wengine.

Natoa hoja.!
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754-440749
source;http://www.kalulunga.blogspot.com/

Jumamosi, 19 Mei 2012

MAKALA YA SANAA NA UREMBO; MASHINDANO YA KUCHORA PICHA ZA WANAWAKE WANENE HUKO IVORY COAST.

Ni wanene na warembo

Jumatatu, 7 Novemba 2011

MIAKA 50 YA UHURU.

Meja Jenerali Said Kalembo akikagua gwaride la JKT Tanga.




INGELIKUWA SI MORALI NA UZALENDO KWA NCHI YETU TUSINGESHINDA VITA VYA UGANDA- MAJOR JENERALI MSTAAFU KALEMBO.

Burhani Yakub
YAPO mambo ambayo yanastahili kukumbukwa wakati huu tunapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru. Miongoni mwa mambo hayo ni vita vya Kagera (1978)Watanzania walianza kuingiwa na wasiwasi mwaka 1971, wakati Idd Amin Dada alivyoasi na kuchukuwa madaraka ya Uganda kwa nguvu baada kuungusha utawala halali wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Milton Obote na kutangaza kuitawala nchi hiyo kijeshi.


Mwanzo wa utawala wake Waganda pamoja na mataifa mengine walidanganyika, wakawa na matumaini makubwa juu ya kiongozi huyo wa kijeshi, kutokana na ahadi zake nyingi kwamba yeye ataitawala Uganda na kuhakikisha eneo lililoko Tanzania, sehemu ya mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi litakuwa sehemu ya Uganda.


Mwaka huo huo, Idi Amin alijaribu kutimiza madai yake kwa kuishambulia sehemu hiyo ya Mto Kagera, lakini Watanzania walikuwa imara katika kulinda ardhi yao, Amin akashindwa, baada ya majeshi yake kurudishwa nyuma na majeshi hodari ya Tanzania.


Pamoja na majeshi yake kurudishwa nyuma, Amin aliwapongeza wapiganaji wake kwa kurudishwa nyuma huku akiwasifia kupata jeraha kidogo kutoka kwa majeshi ya Tanzania.

Baada ya wapiganaji wake kurudishwa nyuma Idd Amin alisema huo ni mwanzo tu, awamu nyingine atatumia silaha nzito zaidi ikiwa ni pamoja na makombora ya kurushwa kwa ndege na kuwaongezea nguvu askari wa miguu, jambo ambalo liliwafanya Waganda kuingiwa na hofu kwamba kiongozi wao atawaingiza katika vita, wasiyojua faida yake.
Mnamo mwaka 1978 kulitokea vita kati ya nchi ya Tanzania na nchi ya Uganda, vita hii ilijulikana kwa jina maarufu la “vita ya Kagera” iliitwa jina hilo kutokana kwamba ilipiganiwa katika ardhi ya Tanzania mkoani Kagera. Vita hii
ilianza mara baada ya majeshi ya Uganda kuivamia Tanzania.


Idd Amin alianzisha tena chokochoko zake za kudai kuwa sehemu ardhi katibu na Mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi ni sehemu ya Uganda.Tanzania ikalazimika kuingia katika vita kuilinda ardhi yake.

Jumanne, 18 Oktoba 2011

SABABU 6 MBOVU ZA KWA NINI UINGIE KATIKA NDOA.

Watu wengi tumewaona kwenye ndoa wakiishi katika hali tofauti za maisha, wako wenye fedha na wasionazo, wako wenye furaha na wasio na wasionao.

Yote hii huweza kuchangiwa na sababu nyingi ikiwemo wanandoa hawa kujikuta wanaingia katika ndoa wakisukumwa na sababu zilizo mbovu na zisizo na msingi
Ziko sababu njema na nzuri za ndoa zinazoongelewa sana na wengi maeneo mbalimbali. Mimi nimejaribu kuzitafuta zile sababu zisizo nzuri ambazo wengine pasipokuwa makini wamezishikilia na kusiruhusu sababu hizi ziwasindikize katika ndoa na hivyo kujikuta wenajuta na kulia katika muda mwingi wa maisha.

Hii pia ni sababu ya ukweli kwamba siku hizi idadi ya ndoa zinazovunjika ni kubwa sana kuliko zamani. Hali ya kiwango cha kudhamiria (commitment) kwa wanandoa ni kidogo sana na hivyo kushusha uthamani wa ndoa zenyewe.

Sababu hizi zitakuwezesha kuubadili mtazamo ulionao juu ya ndoa na kukupelekea kubadili namna  unavyo sema au kuwaza au kutenda kuhusiana na suala zima la ndoa.

SABABU MBOVU

  1. Kuingia katika ndoa kwa lengo la kusaidiwa au kuongeza  kiwango cha kiuchumi ulicho nacho. Hapa wengine wamewageuza wapenzi wao kuwa mitaji au rasilimali ya kuwaondoa wao pamoja na ndugu zao kutoka kwenye umasikini.  Kwa kuthibitisha hili wengine  wamepewa majina kama BUZI, ATM n.k. Katika penzi la namna hii hakuna mguso au muunganiko wa kuhisia baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha pekee ni kile kilicho mfukoni. Athari za penzi la aina hii lina fungua milango mingi kwa wanandoa  kutokuwa  waaminifu na hata kujihusisha na mapenzi  nje ya ndoa.
  2. Hofu ya umri kupita na kuzeeka. Wako wengi sana, hususani watu wa wajinsia ya kike ambao wamejikuta wakiwakubali wanaume wa aina yoyote ili mradi tu nao waolewe maana umri wao ulionekana kusonga sana na hofu ya kutoolewa kutanda. Mwanaume anayehusiana na mwanamke mwenye tabia hii huulizwa au kulazimishwa kila siku kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa binti au kutangaza ndoa.  Ndoa nyingi za aina hii zimeishia kenye talaka na kutengana. Wako wengine ambao, kwasababu wanakiu sana ya kupata watoto na wameogopeshwa sana habari kwamba wana weza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, basi watacheka  na kaka yeyote yule ilimradi tu waolewe au wazae naye  Wengine wajinsi hii wamejuta sana baada ya kujikuta kuwa waliyezaa naye hakuwa BABA wa kweli bali kirukanjia tu na kwahiyo wameishia kulea mtoto au watoto wao wenyewe pasipo mzazi wa pili, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa  linawaathiri watoto wengi.  Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, kukumbuka kuwa hata huko kwenye ndoa kuna waliokosa watoto.
  3. Kuingia kwenye ndoa sababu ya mimba au mtoto aliyepatikana kabla ndoa. Lazima kutofautisha kuwa sababu iliyowapelekea kuzaa mtoto siyo itakayowapelekea kuoana.  Acha sababu ya kuoana kwenu iwe penzi lenu la dhati na sio mimba au mtoto. Suala hili linahitaji pia wazazi wajue kwamba kitendo cha watoto  kupeana mimba au kupata mtoto hakitoshi kuwa sababu ya kuwalazimisha kuoana, maranyingi wazazi wamewalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa sababu ya mimba au mtoto na kujikuta wanawaharibia maisha yao mazima.  
  4. Kulazimika kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya kudumu kwa sababu ya upweke, (Loneliness). Mara nyingi mtu anapokuwa peke yake (single) huwaza kuwa ndoa ndiyo inayoweza kuwa utatuzi mkubwa wa matatizo yake.  Nakubaliana na ukweli wa maandiko kwamba “Sio vema mtu awe peke yake…” lakini ni vizuri tukijua tofauti iliyopo baina ya kuwa peke yako na upweke.  Hivi ni vitu tofauti: kuwa peke yako inamaanisha kukosa mawasiliano au ukaribu na watu wengine, unakuwa kama uliyetengwa, wakati upweke (loneliness) inahusisha nafsi,  akili na hisia kuwa pweke au kujihisi kutengwa na hii ni ngumu kuishuhulikia.  Ni heri kuwa peke yako (single) kuliko kuwa  kwenye ndoa na bado ukajisikia upweke (lonely).  Wako wengine waliodhani ndoa ni suluhisho la upweke waliokuwa nao na mara walipoolewa au kuoa, mawasiliano baina yao yakayumba na hivyo kukomaza  upweke kwa wote wawili.
  5. Kuolewa au kuoa kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu au marafiki. Shinikizo hizi zaweza kuwa za kihisia au hata kihalisia.  Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi mara kwa mara kuoa sababu umri wako una pita na wako wazazi wengine husema wanataka wajukuu.  Hata kama huhisi  kulazimishwa lakini kwa kule kurudia rudia kwa kukumbushwa kila siku kunaathiri hisia zako na kuweza kukupelekea kuingia katika ndoa isiyopangiliwa.  Shinikizo ya kimwili au kihalisia ni pale wazazi wanopolazimisha watoto wao kuoa au kuolewa na watu fulani kwa sababu tu ni marafiki zao (family friends) au kwa sababu ya kulinda utajiri na matarajio yoyote binafsi.  Ndoa nyingi za aina hii zimekuwa kero na dimbwi la maumivu na machozi, baada ya muda kidogo mna jikuta mali mnazo, wazazi wenu wanapatana,  lakini nyie kama wapenzi ni maadui wakubwa.
  6. Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata uhuru. Hii hutokea sana kwa wale waliozoea kubanwa sana na wazazi katika kila wafanyacho hususani katika maamuzi. Wengine huzikimbia familia zao maana hazieleweki, hazina mpangilio na hivyo kutamani kutoka ili wakaanzishe zakwao wenyewe. Kinadada na kinakaka wanachoka kuamuliwa na kuwekewa masharti ya kuvaa, kula, kufanya mambo, kutoka na kurudi kwa muda kwahiyo wanadhani ndoa ndio itawachomoa kifungoni hapo.


MATOKEO YA KUINGIA KATIKA NDOA KWA SABABU MBOVU

Lengo la kuingia kwenye ndoa, liwe zuri au liwe baya ndilo litakalotegemeza aina ya maisha yenu katika ndoa hiyo kuwa ya furaha au ya machungu. Baada tu ya kuoana na huyo mtu wako kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka siyo mingi utaanza kuchoka na kutamani kutoka nje ya hiyo ndoa kwa maana baina yenu hakuna muunganiko wa kindani ya ndoa ya jinsi hii.  Na mara nyingi hali hii hupelekea msongo wa mawazo, mfadhaiko na kukosa furaha ndani ya ndoa.  Na matokeo ya hali hii kumfanya mwanandoa mmoja au wote wawili kuanza kutafuta kutoshelezwa na kuliwazwa nje ya ndoa na hapa vinazaliwa vitu kama uzinzi, kutengana na talaka.

Kwanini ndoa nyingi hushindwa?


Kwa sababu ya kukosa maarifa.

Wanandoa wengi hawajui nini wafanye, nini waelewe ili kufanya ndoa yao zifanikiwe. Thamani ya ndoa na jinsi ndoa inavyochukuliwa siku hizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu, na hii imewafanya wengine kujikuta wako wenye ndoa kwa sababu mbovu na hivyo ndoa nyingi kuvunjika au kuyumba baada ya muda mfupi tu. Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu sio vya maana tena siku hizi, sababu watu wanaogopa kuonekana wa zamani na washamba. Mtazamo wa ulimengu juu ya ndoa umeharibiwa na magazeti, luninga na vitabu mbali mbali.

Siku hizi kuishi bila ndoa ni kitu cha kawaida, kuwa na mpenzi nje ya ndoa sio kitu cha kutisha tena,  mapenzi nje ya ndoa sio ya kushangaza hata kidogo.  Kinyume chake ukionekana kuyashangaa haya, jamii itakushangaa wewe kwa jinsi ulivyo nyuma ya wakati.

Mambo yamebadilika sana. Zamani binti akikutwa bikira wakati anaolewa ilikuwa sifa kwake na familia nzima, siku hizi binti akikutwa bikira atachekwa, na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani. Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya sana  tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa kweli na kudhamiria katika ndoa. Jamii isiyoamini katika uaminifu, na ndiyo maana magomvi mengi hutokea pale simu ya mmoja inapoguswa.  Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili sio jambo la kuzingatiwa tena.  Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya moyoni na walio umizwa, kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao wakitafutatafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili  waliwazane.

Kwa haraka tuangalie sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie katika ndoa na usijute:-

-  Ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja
-  Ni nafasi ya wawili hawa kuonyeshana mapenzi  yao
-  Nafasi ya kutimiziana mahitaji ya mwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi, na mtu sahihi, kwa maadili.
-  Hamu na kiu ya kutengeneza familia yenu.
-  Kutimiza kiu ya kuwa pamoja kwa umoja (companionship)
-  Nia au kusudi la kushiriki vyote kwa pamoja . Kufanya kutenda kwa pamoja ili kutimiza mahitaji yetu wote.
-  Nafasi ya kutumia kwa manufaa kila uwezo na vipawa mlivyokuwa navyo.
-  Kuchangiana katika makuzi yenu ya ujumla, makuzi ya kimwili, kiriho, kihisia n.k

Imeandikwa na:
Chris Mauki
Counselor and Social Psychologist
University of Dar es Salaam
0777 407182, chriss@udsm.ac.tz

[cross-posted toka SamSasali. "Papaa" blog]



source: http://www.wavuti.com/

Jumanne, 4 Oktoba 2011

VITA KUU YA DUNIA NA VUGUVUGU LA UHURU WA TANGANYIKA.

Askari wa Tanganyika waliopigana vita vya kwanza vya dunia, wakati huo Tanganyika ikiwa chini ya Mjerumani




Na Lawrence Kilimwiko
BAADA ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia, huku takriban watu milioni 56 wakiwa wamegeuka makaburi, juhudi kubwa ilielekezwa katika kujenga amani na kuzuia vianzio ambavyo vingepelekea kuzuka upya vita.

Moja ya mambo ambayo hapana shaka yangelipelekea dunia kurudi katika vita, ilikuwa ni suala la ukoloni na makoloni. Hii ni pamoja na kwamba licha ya kumalizika kwa vita, mataifa ya ulaya bado yalipenda kung’ang’ania makoloni yake barani Afrika , Asia na Amerika ya Kusini.
Na kwa kuwa yalikuwa yako taabani baada ya kugharamia vita, yaliekeza nguvu zake katika kuyakamua makoloni ili yaweze kujijenga upya. Mbinu zilizotumika katika kurekebisha uchumi ulioparaganyika kutokana na vita, ikawa ni  kuimarisha unyonyaji kwenye makoloni.
Ukatili mkubwa ukatumika katika kuhakikisha kuwa makoloni haya yanazalisha ziada. Sheria kandamizi zisizojali ubinadamu zikatungwa kwa mijali ya kufanikisha azma ya kufufua uchumi wa ulaya chini ya usimamizi wa askari.
Kwa sababu hiyo, wananchi wa asili katika makoloni haya walijikuta katika mateso makubwa ambayo dawa pekee ilikuwa ni kuuasi utawala wa kikoloni kwa gharama zo zote.
Wakati huo huo. ilitokea kwamba Amerika,  taifa  ambalo halikuathirika na vita liliibuka kuwa lenye nguvu na ushawishi mkubwa kuliko yote duniani. Itakumbukwa kwamba, wakati vita vikipiganwa, Amerika ilipata faida kubwa kutengeneza silaha pamoja na vyakula na kuziuzia nchi zilizokuwa vitani kwani vita vya panzi ni furaha kwa kunguru.
Kwa mtindo huo, wakati mataifa mengine yote yakiwa taabani, Amerika ilikuwa inaelea kwenye lindi la utajiri  usio kifani.
Amerika ikatumia fursa hiyo, kuandaa mkakati wa amani duniani ikiwa ni pamoja na kusimamia uundwaji wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani,maarufu kama IMF na pia kuhakikisha kuwa sarafu ya Amerika , yaani Dola, ndiyo inayokuwa kigezo cha kubadilisha sarafu zingine katika biashara ya kimataifa.
Kama hiyo haitoshi, Amerika ikahakikisha kwamba makao makuu ya Umoja wa Mataifa na yale ya  Benki ya Dunia na IMF yote yanakuwa nchini Amerika. Zaidi ya hapo, taifa hilo lenye nguvu duniani, likahakikisha kuwa, wakati wote Rais wa Benki ya Dunia atakuwa ni raia wa nchi hiyo ilhali Mkurugenzi  wa IMF atoka katika bara la Ulaya.Kwa njia hii, mfumo mzima wa uchumi  wa dunia na biashara vikasimikwa kukidhi matakwa ya America.