Picha jeneza barabarani huko Tarime.

Habari zaidi zinaeleza kuwa vurugu hizo mpaka kukamatwa wa wabunge hao zilianza jana usiku majira ya saa 1: 30 usiku baada ya ndugu na jamaa za wafiwa kueleza kuwa wameona askari Polisi wakinunua majeneza manne na kupakia katika gari hali ambayo iliashiria kuwa kulikuwa na mpango wa polisi kuchukua maiti waliouawa kwa risasi mgodini kwa lengo la kuvuruga mpango wa kuendesha maziko ya pamoja ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika katika uwanja wa sabasaba chini ya uratibu wa Chadema.

Kufuatia taarifa hiyo Tundu Lissu, Waitara na makada wengine wa Chadema pamoja na wananchi walifika katika eneo la Mochwari ambako muda mfupi wananchi wengi walikuwa wamefika pia kuzuia Polisi kubeba miili hiyo usiku.

Lakini polisi walipofika majira ya saa 2:00 usiku na kukuta timu kubwa ya watu ambao wallikuwa wamejitolea kulinda maiti hao wasichukuliwe, walianza kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya watu na ndipo walipowakamata wakina Tundu na wengine.

Baada ya kuwasambaratisha watu hao na akina Lissu kukamatwa, Polisi waliingia na majeneza yao usiku huo na kuanza kuchukua miili hiyo ambayo waliiondoa Mochwari na kuanza kuisambaza asubuhi katika nyumba za wafiwa nako wakizitelekeza barabarani jana asubuhi.

Familia waliyagomea masanduku hayo, kwa vile hawakujua kama ilikuwa na ndugu zao ama maiti wengine na  kwamba hawakushiriki kuitayarisha toka Mochwari hatua ambayo iliifanya miili hiyo kukaa barabarani hadi majira ya saa 4 ambapo katika kijiji cha Nyakunguru waandishi walipokuwa wakipiga picha walikamatwa wakisingiziwa kuchochea ndugu kukataa kuzika.

Utetezi wa Polisi juu ya kitendo hicho:
Akizungumza kwa njia ya simu  Kamanda wa polisi Kanda maalum ya Tarime Constantine Masawe, alikiri kukamatwa kwa watu hao na kueleza kuwa walikamatwa kutokana na jeshi lake kupata taarifa za baadhi ya ngudu wa marehemu kushindwa kuchukua miili ya ndugu zao jana usiku kwa ajili ya maziko.

“Unajua jana baada ya kufanyika Postmortem kama walivyotaka miili yote ilikuwa chini ya familia, sasa uamuzi wa kuzika ulikuwa juu yao, lakini majira ya saa 2 usiku tulipata taarifa kuwa kuna watu wako Mochwari wamewazuia ndugu wanaotaka kuzika wasichukue miili ya jamaa zao, tulipofika tulikuta wapo watu na tulifanikiwa kuwakamata wanane ambao wanne walikuwa ni wakazi wa Singida na wengine wanne wakiwa ni wakazi wa Tarime,” alieleza Kamanda Masawe.

Alisema kuwa baada ya kuwakamata watu hao na kuwatimua wengine waliokuwa wakilinda Mochwari, polisi walisimamia ndugu na jamaa ambao walitaka kuchukua miili hiyo kwa maziko (Usiku) na kuwapa ulinzi.

“Tuliwasaidia kuchukua miili hiyo Mochwari hapo na kuwapelekea nyumbani kwao, hapo unaposema barabarani ni kwamba ndugu walikuwa wakifika na kusema amefika tuliwashusha na jeneza lao, sasa hii habari ya majeneza kuwa barabarani tumegundua kuwa inachochewa na kundi la watu ambao wamekuwa wakiwatisha wasizike,” alieleza Kamanda Masawe.

Sababu za kuzuiwa Ibada ya Maziko:
Aidha mpango wa awali ambao ulikuwa umeandaliwa na Chadema ulikuwa ni kuendesha ibada ya maziko katika uwanja wa Saba Saba leo kuanzia saa 2 asubuhi kabla ya kupelekwa katika vijiji vyao kwa ajili ya mazishi ya kifamilia.

Kwa mujibu wa Tundu Lissu (akizungumza juzi kabla ya kukamatwa) alisema licha ya kuwa kulikuwa na makubaliano baina ya familia, Chadema na jeshi la polisi lilowakilishwa na Kamishina wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja, jeshi la polisi lilibatilisha kibali hicho baadaye kwa madai kuwa walikuwa wamepewa maelekezo toka juu.

“Tumekuwa katika maandalizi ya mazishi hayo tangu jana jioni(juzi). Hata hivyo, jioni hii tumeletewa barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Tarime kututaarifu kwamba haturuhusiwi tena kuwaaga marehemu wetu kama ilivyokubaliwa jana,’ alieleza Lissu huku akibainisha kuwa mpango huu uliratibiwa mahususi kwa lengo la kukwamisha jitihada za Ibada hiyo ya maziko ya pamoja kufanyika.

Polisi walivamia Mochwari kuchukua miili hiyo ili kuharibu mpango wa Chadema wa kuendesha Ibada ya maziko ya pamoja, walitambua kuwa iwapo wangetoa nafasi ya kukucha asubuhi hali ingekuwa kama Arusha kwa vile wananchi walikuwa wakiwaunga mkono Chadema kuaga miili hiyo uwanjwa wa Sabasaba leo saa 2 asubuhi.

Hivyo sambamba na mkakati huo polisi walichoamua ni kuhakikisha Tundu Lissu na wenzake hawapati dhamana ili usiku wa jana waratibu wao kuzika kwa nguvu na kukamatwa kwa waandishi kuna nia ya kuwatisha, kuwazuia pia kutoa taarifa zao za kuiba maiti ikiwa ni pamoja na picha walizopiga jeneza ambalo limetelekezwa barabarani na polisi zisitoke katika vyombo vya habari jana.