Jumatatu, 16 Mei 2011

WIZARA YA UJENZI MAMBO SI SHWARI.

HALI bado si shwari ndani ya Wizara ya Ujenzi licha ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi wa juu wa wizara hiyo mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Wizara ya hiyo imekuwa katika mvutano na malumbano ya muda mrefu kiutendaji huku baadhi ya wafanyakazi wakilalamikia ukiukwaji taratibu unaofanywa na baadhi ya vigogo wa wizarani hapo.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni mwendelezo wa mivutano hiyo, wafanyakazi wa wizara hiyo, wamemwomba Rais Jakaya Kikwete kutumia vyombo vyake kuzuia kile walichodai ubabe unaoendelezwa na waziri wa wizara hiyo, Dkt. John Magufuli anayedaiwa kuendelea kuipotosha serikali na umma kuhusu masuala mbalimbali ndani ya wizara hiyo.

Vyanzo vyetu kutoka ndani ya wizara hiyo vimeeleza kuwa kutokana na mwendelezo wa kile kinachoelezwa jeuri ya Dkt. Magufuli, baadhi ya wafanyakazi hao wamepoteza imani na serikali jambo linalochangia kushusha ufanisi wa wizara hiyo.

“Tunashangaa kuona rais wetu mpendwa anafanyiwa usanii hapa wizarani kwetu. Morali ya kazi imeshuka sana kutokana na migongano ya mambo mengi yanayoendelea. Inasikitisha wakuu wa wizara kuweka watu dhaifu kwenye nafasi nyeti za utendaji kwa maslahi binafsi, kwa mfano Mkurugenzi wa Wakala wa Umeme (TAMESA) ameteuliwa bila kushirikisha ngazi nyingine za wizara.

“Kikubwa na kushangaza zaidi, hadi leo wakurugenzi wa wizara wanakaimu nafasi zao huku wakifanya kazi kubwa za wizara, wengine wanashindwa kujibu hoja nzito wakihofia kuharibu nafasi wanazokaimu, sasa hapa tunawasaidia wananchi au tunacheza ?” Kilieleza na kuhoji chanzo chetu ndani ya wizara hiyo.

Ofisa mwingine wa ngazi ya juu wizarani hapo ameliambia Majira kwamba Rais Kikwete anapaswa kutupia macho Wizara ya Ujenzi kwa kutumia vyombo vyake kwani kinachoendelea ni kulindana bila kujali maslahi ya nchi.

“Mheshimiwa Rais kama anataka ahadi zake zitekelezeke zoezi la uteuzi wa wakurugenzi wa wizara na taasisi zake upitie kwake na si vinginevyo kwa maslahi ya nchi na umma,”alisema ofisa huyo na kueleza kuwa anaielewa vyema wizara hiyo kwani amefanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi

Ofisa huyo ambaye kitaaluma ni mhandisi, alitoa mfano wa kusuasua kwa uteuzi wa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS jambo alilosema linaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa wizara hiyo.

“Kutokana na unyeti wa TANROADS, tunamuomba Rais kuingilia kati mchakato wa kumpata mtendaji mpya mwenye uwezo na sifa za kupambana na ufisadi badala ya kumuingiza mtu ambaye ataonekana kuja kulinda maslahi ya waliomtangulia na watuhumiwa wengine wa ufisadi,” alidai.

Ofisa huyo anasema kwa sasa kutokana na nguvu kubwa ya mafisadi ndani ya wizara, tayari watu wenye uwezo mkubwa wameenguliwa kupisha mtu atakayelinda maslahi ya Mtendaji aliyepita Bw. Mrema na wafanyabiashara watuhumiwa wa ufisadi.

“Patrick Mfugale ambaye Rais alitengua uteuzi wake kwenye nafasi ya ukurugenzi wa barabara sasa ndiye amepewa nafasi ya kukaimu taasisi nyeti kama TANROADS ambayo inahusika na barabara. Hii haiingii akilini, ndio maana sasa Waziri amekuwa akimdhalilisha Rais hadharani kupinga maamuzi yake. Tunamwomba Rais asafishe wizara yetu maana sasa wakubwa wanaangalia maslahi yao tu.”

Vyanzo hivyo vilidokeza kuwa Bw. Mfugale alishiriki katika mchakato uliomuingiza Bw. Mrema TANROADS mwaka 2007 akiwa miongoni mwa wajumbe watano wa Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo ikiitwa Wizara ya Miundombinu, Bw. Andrew Chenge.

Vyanzo hivyo vilieleza kuwa kabla ya Bw. Mrema kuondoka, alifanikiwa kumpa nafasi mjumbe mwingine wa kamati iliyomteua kwa kumteua kuwa Meneja wa Barabara zinazojengwa kwa fedha za serikali.

Wajumbe wengine walikuwa ni pamoja na Mwenyekiti Profesa Burton Mwamila, Bw. Steven Mlote na Bw. Joseph Haule.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni