Alhamisi, 4 Agosti 2011

RAIS WA ZAMANI WA MISRI AFIKISHWA KIZIMBANI AKIWA TAABANI KITANDANI.



Aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak
Thursday, August 04, 2011 4:30 AMHata kama utakuwa madarakani na kwa kutumia nguvu zako madarakani kufanya ufisadi kwa kuiba pesa za wananchi na kutumia rushwa kuwanyima wananchi haki zao, ipo siku yote yataisha na utaanguka na kuwa mtu mwenye kudharauliwa na pesa zote ulizo nazo hazitatosha kunusuru maisha yako.
Hapa nazungumzia kesi ya aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak ambaye enzi za utawala wake alikuwa ni mtu mwenye maguvu mwenye kuogopewa na kila mtu nchini Misri kutokana na ubabe wake, lakini jana aliingizwa mahakamani akiwa mdogo kama sisimizi akiwa hoi bin taabani akishindwa hata kusimama na kupelekea asomewe mashtaka akiwa kwenye kitanda cha hospitali.

Katika hali ambayo wananchi wa Misri waliifurahia ni kumuona kiongozi wao huyo wa zamani akiwa amevalishwa sare nyeupe ya magereza akiwa kwenye kizimba kilichozungushiwa machuma pamoja na wanae ambao wote wanatuhumiwa kwa makosa mbali mbali.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi za kiarabu kiongozi wa nchi amepandishwa kizimbani na wananchi wake, tukiacha mfano wa Saddam Hussein wa Irak ambaye alinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya makosa yaliyokuwa yakimkabili.

Mubarak maisha yake yako hatarini kwani anatuhumiwa kwa mauaji ya watu zaidi ya 800 waliouliwa wakati wa maandamano ya kuuong'oa utawala wake. Mubarak anatuhumiwa kuamuru silaha za moto zitumike kukomesha maandamano ya wananchi waliouchoka utawala wake.

Mubarak huenda akahukumiwa kunyongwa iwapo atapatikana na hatia.

Mamilioni ya wananchi wa Misri walishuhudia LIVE kwenye luninga kubwa zilizowekwa mitaani, wakati mbabe huyo wa zamani akiwa mbele ya sheria.

Mubarak mwenye umri wa miaka 83 alikanusha mashtaka yote aliyosomewa mahakamani yakiwemo mashtaka ya mauaji na rushwa.

Kesi hii iliahirishwa hadi tarehe 15 mwezi huu ambapo Mubarak atarudi tena kizimbani.

Kesi hii ni somo zuri kwa wanasiasa mafisadi wa barani Afrika, Mubarak ananyea debe hivi sasa jela sio kwasababu ya shinikizo la mataifa ya nje bali ni nguvu za wananchi wale waliosema "Tumechoka sasa basi".

Mubarak ingawa anadaiwa kuwa na mamilioni ya dola kwenye mabenki ya nje ya nchi yake, hawezi tena kuyafaidi mamilioni hayo aliyodaiwa kuyaiba nchini kwake akiwaacha wananchi wake wa hali za chini wakiteseka.

Utawala wa Mubarak ulikuwa ni miaka 30, hivyo mafisadi jifunzeni kuwa ingawa mtatesa sana madarakani mkiyarudisha nyuma maisha ya wananchi wenu, ipo siku moja sheria itashika mkondo wake na dhamana ambayo mlipewa na wananchi lakini mkaitumia ndiyo itakayowatokea mbele zenu na kuwaangamiza

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni