Jumamosi, 6 Agosti 2011

EWURA KUPIGA FAINI MILIONI 3 KWA WAFANYABIASHARA YA MAFUTA WAKOROFI.

 Mgomo uliofanywa na kampuni za mafuta kupinga kushushwa kwa bei ya bidhaa hiyo, umeibua hasira za serikali, ambapo sasa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kumchunguza Mkurugenzi wa Kampuni ya Engen, Selan Naidoo, ili kumchukulia hatua iwapo atabainika kuendelea kutoa matamshi yanayolenga kuchochea mgomo huo.

EWURA imesema hatua hizo zitachukuliwa dhidi ya Naidoo, ikiwa ni pamoja na kumnyang’anya leseni ya biashara ya mafuta, kwa vile yeyote anayechochea wenzake kugoma anavunja sheria za nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu, alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya Naidoo kuipa serikali saa 24 kuangalia namna ya kufidia hasara watakayopata pindi wanapouza mafuta kwa bei elekezi la sivyo ataachana na biashara hiyo.

Masebu alisema mchakato ulioifikisha serikali kufikia maamuzi ya kushusha bei ya mafuta, ulifanywa kitaalamu na ulikuwa sahihi kwani ulizingatia sheria, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wote wa bidhaa hiyo. Kutokana na hilo, alisema kamwe hawawezi kumvumilia mtu yeyote anayechochea wenzake kuvunja sheria za nchi, “Tutaangalia kwa undani tabia ya kiongozi wa Engen. Akiendelea na matamshi ya kuvunja sheria za nchi, sheria itachukua mkondo wake, ikibidi tutamnyang’anya leseni,” alisema Masebu.

Pia alisema kampuni yoyote itakayobainika kuendelea kuuza mafuta kwa bei ya zamani, kila moja itatozwa faini ya Shilingi milioni 3 kwa kila siku hadi hapo itakaporekebisha bei hiyo.

Alisema pia wanazichunguza kampuni zote zinazoendelea kugoma kuuza mafuta na kwamba, kwa sasa wanajielekeza katika mikoa ya Mwanza na Manyara, ambako kunadaiwa kuwapo na mgomo baridi.

Vilevile, alisema watatembelea vituo vya kuuza mafuta kuhakikisha vinauza nishati hiyo kwa bei elekezi.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani, ni marufuku kwa wafanyabiashara ya mafuta kukaa na kupanga bei, hivyo iwapo itathibitika jana walifanya kitendo hicho, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Masebu alisema katika kujibu malalamiko ya kampuni za mafuta, Bodi ya EWURA imeamua kufanya marekebisho kuhusu gharama anazotozwa mfanyabiashara kwa kuchelewa kupakua mafuta kutoka kwenye meli bandarini. Katika marekebisho hayo, sasa gharama za meli kukaa bandarini kwa ajili ya kupakua mafuta kutoka siku 3-15, hatalipa mfanyabiashara, badala yake, zitalipwa na serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).



source: http://www.wavuti.com/habari.html#ixzz1UH8ZpSBJ

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni