Jumatano, 1 Juni 2011

MLOKOLE AMUUA MWANAE WAKATI WA MAOMBEZI.


Mama mmoja wa nchini Marekani huenda akahukumiwa miaka 45 jela kwa jaribio lake la kutoa mashetani toka tumboni mwa mtoto wake, jaribio ambalo lilipelekea kifo cha mtoto huyo.Mama huyo, Latisha Lawson mwenye umri wa miaka 31 alidai kuwa mtoto wake wa kiume wa miaka miwili aliyejulikana kwa jina la Jezaih, alikuwa na shetani tumboni mwake linaloitwa "Marzon".

Ili kulitoa shetani hilo, Latisha aliandaa mchanganyiko wa mafuta ya alizeti na siki. Alimnywesha kinguvu mtoto wake huyo wa miaka miwili na kumfunga mdomo wake kwa nguvu ili kumzuia asitapike wala kuutema mchanganyiko huo.

Mtoto Jezaih alishindwa kupumua na matokeo yake alifariki dunia.

Akisomewa mashtaka ya mauaji mahakamani, Latisha aliiambia mahakama kuwa aliamini kuwa pepo baya lilimuingia mtoto wake wakati alipokuwa mjamzito kwani wakati huo hakuwa akimuabudu Mungu.

Mahakama iliambiwa kuwa Latisha pamoja na mwanamke mwingine waliwanywesha watoto wanne mchanganyiko huo ili kuyatoa mashetani waliyo nayo.

Watoto wengine walitapika mchanganyiko huo lakini Latisha alimzuia mwanae kutapika kwa kuufunga mdomo wake kwa nguvu.

Tukio hilo lilitokea mwezi novemba mwaka 2009. Baada ya kuona mtoto wake amefariki, Latisha alianza kuomba dua akimtaka Mungu amrudishe duniani mwanae kama alivyofanya kwa Lazarus kama maandishi yanavyosema.

Baada ya kuona hakuna kinachotokea, Latisha aliuchukua mwili wa mwanae na kuueweka kwenye mfuko wa rambo na kuuficha kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi alipokamatwa mwezi disemba mwaka jana, 2010.

Madaktari wa akili walimfanyia uchunguzi Latisha ambapo ripoti zao zilipelekea mahakama imuone Latisha ana hatia ingawa wakili wake alimtetea kwa kusema kuwa Latisha alikuwa hajui afanyalo wakati huo.

Latisha huenda akahukumiwa miaka 45 jela atakaposomewa hukumu yake mwezi ujao.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni