Jumapili, 28 Agosti 2011

SERIKALI BADO YAWATAMBUA MADIWANI WA CHADEMA WALIOFUKUZWA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, ameamuru madiwani waliofukuzwa wa Chadema, kuendelea na vikao na kulipwa posho zao hadi Mahakama itakapotoa uamuzi juu ya kufukuzwa kwao.

Aidha barua ya Mkuchika yenye Kumbukumbu namba HA.23/235/01/06 iliyotolewa Agosti 23, na kumfikia Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomih Chang'ah, ilieleza kuwa Tamisemi bado inawatambua madiwani hao na wataendelea kulipwa posho zao hadi Mahakama itakapotoa uamuzi kama madiwani hao watano ni wanachama halali wa Chadema au la.

Barua hiyo pia ilieleza kuwa Mahakama ndiye mwamuzi wa mwisho, hivyo ni vyema suala hilo likasubiriwa kutolewa uamuzi, lakini madiwani hao ambao ni Estomii Mallah (Kimandolu), Ruben Ngowi (Themi), John Bayo (Elerai), Charles Mpanda (Kaloleni) na Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed, kisheria wataendelea kuhudhuria vikao na kulipwa posho.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Chang'a alisema amepokea barua hiyo kutoka kwa Waziri Mkuchika yenye maelezo hayo kutokana na barua ya awali aliyoiandika MD/ US/101/ 1/107 Agosti 12.

Alisema suala la madiwani hao kuendelea na wadhifa, ni uamuzi utakaotolewa na Mahakama, kwani walishafungua kesi ya madai, hivyo Mahakama ndiyo itatoa uamuzi kisheria na nakala za barua hiyo wamepewa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima, Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Alisema Sheria ya Serikali za Mitaa namba 8 ya mwaka 1982, kifungu cha 26 (1) (e), inafafanua kuwa Waziri mwenye dhamana na serikali za mitaa, atatamka kuwa nafasi ya Diwani iko wazi, baada ya kupokea taarifa rasmi ya maandishi kutoka kwa Mwenyekiti au
Meya wa Jiji la Arusha.

Alisema suala la kuambiwa kuwa anakumbatia madiwani hao kama Mkurugenzi linamwumiza kichwa na anapokea tuhuma nyingi juu ya madiwani hao pia maendeleo ya Jiji la Arusha hafanyiki, kutokana na mgogoro huo, na Waziri ameshatoa ufafanuzi, hivyo
kutokana na uamuzi wa Waziri busara zinahitajika zaidi.

"Wengi wanadhani nawabeba madiwani hao waliovuliwa uanachama, lakini ukweli siwakumbatii, napokea malalamiko mengi lakini namwachia Mungu, ila naomba busara zaidi itumike kwa suala hili, hususan kwa viongozi wa siasa, maana Waziri ametoa majibu kwenye barua, lakini sijui itakuwaje.

“Nawaomba viongozi wa siasa kutumia busara zaidi, kwani maendeleo ya Arusha yanalala … inaumiza unapotuhumiwa kwa kitu ambacho hujakifanya, inaumiza kichwa changu sana."

Dk Slaa alisema aliwasilisha barua ya kuwavua uanachama madiwani hao kwa Mkurugenzi Agosti 8 lakini anashangaa kuwa barua ya Waziri ilimfikia Agosti 12, na si Agosti 10 kama nukushi inavyoeleza.

“Suala la Arusha inabidi liangaliwe kwa kina, kwani inavyoonekana wanapoteza muda wa maendeleo kwa vitu vya kipuuzi, wasipoangalia kuhusu uamuzi sahihi wa mgogoro wa Arusha, kitakachotokea ni kama suala la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni