Alhamisi, 26 Mei 2011

ADAI KUPONA UKIMWI KWA BABU SAMUNGE LOLIONDO.


TIBA YA BABU SAMUNGE:

Abdallah Ally (38) anayedai alikuwa akiugua ugonjwa wa Ukimwi lakini sasa amepona baada ya kupata dawa kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila, akisaidia kugawa vikombe dawa hiyo kwa wagonjwa wengine katika kijiji cha Samunge
MKAZI wa Kijiji cha Galapo, Babati, mkoani Manyara, Abdalah Ally (38), aliyekuwa mgonjwa wa Ukimwi, amedai kupona ugonjwa huo na kinga zake za mwili (CD4) kuongezeka baada ya kunywa dawa ya Mchungaji, Ambilikile Mwasapila.Ally anakuwa mtu wa pili kujitangaza kupona Ukimwi baada ya kunywa kikombe cha dawa hiyo, baada ya Wilia John Lengume wa Samunge aliyekuwa wa kwanza kutangaza kupona ugonjwa huo baada ya kupata dawa hiyo. Akizungumza jana kijijini hapa, Ally alisema kwamba amekuwa akitumia Dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV), tangu mwaka 2009 kabla ya kupata kikombe cha Babu, Januari 5, mwaka huu. Akiwa na vyeti vya vilivyoonyesha kwamba alikuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Ally alisema kuwa Aprili 22, 2009 alipimwa na kukutwa na maambukizi hayo wakati huo akiwa mfungwa katika Gereza la Babati. Alisema alipima afya yake Februari 25, mwaka huu wilayani Babati na katikia Kituo cha Msalaba Mwekundu na kukutwa hana tena VVU. Alipima tena katika Hospitali ya Wilaya ya Babati ambako pia alikutwa kinga yake ya mwili ni ya kutosha na hana tena VVU ndipo alipoamua kuacha kutumia ARV. Alidai kwamba hata baadhi ya maofisa wa afya waliokuwa wakisimamia matibabu yake wilayani Babati walishangazwa na kupona kwake kwa tiba ya Mchungaji Mwasapila na hilo liliwafanya nao kufunga safari kuja Samunge Aprili 28, mwaka huu kupata kikombe. "Ninavyo vyeti vinavyothibitisha kuwa sina tena Ukimwi na mwezi huu pia natarajia kupima kuona afya yangu ipo vipi," alisema Ally. Alisema kuwa kabla ya kufungwa, alikuwa dereva wa magari makubwa huku akidokeza kwamba kilichosababisha kifungo chake kilichoanza Machi 9, 2009, ni kesi ya kukutwa na pombe haramu ya gongo nyumbani kwake ambayo ilikutwa na polisi Machi 15, 2003 ambayo alidai kuwa iliwekwa nyumbani kwake na mkewe. "Baada ya kukamatwa, kesi ilifikishwa mahakamani na baadaye faili lilipotea hivyo nikaacha kuhudhuria kesi. Lakini baadaye hukumu ilikuja kutolewa nikiwa sipo mahakamani, ndipo nikaja kukamatwa na kufungwa miezi tisa," alisema Ally. Alisema akiwa gerezani ndipo alipopimwa na kukutwa na VVU na Julai 7, 2009, alianza kutumia dawa huku vyeti vyake vikionyesha majina ya dawa alizokuwa akitumia na tarehe alizohudhuria kliniki ya watu walio na VVU, Babati. "Nikiwa uraiani nilianza kupata taarifa za kuwepo kwa tiba hapa Samunge, ndipo nilipojikusanya na kuamua kuja. Baada ya kupata kikombe nilirejea Babati," alisema Ally na kuongeza kuwa ameamua kurejea tena Samunge ili kumsaidia Mchungaji Mwasapila kazi ya kugawa vikombe ikiwa ni ishara ya shukrani kwake.
Chanzo:Mwananchi

Maoni 1 :