Ijumaa, 4 Novemba 2011

MOSHA WA YANGA ATOA ZAWADI YA MILIONI 10 KWA KUIFUNGA SIMBA.




Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Yanga S C, Davies Mosha.
 FURAHA ya wachezaji wa Yanga kuifunga Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya soka nchini, ilinogeshwa zaidi jana baada ya kupewa na zawadi ya sh10 milioni toka kwa Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Davies Mosha.
Mosha alitoa pesa hizo kutimiza ahadi yake kwa wachezaji wa Yanga aliyoitoa kabla ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, ambapo Simba walikubali kipigo cha bao 1-0.
Fedha hizo zilikabidhiwa na mpenzi na mwanachama wa Yanga, Abel Mcharo kwa niaba ya Mosha, ambaye hakuwepo kwenye hafla ya makabidhiano.
"Nimetumwa na Mosha kukabidhi fedha hizi (Sh10 milioni) kama utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa wachezaji iwapo wangeifunga Simba," alisema Mcharo.

Ncharo alisema Mosha ametoa pesa hizo kwa moyo mkunjufu, na zaidi akisukumwa kufanya hivyo kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo kwa klabu hiyo.
"Ameniagiza niwape ujumbe wanachama wa Yanga kuwa, zawadi hii imebeba tafsiri moja tu ambayo ni pongezi kwa wachezaji kutokana na ushindi dhidi ya Simba, na haina sababu wala malengo tofauti na alivyokusudia," alisema Mcharo.
Mcharo aliwaasa wanachama Yanga waache kuangalia walikotoka na badala yake, taswira yao ya sasa iwe mahali walipo na wanakoelekea kwa maslahi ya klabu.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga Ally Mayay, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa klabu, alisema jukumu alilojitwishwa Mosha ni mfano wa kuigwa.
"Ni vizuri wanachama wengine wakaiga mfano wa Mosha. Ameonyesha ni kwa jinsi gani alivyo na mapenzi ya dhati na klabu yetu," alisema.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya wachezaji, kocha wa timu hiyo, Kostadin Papic alisema pesa hizo ni 'mtaji' wa morali kwa wachezaji katika kujituma uwanjani kutafuta ushindi.
Katika hatua nyingine hafla hiyo ya kukabidhi fedha hizo nusura isifanyike baada ya chanzo kimoja cha habari kudai kuwa mmoja wa kiongozi wa juu wa Yanga alitaka fedha hizo zikabidhiwe kwanza kwao tofauti na ilivyofanyika.
Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu baina viongozi wenyewea klabu hiyo muafaka ulifikiwa na fedha hizo zikakabidhiwa kwa wachezaji, huku uongozi ukiwepo kwa ajili ya kushuhudia tu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni