Ijumaa, 6 Mei 2011

ALASSANE QUATTARA AAPISHWA RASMI KUWA RAIS WA IVORY COAST.

Alassane Ouattara anatarajiwa kuapishwa kuwa Rais wa Ivory Coast na mtu ambaye mwanzo alimkatalia ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Novemba.

Mwezi Desemba, kiongozi wa baraza la katiba alimwidhinisha Laurent Gbagbo kuwa mshindi, iliyosababisha nafasi hiyo kushikiliwa naye kwa muda wa miezi minne.

Bw Gbagbo pia anatarajiwa kuhojiwa juu ya madai ya kukiuka haki za binadamu wakati akiwa madarakani.

Hata hivyo, imeripotiwa kuwa mawakili wake kutoka Ufaransa wamenyimwa ruhusa ya kuingia Ivory Coast.

Shirika la habari la AFP limesema walizuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Abidjan na kutiwa kwenye ndege iliyofuata na kurejeshwa Paris.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuipa nchi hiyo msaada wa zaidi ya dola za kimarekani milioni 60.

Kamishna wa maendeleo wa Ulaya, Andris Piebalgs, ambaye yupo Ivory Coast, amesema inabidi waende kwa kasi.

Aliiambia BBC kuwa hali ilivyo nchini humo bado ina utata na kama maisha ya watu hayakuimarishwa haraka, ghasia zinaweza kuanza upya.

Alisema raia wa nchi hiyo wanahisi wamepoteza miaka 25 ya maendeleo kutokana na mapigano ya kisiasa na kikabila ya hivi karibuni.

Takriban watu 3,000 wanaaminiwa kuuawa wakati wa ghasia zilizotokea kwenye nchi inayozalisha kakao zaidi duniani, ambapo awali ilikuwa nchi yenye utajiri mkubwa Afrika magharibi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni