Alhamisi, 3 Mei 2012

HAKIMU AMTAKA WAKILI WA CHADEMA ALIPE GHARAMA ZA MASHAHIDI.

HAKIMU wa Makahama ya Hakimu Mkazi Arusha, Charles Magesa amemwamuru wakili wa utetezi katika kesi inayowakabili viongozi wa Chadema na wafuasi wao 19, kulipa gharama za usumbufu wa mashahidi wawili na mawakili wa serikali watatu ambao walifika kwa ajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Hakimu, Magesa alitoa amri hiyo baada ya Wakili Method Kimomogolo kutofika mahakamani hapo bila kutoa sababu za msingi na badala yake kumtuma Wakili Albart Msando kumwakilisha.

Msando alidai wakili huyo hakuweza kufika mahakamani hapo kwa sababu anakabiliwa na kesi mbili Mahakama ya Rufaa mkoani Arusha ambazo mojawapo ni kesi ya kuvuliwa Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema na ya wanakijiji wa Soitsambu na TBL siku ya Ijumaa.

Amri hiyo ilitolewa na Magesa kutokana na Wakili Msando kusimama na kudai kuwa mshtakiwa Dk. Willibrod Slaa pamoja na mchumba wake, Josephine Mshumbusi wamefiwa na mtu wao wa karibu.

Aliongeza kuwa wakili Kimomogolo hakufika mahakamani hapo kutokana na kuandaa rufaa mbili ambazo anatakiwa kuziwasilisha siku ya Ijumaa ya wiki hii .

Alisema kutokana na wakili kushindwa kufika mahakamani hapo pamoja na Slaa na Josephine aliomba Mahakama hiyo kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo pia kwa sababu washtakiwa wote wana haki ya kuwakilishwa na mawakili wote wawili ambao ni Msando na Kimomogolo.

Alisema mawakili wa Serikali ambao ni Mwahija Ahmed, Awamu Mbwangwa na Edwin Kakolaki pamoja na mashahidi wao kama wanaona kuahirishwa kwa kesi hiyo kunahitaji gharama waseme ili warudishiwe.

Wakili wa Serikali aliiomba Mahakama itoe amri wakili Kimomogolo alipe gharama walizotumia kwa ajili ya kujiandaa na usikilizwaji wa kesi hiyo pamoja na mashahidi wao wawili.

Hakimu Magesa alikubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali ya kuamuru gharama za mawakili wa Serikali pamoja na mashahidi kwa kesi hiyo ambao walikuja jana zilipwe. Kesi iliahirishwa hadi Juni 5 mwaka huu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni