Ijumaa, 12 Agosti 2011

WABUNGE WA DAR ES SALAAM WAMWAGA MBOGA, MEYA WA JIJI AMWAGA UGALI, KAZI KWELI!!!!!!

Raymond Kaminyoge
SAKATA la Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Massaburi na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, jana lilichukua sura mpya baada ya kuivunja bodi ya Shirika la Maendeleo na Uchumi Dar es Salaam (DDC) iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu.
Dr. Didas Masaburi, Meya wa Jiji la Dar es salaam.


Uamuzi huo wa Dk Masaburi ambaye ameingia kwenye mvutano na wabunge wa mkoa wake, ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuvunja bodi hiyo kutokana na kile alichokiita ni kusafisha ufisadi uliotamalaki.

Wakati wabunge hao wa Dares Salaam wakimpa siku  saba meya huyo ili awaombe radhi kutokana na kile walichodai ni kutukanwa na kwamba wanafikiri kwa makalio badala ya ubongo, jana Dk  Masaburi alifanya ziara ya kushtukiza na kuamua kuivunja bodi hiyo.

Dk Masaburi katika ziara hiyo alikuwa akikagua vitega uchumi vya shirika hilo vilivyopo Kariakoo, Magomeni na Mwenge ambako aligundua ufisadi katika ukumbi wa DDC Kariakoo.

Akizungumza, Dk Massaburi alisema katika mkataba wa ujenzi wa vibanda vya maduka 73 vinavyouzunguka Ukumbi wa DDC Kariakoo, unaonyesha  kila kibanda kinapangishwa kwa Sh300,000 kwa mwezi wakati wapangaji wamesema wanalipa hadi kufikia Sh 2.6 milioni kwa mwezi.

Mh.Abbas Mtemvu, Mwenyekiti wa Bodi iliyovunjwa Shirika la Maendeleo la Jiji DDC.


Alifafanua kwamba kati ya Sh 300,000 wanazolipa wapangaji hao,  asilimia 40 zinakwenda DDC  wakati  60 zinachukuliwa na Kampuni ya Nimeta Construction Ltd, waliojenga vibanda hivyo.

“ Inaonyesha vibanda vya maduka haya wamepangisha watu kwa njia za ulanguzi, fedha nyingi zinaingia mifukoni mwa wajanja wachache wakati DDC wanaambulia asilimia 40 ya Sh 300,000 huu ni wizi wa mchana,” alisema Dk Masaburi.

Alisema, “ kutokana na hali iliyopo nimeamua kuivunja bodi ya DDC kuanzia leo (jana) na nitaitangaza bodi mpya hivi karibuni.” Bodi hiyo kwa mujibu wa Meya ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mtemvu, huku wajumbe wakiwa ni Jerome Bwanausi, William Bomani, Rehema Mayunga, Wendo Mwapachu na Issac Tasinga.

Dk Massaburi alimtaka Kaimu Meneja Mkuu wa DDC, Cyprian Mbuya kuripoti kwa Mkurugenzi wa jiji wakati huu inaposubiriwa kutangazwa kwa bodi mpya.

Kwa mujibu wa Dk Masaburi, utaandaliwa utaratibu mpya wa upangishaji wa vibanda hivyo ili fedha zote ziweze kuwa mali ya DDC badala ya kuingia mifukoni mwa wajanja.Katika ziara hiyo, Meya aliongozana na Katibu wa Kata ya Magomeni ambaye pia ni diwani wa Kata ya Magomeni, Julian Bujugo.

Uamuzi huo wa Dk Masaburi ambaye matamshi yake dhidi ya wabunge wa mkoa huo yamekwishafikishwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, itazidi kuongeza mvutano kati yake na wawakilishi hao.

Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni