Jumapili, 26 Juni 2011

LOWASA AISHAURI SERIKALI


Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akichangia bungeni, makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2011/2012, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
ASEMA INAOGOPA KUFANYA MAAMUZI MAZITO
Kizitto Noya, Dodoma
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa ameiambia Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuwa inasumbuliwa na ugonjwa wa woga katika kutoa uamuzi magumu na matokeo yake mambo yake mengi hayaendi kama yalivyopangwa.Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika utawala huu wa awamu ya nne, pia akaitaka Serikali hiyo kubadilika.

Alisema kuwa ni bora kulaumiwa kwa kufanya uamuzi mgumu kuliko kulaumiwa kwa kutofanya uamuzi na kwamba Serikali inapaswa kufanya maamuzi bila kujali matokeo yake huku akipendekeza kwa kuanzia, ikope kwa kutumia rasilmali za nchi.

Alitoa kauli hiyo wakati akichangia hotuba ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2011/2012.
"Ni bora kulaumiwa kwa kufanya maamuzi kuliko kulaumiwa kwa kutofanya maamuzi kabisa,"alisema Lowassa.

Bila kueleza ni maamuzi gani ambayo serikali hiyo imeshindwa kufanya, Lowassa alisema ugonjwa wa viongozi kuogopa kufanya maamuzi ni hatari kwa uchumi wa taifa kwa kuwa kuthubutu ni msingi wa mafanikio katika nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi.

"Kuna ugonjwa wa kutokutoa maamuzi hapa na lazima tukubali kubadilike. Ni heri mtu ukosee kutoa maamuzi kuliko kukaa kimya kabisa, heri uhukumiwe kwa kutoa maamuzi kuliko ulaumiwe kwa kushindwa kutoa maamuzi,"alisema.

Lowassa alitoa kauli hiyo huku serikali ikionekana kushindwa kutatua matatizo mbalimbali yaliyoko nchini hivi sasa ikiwemo matatizo ya usafiri wa reli, msongamano na makontena bandarini na ujenzi wa bandari pamoja na taifa kukabiliwa na mgawo wa mara kwa mara wa nishati ya umeme uliodumu tangu mwaka 2006.

Kabla ya Lowassa hajasisitiza suala la kutoa maamuzi, alitumia muda mwingi kuishauri Serikali itenganishe Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na kueleza mafanikio ya chama tawala, CCM na Serikali katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuwa ni kubwa mno, hivyo inastahili kugawanywa kwa kuiondoa ofisi hiyo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

"Ofisi hii ni kubwa sana, kuna Maafa, Uratibu, Bunge, Uwezeshaji, Uwekezaji na Tamisemi. Tamisemi yenyewe pia imegawanyika katika mambo mengi sana.

Nashauri Serikali itafakari kuigawa Ofisi ya Waziri Mkuu ili Tamisemi iwe yenye kujitegemea. Kwa kuwa sehemu katika Ofisi ya Waziri Mkuu inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, haina budi kupunguziwa mzigo,"alisema.

Mbunge huyo alizidi kueleza, "Muundo huu wa sasa haufai. Tamisemi iwe inayojitegemea ili ifanye kazi zake vizuri zaidi kwani Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa mno na ina majukumu mengi." Kuhusu mafanikio ya CCM na Serikali, Lowassa alisema, sio vyema kubeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 50 baada ya uhuru au kuyatenganisha na mafanikio ya CCM.

"Miaka 50 ya Uhuru ni historia ya CCM na serikali yake, uongozi wake umefanya mengi na siyo vizuri mambo hayo yakabezwa. Watu wanabeza mafanikio hayo, tusiwakubalie. Miaka kumi tu iliyopita CCM imefanya mengi,"alisema Lowassa na kuendelea:


"Mwalimu aliwahi kusema, akija mtu jeuri na fedhuri akakuuliza Tanzania mna nini? Mwambie tuna amani. Tanzania tuna amani na kwa amani hiyo  tumejenga reli ya Tazara(Tanzania na Zambia), Watanzania wanajua na dunia inajua."

Aliendelea, "Kwa amani hiyo tumejenga shule nyingi za msingi na sekondari, Watanzania wanajua na dunia inajua, amani hiyo tumejenga Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho ni kikubwa katika ukanda wote wa Afrika Mashiriki na Kati, Watanzania wanajua na dunia inajua. Unawezeje kuiondoa CCM katika mafanikio hayo makubwa ya nchi yetu?."

Alisema pamoja na mafanikio hayo yote na yale ya uchumi wa nchi kukua kwa asilimia saba, bado nchi ni maskini na kwamba Serikali sasa inapaswa kuhakikisha uchumi huo unaonekana katika maisha ya kawaida ya Watanzania.

Lowassa alisema Serikali inapaswa kufanya maamuzi bila kujali matokeo yake na akapendekeza kwa kuanzia, ikope kwa kutumia rasilmali za nchi ili kujenga reli ya kati na kuboresha bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

"Tutumie utajiri wetu wa gesi kukopa ili tujenge reli na bandari, tufanye hili sasa. Kama tulijenga chuo kikuu kikubwa Afrika Mashariki na Kati, Udom, tutashindwaje kufanya hilo ?,"alihoji.

Akizungumzia matatizo ya jimbo lake la Monduli, Lowassa aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea chakula wananchi waliokumbwa na njaa mwaka jana na akaiomba tena ifanye hivyo mwaka huu kwa kuwa hali bado siyo nzuri.

"Nakupongeza wewe mheshimiwa spika kwa kuteuliwa kuliongoza bunge, nampongeza mheshimiwa waziri mkuu, mawaziri, manaibu mawaziri, wabunge wote na wapiga kura wangu wa Monduli,"alisema Lowassa alipoanza kuchangia hoja hiyo.

 Aliendelea, "Kwa kuwa wapigakura wangu wamenipa heshima kubwa kwa kunichagua tena kwa zaidi ya asilimia 90, nipende tu kuwaahidi kuwa nitawapa utumishi uliotukuka. Lakini, nasikitika sana kwa tatizo la njaa na kuishukuru Serikali kusaidia kuokoa maisha ya watu hao. Naiomba Serikali ipime tabianchi, ili tuone nini kitatokea tena ili kama ni kuhama, watu hao wahame."

Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumza bungeni tangu ajiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008 kwa sakata la zabuni tata iliyoipa kazi ya kufua umeme wa dharura Kampuni ya Richmond Development (LLC).

Viongozi wengine waliojiuzulu kutokana na kashfa  hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni