Ijumaa, 26 Agosti 2011

UMOJA WA NCHI HURU ZA KIAFRIKA WAACHWA NJIA PANDA BAADA YA UTAWALA WA TRIPOLI KUANGUSHWA

Wakati Walibya wanafurahia kuanguka kwa mji wa Tripoli katika mikono ya waasi, Waafrika katika mataifa mengi walijizuwia na furaha hiyo.Umoja wa Afrika hata hivyo haujaweka wazi iwapo utatambua baraza la mpito.


Wakati  Walibya  wengi  wakifurahia  kukamatwa  kwa  mji  mkuu  wa Libya  Tripoli  na  waasi , Waafrika   katika  mataifa  mengi walijizuwia  na  furaha  hiyo. Walikuwa  na  uhusiano  wenye  hisia tofauti  na  Gaddafi. Kwa  upande  mmoja  Gaddafi  alikuwa  ni mgeni  maarufu  wa  kitaifa  kila  mara  anapotembelea  taifa  fulani, kwa  kuwa  alikuwa  akija  na  mkoba  wa  fedha. Alisaidia  sana mapambano  dhidi  ya  ukoloni,  lakini  pia  aliwasaidia   madikteta kwa  kuwapatia   silaha ,  na  pia  alimsaidia  rais  Zuma  katika harakati  zake  za  kuingia  madarakani, licha  ya  kuwa   hilo linapingwa.  Na  pia  umoja  wa  Afrika  unachukua  hatua  za tahadhari  sana  katika    hatua  zinazotokea  kila  siku  nchini  Libya. Leo  Ijumaa  umoja  wa  Afrika  unafanya  kikao  maalum  kwa  ajili ya  Libya. Lakini  bado  hali  haijafahamika  wazi , iwapo  viongozi wa   serikali  na   mataifa  ya  Afrika    watawatambua  waasi  wa Libya.
Baadhi ya Viongozi wa AU walipomtembelea Gaddaffi mwanzoni mwa mwaka huu.

Matamshi  ya  rais  wa  Ghana  John Atta  Mills  yanaonyesha  wazi mshutuko  mkubwa   kuhusiana  na  hali  ya  Gaddafi  ambayo imeuyumbisha   umoja  wa  Afrika.
"Tunatambua   kuwa  baraza   la  usalama   na  amani  la   umoja  wa afrika  litakutana , lakini  Ghana  inachunguza  hali  ilivyo, na tutachukua  uamuzi  sahihi, ikitiliwa  maanani  kile  ambacho  ni  cha manufaa  kwa  taifa  letu".
Kiongozi  mwenzake  mwenye   nguvu  zaidi  wa  Afrika  kusini  Jacob Zuma  ameonyesha   hadi  sasa  msimamo  wa  wazi  wakati akieleza  shutuma  zake  kwa mashambulizi  ya  NATO.
"Tumejikuta  katika  hali, ambapo  mataifa  yaliyoendelea  yameamua kuingilia  kati  katika  bara  la  Afrika, katika  utaratibu  ambao haujakubalika. Tumeona  kuwa  maazimio  haya  yanaendewa kinyume  katika  hali  ambayo  haikubaliki  kabisa".
Zuma  anaitupia   lawama  jumuiya  ya  NATO, kwa  kuendesha  sera za  mabadiliko  ya  utawala   na  kulikandamiza   jukumu  la  Afrika katika  utatuzi  wa  mzozo  huo. Kuhusu   juhudi  zake  mara  mbili zilizoshindwa    za  upatanishi  mjini  Tripoli  hapendi  sana kuzizungumzia. Gaddafi   alimkaribisha  Zuma  katika  hema alimokuwa  akiishi. Ni  hivi  karibuni  tu  waziri  wa  mambo  ya  kigeni wa  nigeria  Ashiru  alitamka  wazi  kuwa  serikali  nyingi  katika mataifa  ya  Afrika  zilikuwa  zikikubaliana  na  Gaddafi. Miongoni mwa  nchi  hizo  ni  Zimbabwe, kuna  mahoteli  kadha  nchini  Kenya na  Afrika  kusini   na  mara  nyingi  chama  tawala  cha  ANC kilipata   fedha  nyingi  kutoka  kwa  Gaddafi  katika  mapambano dhidi  ya  ubaguzi  wa  rangi. kwa  hiyo  si  jambo  la  kushangaza , kwamba  hadi  sasa  mataifa  hayo  hayakuwaunga  mkono  waasi. Anakiri   hivyo  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Afrika  kusini Nkoana- Mashabane  kuwa  haikuwa  rahisi  kulikubali  baraza  hilo la  mpito. Anatoa  wito  lakini.
"Tungependa  kutoa  wito  kwa  mamlaka  ya  mpito  kuanzisha  haraka mjadala   wa  walibya  wote, wenye  nia  ya  kuunda  uwakilishi  halisi wa  serikali  ulio  katika misingi  wa  watu  wa  Libya".
Afrika  kusini  inasisitiza  kuhusu  kile  kinachojulikana  kama utaratibu  maalum, "Roadmap",  ya  umoja  wa  Afrika, ambayo inazungumzia  kuhusu  mjadala  wa  aina  hiyo, kura  ya  maoni kuhusu  katiba  na  hatimaye  ufanyike  uchaguzi. Inawezekana  kwa vyovyote  vile  kuwa  mtazamo  huu  wa  umoja  wa  Afrika ukatekelezwa. Lakini ni  pale  tu  baraza  la  taifa  la  mpito  la  Libya litakapopendelea  kufuata. Huenda  pia  Libya  isiwe  na  haja  na  umoja wa  Afrika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni