Jumanne, 14 Juni 2011

MAHAKAMA YAAMURU ASKOFU AKAMATWE

Askofu Valentino MOKIWA
Mussa Juma, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha imeagiza kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa na Askofu mpya wa Kanisa hilo aliyewekwa wakfu juzi, Stanley Hotay.Askofu Mokiwa, alimweka wakfu Hotay Jumapili, siku mbili tangu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutoa maagizo ya kusitishwa kwa shughuli hiyo.

Kitendo hicho cha Askofu Mokiwa kuendelea na mchakato wa kumweka wakfu Askofu Hotay pamoja na amri ya Mahakama kutaka shughuli hiyo isitishwe, kimeelezwa kuwa ni dharau kwa mahakama.

Sherehe za kuwekwa wakfu Askofu huyo zilifanyika juzi Makao Makuu ya Dayosisi ya Mount Kilimanjaro na zilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Claudio Bitegeko na maofisa kadhaa kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Uamuzi wa kukamatwa kwa maaskofu hao, ulitolewa jana na Jaji Kakusulo Sambo baada ya wakili wa mashtaka, Meinrad D’souza kuwasilisha maombi maalumu ya kutaka Mahakama Kuu itoe adhabu kwa Dk Mokiwa na Hotay kwa kukaidi amri ya Mahakama.

Akitoa uamuzi ambao ulichukua takriban saa moja, Jaji Sambo alisema haihitaji elimu ya chuo kikuu chochote kuona kuwa walichokifanya Maaskofu hao wa Anglikana ni dharau kwa amri halali ya Mahakama.

Alisema kitendo walichokifanya ni kudharau Mahakama tena Mahakama Kuu na kwamba kama hatua kali zisipochukuliwa, nchi haitatawalika katika misingi ya sheria.

“Nchi hii inaongozwa kwa misingi ya sheria  na Rais Jakaya Kikwete amekuwa akieleza kuwa kila mtu anapaswa kuheshimu utawala wa sheria. Inasikitisha kama viongozi wa dini wanakiuka sheria, tukiendelea hivi itakuwa tabu sana,” alisema Jaji Sambo.

Alisema mtu yeyote anayeishi Tanzania ni lazima atii na kuheshimu sheria zilizopo hata kama ni raia wa nchi nyingine.Jaji Sambo alisema wasomi wa sheria wanatambua kuwa, Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kifungu cha 37(2) kinaeleza namna ya kuwashughulikia watu wanaokiuka amri ya Mahakama.

Alisema Askofu Mokiwa ameeleza katika tamko lililowasilishwa Mahakamani jana kuwa alimweka wakfu Askofu Hotay kama Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, lakini hatua hii imekuja kabla ya Mahakama haijatoa uamuzi kwa shauri lililokuwa limefikishwa Mahakamani.

“Hii ni sawa sawa na mwenendo mzima wa kesi unakuwa hauna maana tena, kwani tayari Askofu anayelalamikiwa ameapishwa na taratibu za kumpata Askofu ni zilezile ambazo zimelalamikiwa, hivyo kutokana na hali hii, nimeridhika kuwa amri halali imekiukwa,” alisema Jaji Sambo.

Jaji Sambo alisema katika mazingira hayo, ni wazi kuwa kuna namna ya kuwashughulikia wanaokiuka amri halali ya Mahakama.

Alisema Sura 11 ya Kanuni ya Adhabu Cap 16 ya mwaka 2002, inaeleza kuwa ni makosa kuingilia chombo cha utoaji haki na imeeleza ni nini kinaweza kufanyika kwa atakayekiuka.

Jaji huyo alisema Kifungu cha 114 (i) C na K cha CPA, kinafafanua kosa la kuingilia mwenendo wa kesi Mahakamani na katika kifungu hichohicho, kipengele cha tatu kinaipa Mahakama mamlaka ya kumwadhibu mtu anayevunja sheria hiyo.

"Mtu yeyote ambaye anasababisha kuingiliwa kesi au kuvuruga mwenendo wa kesi yupo hatiani,” alisema Jaji Sambo na kuongeza kuwa kifungu cha 124 CPA kinafafanua kuwa mtu anayevunja maagizo ya Mahakama achukuliwe hatua.“Kwa mazingira haya uamuzi mdogo ambao ulipaswa kutolewa leo sitautoa hadi hapo nitakapopanga tena na wahusika watajulishwa.”

"Hivyo katika uamuzi huu wa sasa, naagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dk Valentine Mokiwa na mlalamikiwa wa pili, Stanley Hotay na taratibu za kujibu kosa hilo la jinai zianze."

Awali, Wakili D’souza alisema kitendo cha Askofu Mokiwa kumweka wakfu Hotay kimeingilia uhuru wa Mahakama na kimeshusha heshima ya Mahakama Kuu, kwani ilitoa agizo la kusitishwa shughuli zozote za kuapishwa kwa kiongozi hiyo.

Hata hivyo, Mawakili wa Utetezi, Joseph Thadayo na Issa Mavura waliomba Mahakama kutokubali maombi ya kuchukuliwa hatua Askofu Mokiwa na Askofu Hotay kwa maelezo kuwa hawakuingilia mwenendo wa kesi hiyo.

Thadayo alimkabidhi Jaji Sambo tamko la Askofu Mokiwa ambalo linaeleza kilichotokea kuwa Hotay amesimikwa kama Askofu wa Anglikana Tanzania na siyo Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.Mara baada ya uamuzi huo, Wakili Thadayo alisema hawana la kufanya zaidi ya kutekeleza maagizo hayo.

“Tutashauriana cha kufanya lakini kwa sasa ndiyo hivyo imeamriwa,” alisema Thadayo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni