Jumatano, 23 Mei 2012

MBOWE AKANA KUWAFUNDISHA UCHAWI AKINA NASSARI, MBILINYI NA WENZIE!!!!!!!

Mbowe, je Nassari na wenzake si kama watoto wanaofundishwa uchawi?

 DR. WILBROAD SLAA KATIBU MKUU WA CHADEMA



 MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA FREEMAN MBOWE

 GORDON KALULUNGA

MAJUMA kadhaa yaliyopita Tanzania na Dunia kwa ujumla imeduwazwa na ujasiri wa Mbunge kijana wa Jimbo la Arumeru Mashariki Nassari Joshua (Chadema) pale alipotamka kuwa yeye na chama chake wana mipango ya kujitenga na kuunda Taifa lao.

Taarifa hii licha ya kuwaudhi watanzania wengi wakiwemo viongozi wa chama hicho cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hasa Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe, lakini vijana wenzake ambao ambao wanajiita ‘’Makamanda’’ walinyosha vidole juu na kushangilia kana kwamba ni jambo jema sana kwa mustakabali wao na vizazi vyao.

Kutokana na matamshi ya Mbunge huyo maarufu kwa jina la ‘’Mheshimiwa’’, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa aliinuka na kukanusha vikali matamshi hayo huku akisema kuwa huo si msimamo wa chama hicho jambo ambalo kwa wazalendo walimsifu Mbowe kwa ujasiri wa kusimamia misimamo ya chama chake.

Miongoni mwa matamshi anayotuhumiwa kuyasema Nassari ni kumpiga marufuku Mkuu wa Nchi kukanyaga Arumeru na Kanda ya Ziwa, eti kwa kuwa maeneo hayo ni ya Chadema na wakati wowote watatangaza Rais wao kama ilivyokuwa Sudani Kusini. 
Mengine ni kumhusisha mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani na masuala ya uteuzi wa viongozi wa nchi unaofanywa na baba yake.


Baada ya kutoa matashi hayo jukwaani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisimama na kusema kuwa matamshi hayo si ya Chadema bali ni ya vijana hao wenye damu ya moto wa gesi na ni kauli zao binafsi na yeye haziungi mkono.

Hongera sana Freeman Mbowe kwa msimamo huo kuutangaza hadharani ili jamii iendelee kukiamini chama hicho cha siasa kuwa kinajali pia maslahi ya nchi kwa ujumla na hii kwangu ni mara ya pili kukusikia ukikanusha matamshi ya wabunge wa chama chako ikiwemo kauli ya Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi(Sugu) alipotamka kuwa viongozi wote wa Serikali wanatakiwa kupopolewa mawe.

Natoa hongera kwa Freeman Mbowe kwasababu ya uwezo wako wa kujenga hoja za kitaifa kwa mustakabali wa Tanzania yetu na wala si chama chako au familia yako au kutafuta sifa ya kushangiliwa kwa kunyooshewa vidole juu ya anga kama ilivyo alama ya chama hicho na vingine duniani.

Lakini mbali na kukupongeza Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuna jambo linanitatiza kidogo labda kupitia makala haya nikitoa hoja naweza kupata ufafanuzi kuhusu kauli za wabunge wa chama chako, je kweli hakuna vikao rasmi ama visivyo rasmi ambavyo chama chako kinapanga mambo haya?

Hainiingii akilini kuwa chama chako na wabunge wa chama hicho huwa hamyazungumzi haya wanayoyaropoka majukwaani mengine katika majukwaa ambayo mnakuwa wote baada ya kutoka katika vikao vya ndani, je kweli vijana wako hao wanajianzia tu?

Mbowe hivi kweli unataka kuwaaminisha watanzania kuwa chama hiki cha siasa kikipata ridhaa kutoka kwa wananchi kuongoza dora katika chaguzi zijazo hawa ndiyo watakuwa Mawaziri au wakuu wa mikoa Tanzania?

Nina mengi ya kukuuliza lakini naona una majukumu mengi ya chama na kitaifa sijui kama waweza kujibu maswali haya ambayo wengine watayatafsiri kuwa ni maswali magumu kiuhalisia lakini ni maswali mepesi kisiasa.

Ninachoweza kukiamini ni kwamba kwa sababu mikutano ya hadhara hasa mnapokuwepo ninyi viongozi wa kitaifa kwa kila chama cha siasa hapa nchini Tanzania ni kwamba kwa sababu kunakuwa na vikao vya ndani na mmnajipanga kuwa nani akaseme nini na nani anaweza katika masuala yepi basi nalazimika kuamini kuwa yawezekana uliamua kumgeuka kijana wako baada ya kuona ametoboa alidari ya siri za vikao vyenu.

Naamini hivyo kwasababu Mbunge huyu kijana sidhani kuwa alikuwa amelewa alipokuwa amepanda jukwaani siku chache baada ya umma wa watanzania kupitia wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki kumpa ridhaa ya kuwa mtumwa wao katika jimbo hilo.

Mbunge huyu namfananisha na mtoto mdogo ambaye huwa anafundishwa uchawi bila kupewa miiko ya wapi anaweza kuyasema masuala hayo ya kishirikina.

Ndiyo, Nassari ni sawa na mtoto ambaye anafundishwa ushirikina kwa sababu mifano hiyo ipo katika jamii zetu ambapo tumeshuhudia mahala pengi watoto wakitamka kuwa wanaruka na Bibi zao au wazazi wao huku wakifanya masuala ya kishirikina na wanapobainika kuwa wameanza kutoa siri hiyo wale wanaowafundisha huwa wanaiaminisha jamii kuwa watoto wao wanaropoka.

Nalazimika kueleza mfano huu ambao wengi wetu ni mashuhuda na ninaamini mfano huu inashabiiana sana na mfano wa matamshi ya Mbunge Nassari na Mbowe ambapo Nassari alisema kuwa chama chao kinataka kufanya hivyo, lakini Mbowe anasema kuwa huo si msimamo wa chama bali na wa vijana kana akina Nassari na chama chake hakihusiki..’’kufundishwa ushirikina na kuropoka’’ kisha mfundishaji anasema mtoto anaropoka.

Nieleweke wazi kuwa katika makala haya sielekezi moja kwa moja kidole kwa Mbowe na viongozi wenzake kuwa huo ni moja ya mipango ya chama chake. La hasha! Bali ni mtazamo mpana ambao kwa pamoja yatupasa tujiulize kuwa Je ni kweli Nassari aliropoka kuhusu kujitenga na kutamka Rais wa kanda ya Kaskazini?

Kama ni kweli kutoka katika sakafu ya moyo wa Mbowe na viongozi wakubwa wa Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kuwa huo si msimamo wao na wala ule uhamasishaji wa Mbunge wa Mbeya mjini kuwa viongozi wa Serikali na familia zao wapigwe mawe, basi nakushauri Mbowe usiwashirikishe katika mambo makubwa vijana wako.

Kati ya vijana ambao nawashauri Chadema wasiwashirikishe katika vikao vikubwa ni pamoja na Mbunge Nassari Joshua, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), John Heche, Diwani wa zamani wa CCM Sombetini ambaye hivi karibuni alihamia Chadema, Alphonce Mawazo na Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Ally Bananga ambaye pia amejiunga Chadema.

Nashauri hivyo kwasababu yawezekana watu hawa bado vifua vyao havijakomaa kutunza mambo makubwa mnayoyapanga sawa na mtoto anayefundishwa uchawi na wazazi au walezi wake kisha dakika kadhaa anamwaga hadharani kwasababu hawawezi kuhimili na kudhani kuwa wakitamka hivyo hadharani basi wataonekana kuwa wamekomaa kisiasa huku wao mategemeo makubwa ni kupigiwa makofi.

Freeman Mbowe hivi kweli hakuna kikao chochote cha siri au cha dhahili ambacho chama chako kilikaa na kupanga mipango hiyo ya kihaini? Au ukweli wako unabaki pale pale kuwa Nassari aliropoka!!

Na kama Nassari aliropoka je unalijua kundi lake ndani ya chama chako kuwa yupo na nani nyuma yake ambao wana mipango ya namna hiyo? Na je unatambua kuwa tetesi nyingi za Tanzania mwisho wake unakuwa kweli? Basi Mwenyekiti kama haya ni magumu kiuhalisia hebu toa ufafanuzi vema kwa umma wa Watanzania hata kisiasa kuwa Nassari ameropoka na wala hakufundishwa ‘’uchawi’’ kama wanavyofanya watoto wengine.

Natoa hoja.!
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754-440749
source;http://www.kalulunga.blogspot.com/

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni