Jumatatu, 15 Agosti 2011

GERVINHO AZUA BALAA LIGI UINGEREZA.

Joey Barton kiungo wa Newcastle amekiri "alianguka kirahisi" wakati wa purukushani na Gervinho lakini akasisitiza mshambuliaji huyo wa Arsenal alistahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Joey Barton

Joey Barton

Gervinho alitolewa katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England akiichezea Arsenal kwa kumchapa kibao Barton, ambaye naye alioneshwa kadi ya njano kwa kumsukasuka Gervinho.
Baada ya kwenda sare ya 0-0, Barton aliandika katika mtandao wa tweeter: "Nilijiangusha kirahisi sana, hakuna ubishi kwa hilo. Lakini bado huwezi kuinua mikono yako. Mwamuzi alitenda haki, hakukosea."
"Iwapo unainua mikono yako na kumpiga mwenzio usoni, huna budi kutolewa nje. Watu walitaka nifanyeje, nisimame na kuanza kurusha ngumi?"
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alisema wachezaji wote wawili walipaswa kupewa adhabu inayofanana.
Siielewi ile kadi nyekundu," alisema Wenger. "Nina hakika asilimia 100 mwamuzi hakuona kilichotokea.
"Nadhani alikuwa amegeuka upande mwengine wakati purukushani zikitokea. Iwapo aneona tukio lenyewe, angewatoa nje wachezaji wote wawili au asingemtoa yeyote."
Wachezaji hao walishikana baada ya Gervinho kuanguka chini eneo la sanduku la timu ya Newcastle na Barton akamfuata kwa hasira na kuanza kumkunja fulana ya Gervinho."Kwa nini Joey Barton alikwenda pale na kuanza kumkunja fulana yake na kumuinua?" aliongeza Wenger. "Ni kadi ya manjano kwa wote au kadi nyekundu kwa wote na kilichotokea hakikuwa kikubwa sana.
Kuhusu kukata rufaa? Nitaangalia tukio lile kwa makini kwanza, lakini nadhani ninashawishika kusema nitakata rufaa."
Meneja wa Newcastle Alan Pardew alimtetea Barton, ambaye yupo katika orodha ya wachezaji wanaohama katika klabu hiyo baada ya kuishutumu klabu na alipangwa mechi ya Jumamosi baada ya kumshawishi meneja wake kwamba hana nia ya kuhama tena.
"Gervinho alijiangusha, hakuna tatizo na hilo," alisema Pardew. "Jinsi alivyofanya Joey kumfuata ilikuwa ni kumtia adabu na kukatokea kutoelewana. Lakini baadae akamchapa kibao na huwezi kufanya hivyo."

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni