Jumatatu, 7 Novemba 2011

MIAKA 50 YA UHURU.

Meja Jenerali Said Kalembo akikagua gwaride la JKT Tanga.




INGELIKUWA SI MORALI NA UZALENDO KWA NCHI YETU TUSINGESHINDA VITA VYA UGANDA- MAJOR JENERALI MSTAAFU KALEMBO.

Burhani Yakub
YAPO mambo ambayo yanastahili kukumbukwa wakati huu tunapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru. Miongoni mwa mambo hayo ni vita vya Kagera (1978)Watanzania walianza kuingiwa na wasiwasi mwaka 1971, wakati Idd Amin Dada alivyoasi na kuchukuwa madaraka ya Uganda kwa nguvu baada kuungusha utawala halali wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hayati Milton Obote na kutangaza kuitawala nchi hiyo kijeshi.


Mwanzo wa utawala wake Waganda pamoja na mataifa mengine walidanganyika, wakawa na matumaini makubwa juu ya kiongozi huyo wa kijeshi, kutokana na ahadi zake nyingi kwamba yeye ataitawala Uganda na kuhakikisha eneo lililoko Tanzania, sehemu ya mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi litakuwa sehemu ya Uganda.


Mwaka huo huo, Idi Amin alijaribu kutimiza madai yake kwa kuishambulia sehemu hiyo ya Mto Kagera, lakini Watanzania walikuwa imara katika kulinda ardhi yao, Amin akashindwa, baada ya majeshi yake kurudishwa nyuma na majeshi hodari ya Tanzania.


Pamoja na majeshi yake kurudishwa nyuma, Amin aliwapongeza wapiganaji wake kwa kurudishwa nyuma huku akiwasifia kupata jeraha kidogo kutoka kwa majeshi ya Tanzania.

Baada ya wapiganaji wake kurudishwa nyuma Idd Amin alisema huo ni mwanzo tu, awamu nyingine atatumia silaha nzito zaidi ikiwa ni pamoja na makombora ya kurushwa kwa ndege na kuwaongezea nguvu askari wa miguu, jambo ambalo liliwafanya Waganda kuingiwa na hofu kwamba kiongozi wao atawaingiza katika vita, wasiyojua faida yake.
Mnamo mwaka 1978 kulitokea vita kati ya nchi ya Tanzania na nchi ya Uganda, vita hii ilijulikana kwa jina maarufu la “vita ya Kagera” iliitwa jina hilo kutokana kwamba ilipiganiwa katika ardhi ya Tanzania mkoani Kagera. Vita hii
ilianza mara baada ya majeshi ya Uganda kuivamia Tanzania.


Idd Amin alianzisha tena chokochoko zake za kudai kuwa sehemu ardhi katibu na Mto Kagera, katika mkoa wa Ziwa Magharibi ni sehemu ya Uganda.Tanzania ikalazimika kuingia katika vita kuilinda ardhi yake.

Amiri Jeshi Mkuu, Mwalimu Julius Nyerere akayaamuru majeshi ya Tanzania kuikomboa na kuilinda ardhi ya Tanzania.
Meja Jenerali Said Kalembo pamoja na wanajeshi wenzake wakalazimika kuingia vitani kulinda mipaka ya Tanzania na anaeleza;‘Vita ile dhidi ya Idd Amin ilinipa funzo kubwa sana kwani tuliweza kuyashinda majeshi ya Uganda ambayo yalikuwa yametuzidi kwa silaha za kisasa, ndege, magari na ndege za kali za kivita na mafunzo ya kivita ya muda mrefu ya askari wake lakini sisi tuliweza kushinda.
“Ninapoikumbuka vita ya Uganda, namkumbuka sana Mwalimu Nyerere na hili ningependa iwe ni sehemu ya Watanzania kuadhimisha miaka 50 kwa kumuenzi vyema baba wa Taifa alikuwa sehemu kubwa ya ushindi wetu.
“Siri ya ushindi wetu dhidi ya majeshi ya Idd Amin nchini Uganda ilitokana na muundo wa jeshi letu ambalo Mwalimu Nyerere aliliunda kwa mfumo wa kuwa ni la wananchi,yaani jeshi la kuwasaidia wananchi na siyo adui kama ilivyo kwa majeshi ya nchi nyingine.
 “Askari wetu kila kijiji na miji walipokuwa wakiingia Uganda kupigana na majeshi ya Idd Amini, walikuwa wakipokewa kwa shangwe kutokana na ukweli kwamba sisi tulikuwa tukifanya kazi ya kushambulia wakati huo huo tukiwasaidia wananchi wa vijiji vya Uganda kwa matibabu na hata misaada mingine ya kibinadamu.
“Aina hii ya jeshi tuliichukua kutoka China kwani Mchina anaamini kuwa jeshi la wananchi ni kama samaki na maji,bila maji samaki hawezi kuishi,” anaeleza Kalembo
“Aina ya upiganaji wetu iliwashangaza wananchi wa Uganda wakaona kumbe sisi si adui wao kwani tofauti baina yetu na jeshi la Uganda ni kuwa askari wake walikuwa ni wanyanyasaji na wababe kwa watu wao.
 “Jambo hili lilitusaidia sana kwani kila tulipokuwa tukifika, wananchi walikuwa wakitushangilia na kutupa siri za majeshi ya Idd Amin walikuwa wakituonyesha sehemu zote walizokuwa wakijificha hivyo ikawa rahisi kwetu kuwashambulia,” Kalembo anasimulia.
Hotuba ya Mwalimu Nyerere.
“Siri nyingine  ya ushindi wetu ilitokana na maneno aliyoyatoa Mwalimu Nyerere wakati akilihutubia taifa kuelezea juu ya Tanzania kuvamiwa ardhi yake na Idd Amini.
“Akiwa amiri jeshi mkuu, Mwalimu Nyerere alitoa hotuba ambayo sisi askari ilitupa nguvu ya kwenda vitani na hata tulipokuwa mstari wa mbele tulipokumbuka maneno ya hotuba ile tulipata ari na nguvu ya kuongeza mashambulizi dhidi ya adui na hatimaye tukapata ushindi.”
“Katika hotuba yake Amiri jeshi mkuu alisema hivi “Idd Amini amevamia ardhi ya nchi yetu, kazi yetu ni moja tu ya kumuondoa na kuhakikisha ardhi yetu iko salama, Nia ya kumpiga tunayo, sababu ya kumpiga tunayo, uwezo wa kumpiga tunao, tunataka dunia ituelewe.”
“Maneno haya ya Amiri jeshi yalitupa moyo mkubwa wa uzalendo wa kuipenda na kuitetea nchi yetu kwa nguvu zetu zote, yalisababisha tupigane kwa kujitoa tukiamini kuwa tunapigania nchi yetu kwa lengo la kuikomboa kutoka kwa mvamizi,
“Baadhi ya mambo ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere ambayo yalionyesha kipaji chake halisi ni namna alivyokuwa na uwezo wa kutoa hotuba zenye kuhamasisha na kuwapa moyo wananchi wake,” anaeleza Kalembo.
“Kutokana na uzalendo wa kuipenda nchi yao, wananchi wa Tanzania walijitolea mali zao kwani wapo waliotoa mabasi, malori na misaada mingine ya hali na mali ili iweze kwenda kuwasaidia askari waliokuwa vitani, huu ni morali wa hali ya juu wa kuipenda nchi ambao kwa kipindi hicho ulikuwapo.”
“Kama si mambo hayo niliyoyataja, ingekuwa vigumu sana kwa jeshi la Tanzania kushinda kwani ikilinganishwa na wenzetu wa Uganda, jeshi la Idd Amini lilikuwa limepata mafunzo ya kijeshi ya kivita kwa mbinu za kisasa kwa wakati ule, ilikuwa na vifaa vya kivita vya kisasa kama ndege za kwenda kwa kasi, vifaru na mizinga ya kushambulia kwa umbali wowote,” Kalembo anasimulia.
Aprili 1979 vita ilimalizika baada ya majeshi ya Tanzania kumuondoa Idd Amin

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni