Alhamisi, 24 Novemba 2011

MFANYAKAZI TRA KORTINI KWA WIZI SHILINGI MIL. 944/-

T R A Boss, Mr. Kitilya.
MFANYAKAZI wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sangu John amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka 132 akidaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 944, mali ya mwajiri wake kwa njia za udanganyifu pamoja na kulipa mishahara hewa.


Mashitaka hayo alisomwa jana mbele ya Hakimu Aloyce Katemana na mawakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon, Osward Tibabyekomya wakisaidiana na Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro.


Mashitaka yalikuwa ni ya kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wake, kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kusababisha hasara kwa mamlaka hiyo ya Sh 944,169,330.


Katika mashitaka ya kwanza, John alidaiwa Juni 19, 2006 katika ofisi za TRA Makao Makuu Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya, alighushi orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi huo, akionesha wafanyakazi hewa tisa wa shirika hilo walitakiwa walipwe Sh 12,000,000 huku akijua si kweli.


Katika mashitaka ya kutumia nyaraka kumpotosha mkuu wake wa kazi, alidaiwa mojawapo ni Juni 20, 2006 katika ofisi za TRA akiwa mwajiriwa, aliwasilisha orodha hiyo kwa mkuu wake wa kazi akidai kwamba wafanyakazi hao walitakiwa kulipwa fedha hizo huku akijua sio kweli.


Mashitaka mengine alidaiwa kwa nia ya kudanganya ambapo alijipatia kutoka Benki ya NBC fedha hizo akijidai kuwalipa watu hao kwa mshahara wa Juni 2006. Katika mashitaka, mengine alidaiwa kudai malipo hayo hewa miezi mingine kuanzia Juni 2006 hadi Agosti 2009.


Mashitaka mengine John alidaiwa alighushi nyaraka kuonesha mishahara ya wafanyakazi wa TRA, Novemba ni Sh 2,207,122,430 akijua sio kweli, alidaiwa kuendelea kumdanganya mwajiri wake katika miezi mingine katika kipindi hicho akionesha mishahara tofauti na iliyokuwa ikistahili wafanyakazi wa TRA kwa mwezi.


Aidha, mshitakiwa huyo alishitakiwa pia kwa kufanya mchezo huo aliisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndio ilikuwa mwajiri wake Sh 944,169,330.


Alikana mashitaka yote na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa nusu ya fedha hiyo, Sh 472,084,665. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Desemba 5, mwaka huu na upelelezi haujakamilika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni