Ijumaa, 16 Septemba 2011

WALIOLIPUA MABOMU MGAHAWA WA WAETHIOPIA UGANDA WAHUKUMIWA

 
Eneo lilokumbwa na mashambulio ya bomu
Eneo lilokumbwa na mashambulio ya bomu
Raia wawili wa Uganda wamehukumiwa kifungo gerezani kwa kuhusika na mashambulizi ya bomu mwaka 2010 ambayo yalisababisha vifo vya watu 76 katika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Edris Nsubuga, ambaye amekiri kutega mabomu amehukumiwa miaka 25 gerezani, ihali Muhamoud Mugisha amehukumiwa kifo cha miaka mitano kwa kuhusika katika njama ya kufanya mashambulizi hayo .
Wanamgambo wa Kiislamu wa Somalia al-Shabab walisema walitekeleza mashambulio hayo .
Mabomu hayo yalitegwa katika mkahawa mmoja ambao pia ulikuwa na sehemu ya baa ambako watu walikuwa wamekusanyika kutazama fainali ya kombe la dunia katika televisheni.
Al-Shabab, kundi ambalo linahusishwa na mtandao wa al-Qaeda, linasema kuwa mashambulio hayo yalifanywa kulipiza kisasi cha jeshi la Uganda kuunga mkono serikali ya mpito ya Somalia.
Edris Nsubuga ambaye alikuwa akabiliwe na hukumu ya kifo ,ameepuka hukumu hiyo baada ya kukiri makosa yake.
Mapema wiki hii alikiri mashtaka matatu ya ugaidi yanayohusisha pia "nia ya kupeleka na kutega mabomu".
Natumai atatumia wakati wake gerezani kutafakari aliyoyatenda ambayo yamenilazimu nimuweke kando na jamii
Jaji Alfonse Owiny-Dollo
Jaji Alfonse Owiny-Dollo alisema kuwa Nsubuga aliomba msahama na kusema alitumiwa wakati ambapo hangeweza kufanya maamuzi yafaayo kwani wakati huo alikuwa anakabiliwa na matatizo mengi ya nyumbani.
Muhamoud Mugisha nae alikiri kuhusika na njama za kutenda vitendo vya kigaidi.
Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo mwaka jana Mugisha alisema anauhusiano na al-Qaeda.
Washukiwa wengine 12 wamekanusha mashtaka hayo na kesi yao inaendelea.
Washukiwa watano walifutiwa mashtaka dhidi yao kutokana na upungufu wa ushahidi, walikuwa nipamoja mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya Al-Amin Kimathi ambaye alizuiliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja korokoroni.
Alikuwa ameishutumu serikali ya Kenya kwa kuwahamisha kinyume na sheria washukiwa hadi Uganda na alikuwa amekwenda Uganda kuwapa ushauri washukiwa hao wakati alipokamatwa na kuzuiliwa.
Amesema alikuwa anaadhibiwa kwa kazi yake ya kutetea haki za binadamu ambayo ilifichua mpango wa washikiwa kusafirishwa kwa siri hadi nchi nyengine ambako hufanyiwa mahojiano na maafisa wa upelelezi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni