Jumatano, 30 Novemba 2011

RAIS KIKWETE ATIA SAINI MSWADA WA KUUNDWA TUME YA KURATIBU UUNDWAJI WA KATIBA MPYA.

RAIS Jakaya Kikwete ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Kikwete alisaini muswada huo jana, ikiwa ni siku 11 tangu upitishwe na Mkutano wa Tano wa Bunge la 10 mjini Dodoma, Novemba 18, mwaka huu.

Hatua hiyo ya Rais kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo.

“Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

“Pamoja na kutiwa saini hiyo, bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.

“Hivyo, Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasikiliza na kuchukua hatua zipasazo,” iliongeza taarifa hiyo ya Ikulu.

Aidha, Rais Kikwete ametia saini Muswada huo siku moja baada ya kuwa amekutana kwa siku mbili mfululizo na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao waliomba wakutane naye na kuzungumza kuhusu Muswada huo wenye kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Jumapili na Jumatatu, Rais Kikwete na baadhi ya watendaji wake na Chadema kwa upande mmoja, walikuwa na mazungumzo kuhusu Muswada huo ambao ulipitishwa na Bunge bila ushiriki wa wabunge wa Chadema na wa NCCR-Mageuzi ambao walisusa.

Kususia mjadala wa Muswada huo kwa wabunge hao wa vyama hivyo, ulitokana na madai yao ya kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni wakidai haukuwa umesomwa na wananchi na kuuelewa, hivyo kukosa kuuchangia, lakini walikataliwa na Spika Anne Makinda.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa Ikulu juzi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutakuwa na haja ya sheria hiyo baada ya kusainiwa kuendelea kuboreshwa, ili ikidhi mahitaji ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.

Pia kutakuwa na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Awali ilielezwa kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya uelewano ambapo Rais Kikwete aliwahakikishia Chadema kuwa yeye na Serikali yake wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.



Makubaliano ya juzi, yalimaliza sintofahamu iliyokuwa imeanza kuibuka kwa Chadema na makundi mengine kutaka kufanya maandamano nchi nzima, kupinga Muswada huo kusainiwa na kushinikiza urejeshwe bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza.

Lakini pia kunatoa fursa pana kwa wawakilishi na wabunge kurudi kwa wananchi kuwahimiza kujitokeza kutoa maoni na mawazo yao kuhusu aina ya Katiba inayotakiwa na Watanzania wote.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa ni jambo muhimu kwa mchakato huo kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Wakati huo huo, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Jakaya Kikwete na Chadema yamepongezwa na wasomi na kupingwa na wanaharakati.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, amesema makubaliano hayo, ni mchakato wa kisiasa ambao matokeo yake pia yatakuwa ni ya kisiasa.

Bana alisema wananchi waone kama ni mambo ya kisiasa na matokeo yake yanaweza kutokea kinyume na matarajio ya wengi “Ndiyo maana nasema ile ni siasa.”

Alisema kwa vile Serikali ina taratibu zake za utendaji na kwa kuwa kikao cha Chadema na Rais si kikao rasmi cha kiserikali, uamuzi wake unaweza kuwa kinyume na matarajio ya wengi.

Hata hivyo, msomi huyo alisema mkutano huo umeonesha nia njema ya Rais ya kutaka kuona mchakato wa Katiba unaendeshwa kwa maridhiano na kusiwepo kudharauliana.

Pia alisema kitendo cha Chadema kuomba kukutana na Rais na ikafanikiwa, imepandisha umaarufu na hadhi ya chama hicho. Kilichobaki ni namna ambavyo watatafsiri matokeo ya kikao hicho.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema kitendo cha Rais kukubali kukutana na Chadema ni dalili nzuri kuwa amesikiliza kilio cha wengi wanaopinga Muswada wa mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, Nkya alionesha wasiwasi kuhusu msimamo wa Ikulu kuwa Rais Kikwete atasaini Muswada huo na kueleza kuwa kuna uwezekano msimamo huo ukafanya maoni ya wananchi wengi yasisikilizwe.

Alisema Rais angesikiliza vyama vyote vya siasa na umma wa Watanzania na kufanya uamuzi ambao lazima uendane na ambacho wananchi wengi wanataka.

“Rais yuko juu ya vyama vya siasa na kila jambo analofanya ni lazima atangulize maslahi ya umma,” alisema. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye ni
miongoni mwa wabunge waliosusa mjadala wa Muswada huo, alisema ameshituka baada ya kusoma makubaliano ya kikao hicho.

“Kile kilikuwa ni kikao kikubwa, nilitarajia Rais akubaliane na kilio cha wengi cha kutosaini Muswada huo, lakini nimesikia atausaini kinyume cha maombi ya wananchi wengi,” alisema
Kafulila.

Mbunge huyo alisema aliamua kutoka nje ya Bunge kwa vile alishaona CCM na Serikali yake, hawana dhamira ya dhati ya kusikiliza kilio cha wananchi cha kutaka mchakato wa Katiba uwashirikishe.

“Walishaamua mchakato huu uhodhiwe na mfumo wa chama chao na si kuupa nafasi umma wa Tanzania,” alisema Kafulila na kuongeza kuwa malengo ya wabunge kutoka nje hayakuwa ya kukutana na Rais, bali kupinga CCM kuhodhi mchakato wa kutunga Katiba mpya.

Alisema mkutano wa Chadema na Rais ungekuwa na mafanikio kama ingeamriwa kuwa Rais asisaini Muswada huo hadi wananchi wapate fursa ya kutoa maoni, baada ya Muswada huo
kutafsiriwa kwa Kiswahili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni