Jumatano, 9 Novemba 2011

DK SLAA ASHITAKIWA KWA KUTOA MANENO YA UCHOCHEZI KUWA WATAANDAMANA KUMTOA RAIS KIKWETE MADARAKANI.























Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, akishuka kutoka kwenye Karandinga la Polisi, kusomewa mashitaka yanayomkabili na washitakiwa wengine 26 waliofikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa kosa la kufanya mkusanyiko kinyume na sheria. Picha na Filbert Rweyemamu.

Mahakamani
Dk Slaa, Lissu na wafuasi wengine 25 wa Chadema walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka matatu tofauti likiwamo la uchochezi ambalo linamkabili Dk Slaa pekee.
Viongozi hao wa Chadema na wafuasi wao, walifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa polisi majira ya saa nane mchana na kesi hiyo ilianza kutajwa mahakamani saa 9:00 alasiri.

Wakili wa Serikali, Haruna Matagane alisema watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali usiku wa Novemba 7, mwaka huu na saa 12 asubuhi Novemba 8, mwaka huu licha ya kutakiwa kutawanyika na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Mvulla.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Devota Kamuzora, mwendesha mashtaka huyo alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walikaidi amri halali ya SSP Mvulla kinyume cha sheria walipotakiwa kutawanyika.

Alisema Dk Slaa anashitakiwa kwa kosa moja pekee la kutoa maneno ya uchochezi kinyume na sheria mnamo Novemba 7, mwaka huu saa 11:30 jioni.

“Tunatoa muda ifikapo saa kumi na moja jioni wanataka kumpeleka kwa ndege Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji kwa IGP Said Mwema ili wampangie wilaya nyingine ya kuhamia,” Matagane alisema akinukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Dk Slaa.
Wakili huyo wa Serikali alisema Dk Slaa pia anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kutaka Lema atolewe Kisongo ifikapo saa kumi  jioni la sivyo kutakuwa na maandamano ya kumtoa Rais Jakaya Kikwete madarakani.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mawakili wa utetezi, Method Kimomogoro na Arbert Msando waliomba watuhumiwa hao wapatiwe dhamana kwa kuwa yanaruhusu kufanya hivyo ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Kamuzora akiwataka washtakiwa wote kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja kuweka ahadi ya kiasi cha Sh5 milioni.Watuhumiwa 20 wakiwamo viongozi walipata dhamana na kesi yao imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu
.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni