Jumapili, 29 Mei 2011

MMAREKANI AFUKUZWA NCHINI.

Mmarekani amriwa kuondoka

Anthony Mayunga, Tarime
MWANDISHI wa Habari wa Marekani, Joycelin T. Edward (27) amehukumiwa ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh50,000 baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini na kufanyakazi kinyume cha sheria.

Hukumu dhidi ya mwandishi huyo aliyekamatwa juzi, ilitolewa jana na Mahakama ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Hata hivyo, Joycelin alimudu kulipa faini na kuachiwa huru na muda mfupi baadaye alitakiwa kuondoka nchini mara moja.Hatua hiyo ilikuja baada ya vyombo vya dola, kumkabidhi rasmi vifaa vyake vya kazi.

Mapema, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Kasmir Kiria, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Yusto Ruboroga, kuwa Mei 22 mwaka huu, mwandishi huyo aliingia nchini na kufanya kazi katika eneo la Nyamongo, bila kibali cha Idara ya Habari (Maelezo).

Alidai kuwa Mei 26 mwaka huu mshtakiwa alikamatwa na polisi na kuachiwa lakini aliakamatwa tena na maofusa wa Idara ya Uhamiaji katika Wilaya ya Tarime.Ruboroga alidai kuwa katika uchunguzi wao, maofisa wa idara hiyo, walibaini kuwa mshtakiwa hakuwa na vibali vinavyomruhusu kufanya kazi nchini na kwamba wakati huo Joycelin alikuwa tayari ameishafanya kazi na kutuma taarifa nchini Canada.

Hata hivyo akiongea na gazeti hili baada ya kuachiwa huru Joycelin, alisema yeye ni mwandishi wa kimataifa na amekuwa akifuatilia migogoro kama ule wa Nyamongo.

Alisema kabla ya kuingia Tanzania, alikuwa nchini Uganda.Katika hatua nyingine, wenyeviti wa vijiji vya Kewanja, Matongo na Nyangoto, wilayani Tarime wamelalamikia uamuzi wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Constantine Massawe wa kuwanyang'anya bastola walizokuwa wakizimiliki kihalali.

Viongozi hao ambao vijiji vyao vinazunguka mgodi wa African Barrick wa North Mara, walisema uamuzi huo ulifanywa Mei 5 maka huu kufuatia kile kilichodaiwa na polisi kuwa zingetumika katika vurugu za koo.

Wenyeviti waliolalamikia hatua hiyo ni Elisha Nyamhanga wa Kijiji cha Nyangoto, Daud Itembe wa Matongo na O'Mtima Tanzania wa Kewanja.Walidai kuwa maelezo na hatua hizo hazikuwatendea haki hasa ikizingatiwa kuwa watu wanaomiliki silaha kihalali ni wengi.

"Massawe alitutaka twende ofisini kwake na silaha zetu na vibali, tulipofika silaha hizo zilichukuliwa kwa madai kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha hali ya amani si nzuri na kuwa vurugu za koo zingeibuka na huenda silaha zao zingetumika," alisema mmoja wa viongozi hao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni