Jumatano, 30 Novemba 2011

HUKUMU KESI YA JERRY MURO NA WENZAKE KUTOLEWA LEO.

BAADA ya kesi inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake kuunguruma kwa zaidi ya mwaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo inatarajiwa kuhitimishwa kwa kutolewa hukumu.

Muro na washitakiwa wenzake Deogratius Mgasa na Edmund Kapama, wanadaiwa katika kesi hiyo kuomba na kutaka kupokea rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Michael Wage.

Kwa mara ya kwanza, Muro, Kapama na Mgasa walipandishwa kizimbani Februari 5, mwaka jana na kusomewa mashitaka yao na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Boniface Stanslaus akisaidiana na mwendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincolin mbele ya Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe.



Washitakiwa hao baadaye waliachiwa kwa dhamana ya kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika na hivyo kuendelea kufika mahakamani wakati kesi ikiendelea.

Juni mwaka jana, upelelezi wa kesi hiyo ulikamilika ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa utakuwa na mashahidi 11 ambapo Wage akiwa mmoja wa mashahidi hao.

Katika maelezo ya awali, Muro alidaiwa kujitambulisha kama kapteni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania pamoja na kuwatambulisha washitakiwa wenzake kuwa ni vigogo wa Takukuru.


Alidaiwa Juni mwaka jana, alimpigia simu Wage akimtaka aje jijini Dar es Salaam, kwani ana tuhuma dhidi yake anataka kuzitoa kwenye kipindi chake cha Usiku wa Habari.

Alidaiwa pia akiwa na wenzake walimtisha Wage na kumuomba rushwa hiyo ambapo siku waliyopanga Wage akampatie Muro, alitoa taarifa Polisi walifika eneo la tukio na kumkamata Muro na baadaye Kapama na Mgasa walitafutwa na kukamatwa pia.

Baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao, Machi 9, mwaka huu, Hakimu Mirumbe aliwakuta na kesi ya kujibu washitakiwa wote watatu na hivyo kutakiwa kuanza kujitetea Machi 29, mwaka huu.

Baada ya utetezi, mahakama hiyo ilipokea majumuisho ya pande zote mbili na kupanga siku
ya leo kutoa hukumu.

Kesi hiyo inasikilizwa kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mgeta

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni