Jumanne, 28 Juni 2011

OCEAN VIEW MAMBO SAFI KAGAME CUP


Timu ya Ocean view ya Zanzibar imejiwekea mazingira mazuri zaidi ya kufuzu robo fainali ya michuano ya Kombe Kagame baada ya kuifunga Red Sea ya Eritrea mabao 2-0.

Kutokana na ushindi wa mchezo huo uliofanyika mchana Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Ocean View imefikisha pointi sita na kuongoza kundi hilo, baada ya mchezo wa kwanza kuifunga Etincelles ya Rwanda mabao 3-2.

Ocean View sasa imebakisha michezo miwili wa kwanza itacheza na Simba kesho na mwingine itaumana na Vital ‘O ya Burundi Jumapili.

Kihesabu inaweza kuonekana kana kwamba tayari Ocean View imefuzu kwa vile timu zinazotakiwa kufuzu robo fainali kwa Kundi A ni tatu, lakini kisoka bado kwa vile inaweza kupoteza michezo yake yote iliyobaki, kisha wapinzani wake wakashinda michezo yao hivyo kupita pointi sita ama kuwa sawa na badala yake idadi ya uwiano wa mabao ukaamua.

Katika mchezo wa jana, Ocean View ilipata bao la kwanza dakika ya 35 mfungaji akiwa Haji Suleiman kutokana na pasi ya Mohammed Hamduni.

Red Sea licha ya kufungwa mchezo huo ilipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini umaliziaji haukuwa mzuri, ambapo itajutia zaidi nafasi iliyopata dakika ya 16 wakati Abraham Tedros alipoingia ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilipanguliwa na kuwa kona butu.

Red Sea ililazimika kucheza pungufu dakika ya 77 baada ya Aron Zekarias kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko Salum Shebe.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ambapo dakika ya 86 Said Rashid alifunga bao la pili kwa shuti lililoenda moja kwa moja wavuni.

Kulingana na taratibu za Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), timu tatu za Kundi A, pamoja na timu mbili za juu Kundi B na mbili za Kundi C zitacheza robo fainali pamoja na timu itakayokuwa na uwiano mzuri wa pointi kutoka Kundi B ama C.

Katika mchezo mwingine uliofanyika jioni kwenye uwanja huo timu ya Vital ‘O ya Burundi ambayo mchezo wa kwanza ilitoka 0-0 na Simba iliifunga Etincelles ya Rwanda mabao 3-1
Mabao ya washindi yalifungwa na Nzigamasabo Steive, Minzi Stanley na Mbakiye Babi wakati la Etincelles lilifungwa na Ochaya Sylvan.

Vital’O sasa imefikisha pointi nne kwa michezo miwili. Michuano hiyo inaendelea tena leo kwa mchezo wa Kundi B, ambapo Bunamwaya ya Uganda itacheza na Elman ya Somalia

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni