Jumanne, 8 Mei 2012

WATUHUMIWA SABA WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KESI YA RUSHWA HUKO SAME.

Bw. Edward Hosseah, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Omary Magongo, Same
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha watu saba katika mahakama ya Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za udanganyifu,  ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.


Washtakiwa waliofikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Gabriel Kurwijira,  ni Diwani wa Kata ya Vumari, Joseph Kateri na aliyekuwa Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Dawson Daniel.

Wengine ni aliyekuwa Mkuu wa Sekondari ya Vumari, Johnson Misheto, Mwenyekiti wa bodi ya sekondari hiyo, Mchungaji mstaafu, Moses Tezura, Mwalimu Agnes Makundi, Mjumbe wa bodi, Ernest Mbike na mfanyabiashara Upendo Abraham, anayemiliki duka la vifaa vya ujenzi la Nashy Hardware wilayani hapa.

 Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Susan Baltazar, alisema washtakiwa kwa pamoja kati ya Januari na Juni 2008 wilayani hapa, walikula njama na kutenda kosa kwa kutumia nyaraka zenye maelezo ya uongo kumdanganya mwajiri wao kuwa Nashy Hardware alikuwa ameuzia vifaa vya ujenzi sekondari, jambo ambalo halikuwa kweli.

Baltazar alidai kuwa katika kipindi hichohicho, Misheto, Tezura, Daniel, Kateri na Mbike katika Sekondari ya Vumari, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kuruhusu mfanyabiashara Nashy Hardware kulipwa kwa madai kuwa ameuzia shule vifaa vya ujenzi wakati haikuwa kweli, hivyo kusababisha ubadhirifu wa mali ya umma.

Katika kosa la tatu, ambalo linawahusu Misheto, Makundi na Abrahamu, wanatuhumiwa kutumia nyaraka za uongo kuwa wamepokea vifaa zilizothibitisha kuwa Nashy Hardware alikuwa amevifikisha shuleni hapo.
Washtakiwa hao ambao walikwamisha mradi wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu, wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na vifungu namba 22,31 na 32 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Washtakiwa wote wanadaiwa kuingizia Serikali hasara ya zaidi ya Sh13.4 milioni, walikana mashtaka na wako nje baada ya kutimiza masharti  kwa kuwa na mtu mmoja wa kuaminika na kusaini hati ya thamani ya Sh5 milioni.

Hata hivyo, Mshtakiwa Mbike alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kupelekwa rumande. Kesi iliahirishwa hadi Mei 16, mwaka huu itakapotajwa tena

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni