Jumatatu, 1 Agosti 2011

POMBE ZA HARUSI ZAMUUA MZAMBIA

Wahudumu wa Afya wakitoa mwili wa marehemu ndani ya hoteli.

RAIA wa Zambia amekutwa amekufa ndani ya Hoteli ya Southern Sun jijini Dar es Salaam, huku watu wengine watatu wakiwa katika hali mbaya kwa kile kinachosemekana kuzidiwa na ulevi.

Wanaume hao wanne walikutwa katika chumba namba 425 ghorofa ya nne ndani ya hoteli hiyo iliyoko katikati ya Jiji, watatu wakiwa hawajitambui.

Aliyefariki ametambuliwa kwa jina moja la Baster. Mwandishi wa gazeti hili alifika hotelini hapo saa saba mchana na kukuta Askari wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, wakiendelea na kazi yao huku wafanyakazi wa hoteli hiyo wakionesha wasiwasi kutokana na tukio hilo.

Katika mlango wa nyuma wa hoteli hiyo, maiti ya Mzambia huyo ilitolewa na wahudumu wa afya wa kampuni binafsi na kuiingiza katika gari la kampuni hiyo kisha kuondoka nayo chini ya ulinzi wa Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alithibitisha kifo hicho na kusema Polisi wanaendelea na uchunguzi.

Wanaume watatu waliokuwa hai walifikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakiwa mahututi, lakini baada ya kuwekewa maji, mmoja wao, Eliud Sikwabi ambaye ni Muingereza, alizinduka na kuhojiwa na kuwataja wenzake Ikbar Bahabur wa Zambia na Mtanzania aliyetajwa kwa jina moja la Omari, ambaye anayeaminika alishiriki katika harusi iliyofanyika usiku wa kuamkia jana ambako alitumbuiza.

Kamanda Shilogile alisema kinachoonekana kuwa watu hao walikunywa sana pombe kali, ndiyo sababu ya hali hiyo ambazo walianza kunywa pombe hizo katika sherehe ya harusi ya mtoto wa Jaji Mark Bomani.

Aliyekuwa amepanga katika chumba hicho cha Hoteli ya Southern Sun ni Sikwabi.

“Inasemekana watu hawa baada ya kutoka kwenye harusi hiyo, waliendelea kunywa pombe hizo chumbani na hata Polisi wamekuta mabaki ya pombe hizo chumbani na uchunguzi wa pombe hizo unaendelea,” alisema Kamanda Shilogile.

Akizungumza na gazeti hili jana, Jaji Bomani alikiri watu hao kuwepo katika harusi ya mwanawe, Clement Bomani iliyofungwa juzi asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph na baadaye walipata chakula cha mchana katika Ukumbi wa Mlimani City.

Jaji Bomani alikiri kuwa watatu waliolazwa katika Hospitali ya Muhimbili ni marafiki wa mtoto wake huyo, lakini alisema aliyefariki dunia hawamtambui, bali alifika na rafiki zake hao.

Alisema baada ya chakula cha mchana, vijana walikuwa na sherehe yao jioni iliyofanyika nyumbani kwake Mikocheni, ambako walikunywa pombe.

Kamanda Shilogile alisema, wanaendelea na uchunguzi kutokana na kuwa matukio ya vifo vinavyotokana na pombe au sumu uchunguzi wake huchukua muda mrefu. Aliahidi kuzungumzia suala hilo kwa undani leo.

Awali, Meneja wa zamu wa kike (jina lake halikufahamika) ambaye mwandishi alimsubiri kwa karibu saa moja, alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai ya Mkurugenzi Mkuu pekee ndiye anayeweza kuzungumzia.

Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Adam Fuller, alisema kwa kuwa uchunguzi wa Polisi unaendelea, hana cha kueleza.

Chanzo; Gazeti la Habari Leo

Maoni 1 :

  1. Sehemu nzuri na yenye siri kwa adui yako kukupata ni pale kwenye sehemu za pombe (Kwani hawa watu ilikuwa mara yao ya kwanza kuonja pombe ili wazidishe kiasi hicho?)

    JibuFuta