KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, helikopta inayotumiwa na CCM katika kampeni za Igunga imeripotiwa kupotea ikiwa angani wakati ikijaribu kutafuta vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Dk Dalaly Kafumu.Taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo zilianza kuzagaa jana majira ya saa tano asubuhi mjini Igunga na baadaye zilithibitishwa na mmoja wa maofisa wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe kuwa walipotea mara kadhaa baada ya mtu wanayemtegemea kuwaongoza njia kupoteza ramani akiwa angani.
“Unajua tumemchukua mtu ambaye anaifahamu vizuri Igunga ili aweze kuielekeza helikopta mahala pa kwenda, lakini kwa bahati mbaya mtu huyo alipokuwa angani alishindwa kwa sababu ya kupoteza ramani,” alisema ofisa huyo.
Helikopta ya CCM.
Awali taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo zilitolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika katika Kata ya Nkinga jana asubuhi, akisema kuwa alipata habari kuwa helikopta ya CCM ilikuwa imepotea.Mmoja wa watu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo alisema walipotea mara kadhaa na kwamba katika harakati hizo walitua kwenye kijiji kimojawapo cha Wilaya ya Igunga jana saa nne asubuhi, lakini walijikuta kwamba wamekosea, hivyo kuondoka kwani watu hawakuwa tayari kwa mkutano huo.
January Makamba ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Siasa na Mambo ya Nje) alikanusha taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo na kuziita kuwa ni “uzushi wa kisiasa”.
Helikopta ya CCM ambayo iliwasili juzi asubuhi na kuanza kutumika katika kampeni, inadaiwa kutumia mmoja wa wenyeji wa wilayani hapo katika ziara yake kutokana na kutokuwapo kwa maandalizi ya ramani inayojulikana kama GPRS.
“Hatuna ramani ya kumwogoza rubani, hivyo tunafanya kazi hii kwa kutumia wenyeji wanaoifahamu vizuri Igunga, kama unavyojua huko angani wakati mwingine ni vigumu kutambua eneo na hili ni tatizo kwetu," alisema ofisa huyo.Helikopta hiyo ya CCM ilirejea mjini Igunga jana majira ya saa tisa alasiri na haikufahamika iwapo kurejea huko mapema kulitokana na matatizo hayo yaliyoelezwa.
Mratibu wa Kampeni za CCM Igunga, Mwigulu Nchemba hakupatikana kuzungumzia suala hilo na pale alipotafutwa kwa simu, ilikuwa ikiita bila majibu.
Masanduku ya Kura
Katika hatua nyingine, Chadema kimesema kuna njama za kuingiza kura bandia Igunga na kwamba tayari karatasi na masanduku ya kura yamefikishwa mjini Nzega kwa ajili ya kuingizwa Igunga siku ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana majira ya saa tano asubuhi katika Kata ya Nkinga, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema Chadema kina taarifa za uhakika kwamba tayari karatasi hizo zimeshawasili wilyani Nzega.
“Ndugu waandishi mlioko katika mkutano huu, hii ni taarifa rasmi ya chama na kwamba tuna taarifa za uhakika kwamba karatasi hizo zimehifadhiwa nyumbani kwa ofisa mmoja wa Serikali,” alisema Mbowe.
Aliendelea kusema kuwa tayari karatasi hizo zimeshapigwa kura na kudumbukizwa kwenye maboksi ya kupigia kura tayari kwa kuyaingiza kwenye vituo vya kupiga kura.
Mbowe alisema kuwa tayari vijana wa Chadema wameshakwenda Nzega kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha karatasi hizo haziingii Igunga.
Mbowe aliendelea kusema kuwa mpango huo wa CCM unatekelezwa kwa msaada mkubwa wa usalama wa taifa na kuonya kuwa iwapo zinaingia Igunga basi hapatakalika.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Chadema zimedai kuwa karatasi hizo pamoja na maboksi hayo ya kura yamehifadhiwa nyumbani kwa mkuu wa wilaya hiyo, taarifa ambazo zimekanushwa vikali na kiongozi huyo.
Mwananchi lilizungumza kwa simu na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Florence Horombe ambaye alisema kwamba, hana taarifa za kuwapo kwa masanduku hayo ya kura katika wilaya yake.
“Sina taarifa yoyote kuhusiana na karatasi hizo au jambo lolote kama hilo,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Nahodha: Hatumchagui mfalme Igunga
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha amesema Jeshi la Polisi litatumia ikiwezekana fedha zote lilizo nazo kuhakikisha kwamba linawapata wahusika wa kitendo cha kumwagiwa tindikali kwa mmoja wa wakazi wa Igunga, Mussa Tesha.Alisema mjini Igunga jana kuwa “tutafanya kila tuwezalo, tutatumia fedha zetu zote polisi tulizonazo, kuhakikisha watuhumiwa hawa wote wanne wanakamatwa na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria”.
Nahodha alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za viongozi wa vyama vya siasa mjini Igunga, mkutano ambao uliibua hoja kwamba mtuhumiwa aliyekamatwa kisha kufikishwa mahakamani George Salum, alionewa.
Nahodha alisema kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani wahusika wawe na subira na kwamba ikiwa mahakama itabaini kutohusika kwa mtuhumiwa huyo, basi ataachiwa.
Nahodha aliweka bayana kwamba juzi alimtembelea mtuhumiwa huyo gerezani na kubaini kwamba miongoni mwa wanaosakwa ni mtuhumiwa George Ernest Nyati na kwamba kufanana kwa majina hayo ndiyo chanzo cha manung’uniko hayo.
“Nimeambiwa kwamba yule mgonjwa (Tesha), anapata nafuu, sasa nami namuombea akipata nafuu hiyo hasa ya macho, tutaitisha gwaride la utambulisho na yeye atawatambua hata kama asipoweza kuwaona basi hata kwa sauti zao maana ni watu ambao aliwazoea na alikuwa akiwafahamu,”alisema Nahodha.
Katika mazungumzo yake waziri huyo alisema uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Igunga keshokutwa si wa kumchagua mfalme wala mwakilishi wa wananchi peponi, bali ni wa mbunge pekee.
Kutokana na hali hiyo, Nahodha ambaye yuko Igunga tangu Jumanne wiki hii alisema hakuna haja ya vyama vya siasa kuwa na uhasama na badala yake zifanyike siasa za kistaarabu ambazo zinawezesha wananchi wa Igunga kupata mwakilishi wanayemtaka.
“Ninachotaka kuwaeleza wenzangu hapa, ni kwamba hatuchagui mwakilishi wetu peponi, la hasha, ila tunamtafuta mbunge tu, hivyo kadhia hii yote haina maana, sidhani kama ni sahihi sana kuwa na mvutano mkubwa katika jimbo dogo tu la uchaguzi,”alisema Nahodha muda mfupi kabla ya kuingia katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa.
Nahodha alirudia kauli hiyo wakati alipozungumza na viongozi hao pale alipowaambia kwamba: “Hatumchagui mfalme wa Igunga”, hivyo kuwataka viongozi hao kuhakikisha wafuasi hao wanaendesha siasa za kistaarabu zisizo na uhasama.
Waitara wa Chadema alizungumzia suala la madai ya kutaka kutekwa kwa mbunge wa Viti Maalumu Ester Bulaya (CCM) na kurushiwa risasi ambapo baadaye kesi hiyo ilibadilishwa na yeye (Waitara) kutuhumiwa kurusha risasi huku polisi wakionekana kuegemea upande wa CCM."Ninachosema hapa kuwe na usawa wa kushughulikiwa matukio ya uhalifu na mtu anapofanya kosa, ashughulikiwe kama yeye na chama kisihusishwe, kwa sasa hakuna ugomvi na polisi bali ugomvi uliopo ni wa makada wa CCM na Chadema, hapa kuna uhasama nasema ukweli," alisema.
Waitara alitaka kuhakikishiwa juu ya ushiriki wa polisi katika mchakato wa kuchakachua kura kwa kuwa katika chaguzi zingine polisi wamekuwa wakihusishwa.Kada wa CCM, Shaibu Akwilombe alitaka kuwapo kwa utaratibu mzuri kwa ajili ya watu wanaosubiri matokeo utakaoepusha vurugu kwa kuwa sheria iliyopo inasema mtu akipiga kura akae umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura jambo ambalo alisema ni hatari iwapo watajikusanya wengi wakiwa na itikadi tofauti.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adam, alikiri kutokea kwa mfululizo wa matukio ya kujeruhiana, kuchaniana picha na mabango, lakini alikanusha matukio hayo kuhusishwa na CCM ambapo aliitupia shutuma nzito Chadema kuwa ndio imekuwa ikitajwa mara kwa mara kuhusika na matukio hayo.
Polisi: Hatutapendelea chama chochote Igunga
Wakati huo huo, uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora ukitarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili, Jeshi la Polisi nchini limeweka wazi msimamo wake kwa kusema: "Tutahakikisha hatutumiki kwa maslahi ya chama chochote cha siasa".Kadhalika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia kwa Mwenyekiti wake wa muda, Profesa Amon Chaligha imesema, itahakikisha uchaguzi wa Igunga unakuwa huru na wa haki na kwamba mshindi halali ndiye atakayetangazwa.
Polisi katika tamko lililotolewa na Kamishna wake wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja imesema itahakikisha upigaji kura unafanyika kwa amani, bila vikwazo wala bughudha, kulinda usalama wa vifaa vya kupigia kura na kuhakikisha mchakato wa kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo unakuwa wazi, huru na wa haki.Chagonja aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Igunga kuwa chombo cha umma, polisi watasimamia sheria, kanuni na taratibu zote za uchaguzi "bila upendeleo wowote" na kwamba usalama utaimarishwa kabla, wakati na baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
"Jeshi la polisi litaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu zote bila upendeleo wowote. Kama chombo cha Umma, litahakikisha halitumiki kwa maslahi ya chama chochote cha siasa," alisema Chagonja.
Uchaguzi mdogo wa Igunga unatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili, Oktoba 2, 2011 na vyama vinane vimesimamisha wagombea wakiwania kurithi nafasi iliyoachwa wazi na mbunge aliyejiuzulu, Rostam Aziz kutoka CCM.
Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Geofrey Nyang'oro na Daniel Mjema, Igunga
CREDITS; Gazeti la Mwananchi.