Ijumaa, 9 Septemba 2011

MCHUNGAJI MTIKILA ALILIA JENGO LA MAHAKAMA YA RUFAA LISIUZWE.

Mch. Mtikila.

 
Mwenyekiti wa Democratic Party, DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi akipinga kuuzwa jengo la Mahakama ya Rufani Tanzania.

Mtikila alifungua kesi hiyo leo Septemba 9, 2011 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, ambayo imepewa namba 23/2011 na walalamikiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Mtikila anadai jengo la mahakama hiyo ni miongoni mwa majengo ya kumbukumbu na historia, ambayo yanapaswa kuhifadhiwa. Anadai jengo hilo licha ya kuwa la kihistoria na utamaduni, pia ni urithi wa vizazi vijavyo na ni kosa kulifanyia mabadiliko yoyote.

Mtikila anadai jengo hilo lilipokabidhiwa kwa Idara ya Mahakama, Serikali ililifanyia ukarabati uliogharimu shilingi bilioni mbili ili likidhi mahitaji ya kuwa Mahakama ya Rufani. Anadai hilo lilitokana na kuongezeka kwa shughuli za mahakama, anadai kutokana na hilo, lilijengwa jengo lingine la ghorofa mbili nyuma ya jengo la zamani, kwa gharama ya sh. bilioni 1.3. Pia  ilikubaliwa kujengwa sanamu ya Jaji Mkuu wa kwanza, hayati Augustino Said kama kumbukumbu yake.
Anaiomba Mahakama itamke kuwa, walalamikiwa wana wajibu wa kulihifadhi jengo hilo kulingana na sheria za uhifadhi wa mali za kale; Pia iwazuie walalamikiwa kulitoa na kulivunja jengo hilo, badala yake lihifadhiwe kulingana na sheria ya mali za kale.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni