Jumatatu, 27 Juni 2011

EL MEREIKH YAILAZIMISHA SULUHU YANGA

BAO tata lililofungwa dakika ya 63 na Stephen Worgu jana lilifanya mchezo wa Yanga na El Merreikh ya Sudani umalizike kwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Kundi B la michuano ya Kombe la Kagame Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Worgu alifunga bao hilo kwa mpira ulionekana kama umegonga mwamba na haukuvuka mstari wa goli, lakini mwamuzi Mganda Dennis Batte akiashiria mpira uendelee.

Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1, huku wachezaji wa El Mereikh ya Sudani wakinyoosha mikono kulalamika kwamba mpira ulivuka mstari wa goli, kabla ya kipa Yaw Beko kuokoa.

Sekunde chache baadaye mwamuzi msadizi Simba Honore wa Rwanda alinyoosha kibendera juu kumpa ishara Batte kwamba mpira ulivuka mstari na kwamba lilikuwa bao, hivyo Batte kuashiria mpira uwekwe kati.

Ukiacha bao hilo, mchezo wa jana ulikuwa wa ushindani karibu dakika zote 90, huku Yanga ikitawala kipindi cha kwanza na wageni kudhibiti kipindi cha pili.

Yanga ilipata nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza, lakini Kenneth Asamoah, Davies Mwape, Julius Mrope na Rashid Gumbo kwa nyakati tofauti walishindwa kuzitumia.

El Merreikh nayo ilipata nafasi nyingi za kufunga, lakini mashuti ya washambuliaji wake ama yalishindwa kulenga lango ama yaliokolewa na kipa Berko.

Wachezaji Kelechi Osunwa, Wawa Pascal, Remi Adiko walikuwa wakiisumbua ngome ya Yanga lakini umaliziaji ulikuwa butu.

Katika mchezo huo Merreikh ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya pili mfungaji akiwa Osunwa kwa kichwa, kabla ya Yanga kusawazisha dakika tano baadaye baada ya beki Ahmed Albasha wa Merreikh kujifunga baada ya kumrudishia mpira uliomshinda kipa wake Isam Elhadari.

Yanga iliongeza mashambulizi na kupata bao la pili dakika ya 35 mfungaji akiwa Kenneth Asamoah.

Juzi wawakilishi wengine wa Tanzania Bara katika michuano hiyo Simba, ilitoka 0-0 na Vital ‘O ya Burundi mchezo wa Kundi A.

Yanga: Yaw Berko, Godfrey Taita, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Julius Mrope, Rashid Gumbo, Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah, Kigi Makasi.

El Merreikh: Isam Elkhadari (Gk), Saeed Mustapha, Badr Eldin, Ahmed Albasha, Nasr Eldin, Musab Omer, Kelechi Osunwa, Balla Gabir, Wawa Paschal, Karim Eddaffi na Remi Adiko.

Wakati huohuo, John Nditi anaripoti kutoka Morogoro kuwa timu ya APR ya Rwanda jana iliifunga Ports ya Djibouti mabao 4-0 mchezo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri.

Mabao ya APR ambao ni mabingwa watetezi yalifungwa na Nyirenda Victor aliyefunga mawili, Logbo Landry na Kwizera Ernest

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni