Alhamisi, 31 Mei 2012

HALI YA AMANI HUKO SYRIA NI MBAYA, ANNAN AKARIBIA KUNYOOSHA MIKONO.

Koffi Annan katika Mkutano na waandishi wa Habari mjini Damascus.
Hali yazidi kuwa tete Syria
Kiongozi Mkuu wa waasi nchini Syria amemtaka Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu, Koffi Annan kutangaza kuwa mpango wake umeshindwa.
Kanali Riad al Assad amesema hii itawaweka huru waasi kutokana na mpango wa kusitisha mapigano, ambao Marekani imesema unaweza kuvunjika na kusasbisha mgogoro mpana zaidi katika mashariki ya kati.
Tamko hili la kanali al Assad linakinzana na lile lililotolewa na waasi la kumpa masaa 48 rais Bashar al Assad kutekeleza mpango wa Annan. Assad aliiambia Televisheni ya Al-Jazeera kuwa hakuna muda wa mwisho lakini wanamtaka Annan atangaze kushindwa kwa mpango wake ili wawe huru kuendesha operesheni dhidi ya utawala wa rais Assad.
Majengo mjini Homs yakitoa moshi baada ya kushambuliwa. Majengo mjini Homs yakitoa moshi baada ya kushambuliwa.

Hakuna dalili za mafanikio
Mpango wa Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, haujaweza kusitisha mauaji nchini Syria na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice ameonya kuwa Baraza la Usalama lisipoushinikiza utawala wa Assad kuacha ukandamizaji wa wapinzani, mataifa yatalaazimika kuchukua hatua nje ya Umoja huo.

"Na kwa hakika hiyo ndiyo hali mbaya zaidi ambayo kwa bahati mbaya ndiyo inaelekea kutokea sasa hivi, pale vurugu zitakapongezeka na mgogoro kusambaa na kufikia kiwango cha juu cha utovu wa huruma,na kuhusisha mataifa katika kanda, na kuanza kuchukua sura ya kiitikadi na tutakuwa na mgogoro mkubwa si ndani ya Syria tu bali ndani ya kanda nzima," alisema Balozi Rice
Miili ya watu waliouawa mjini Houla ikizikwa. Miili ya watu waliouawa mjini Houla ikizikwa.

Katika hali kama hiyo, mgogoro wa Syria ambayo ina waumini wengi wa madhehebu ya sunni lakini mtawala wake wa Kabila la Alawite ana uhusiano wa karibu na dola la Kishi'a la Iran unaweza kugeuka wa uwakala ambapo silaha zitakuwa zinatoka kila kona, alisema Rice.
Mgawanyiko miongoni mwa wapinzani
Matamshi kutoka kwa waasi, yanaonyesha namna wapinzani wa rais Assad wamegawanyika, zaidi ya miezi 14 tangu kuanza kwa harakati za ukombozi wa Syria. Waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliripoti siku ya Jumatano kuwa waligundua miili ya watu 13 waliouawa na kuzikwa pamoja Mashariki mwa Syria, siku chache baada ya mauaji ya watu 108 katika mji wa Magharibi wa Haula ambapo jeshi na wanamgambo watiifu kwa utawala walishtumiwa kwa mauaji hayo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameonya kuwa janga kubwa linaelekea kuitumbukiza Syria katika vita vya maafa makubwa ambapo kamwe madhara yake hayatakuja kuisha. Akizungumza mjini Istanbul, Ban alisema mauaji ya raia wasio na hatia, kama yaliyoshuhudiwa wiki iliyopita yanaweza hayapaswi kuendelea na kwamba jumuiya ya kimataifa inaitaka Syria kutekeleza wajibu wake kwa raia.
Wakati huo huo, Urusi na China zinaendelea kushikilia msimamo wao wa kupinga hatua zozote za kuingilia kijeshi nchini Syria na Urusi imesisitiza kuwa msimamo wake huo bado uko pale pale.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni