Jumatatu, 21 Novemba 2011

EWURA-BEI YA PETROLI YASHUKA DIZELI YAPANDA.

WAKATI bei ya petroli imeshuka dizeli na mafuta ya taa yamepanda, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza jana.


Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu imeonyesha kuwa petroli imeshuka kwa Sh22.86 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 1.12 na dizeli imepanda kwa Sh51.23 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 2.58 huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh46.45 kwa lita sawa na asilimia 2.35.


“Mabadiliko haya ya bei za mafuta hapa nchini yametokana na kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia na kupanda kwa bei ya dizeli na mafuta ya taa katika soko la dunia. Pia kushuka kwa shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani,” alieleza Masebu katika taarifa yake.


Alisema kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani alimradi ziwe chini ya bei ya kikomo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa ni Sh2,020, dizeli Sh2,034 na mafuta ya taa Sh2,021.


Jijini Arusha petroli itakuwa ikiuzwa kwa Sh2,104, dizeli itakuwa Sh2,118 na mafuta ya taa Sh2,105. Mbeya petroli itakuwa ikiuzwa kwa Sh2,127, dizeli 2,141 na mafuta ya taa yatakuwa ni Sh2,128. Mwanza petroli itauzwa kwa Sh2,170, dizeli Sh2,184 na mafuta ya taa Sh2,171.


Wiki mbili zilizopita Ewura, ilitangaza kupanda kwa bei ya petroli kwa Sh49.17, dizeli Sh2.69 na mafuta ya taa kwa Sh19.43. hadi jana, petroli ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,043, dizeli Sh1,983 na mafuta ya taa Sh1,975

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni