Jumamosi, 10 Septemba 2011

MANJI AWASHTAKI KAGODA, KAINERUGABA NA WENZIE, HII KALI SUBIRI TUONE MWISHO WAKE!!!!

BAADA ya mwanaharakati na mwanasheria Kainerugaba Msemakweli, kuibua tena kashfa ya Kagoda, akimhusisha mfanyabiashara Yusufu Manji, kesi kubwa ya aina yake imefunguliwa jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria na Mwanaharakati Msemakweli Kainerugaba,mmoja wa walalamikiwa na Manji.


Kesi hiyo iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mfanyabiashara Manji jana, inahusisha pia mfanyabiashara mwingine maarufu, waandishi wa habari na mwanasheria aliyewahi pia kufanya kazi katika moja ya kampuni zake na Kagoda yenyewe.

“Manji ameshitaki zaidi ya watu saba na taasisi mbili na inamhusisha mfanyabiashara, ambaye kwa madai ya Manji, katika siku za karibuni, ameonekana kuikingia kifua kampuni iliyochota mamilioni ya fedha katika Akiba ya Akaunti za Kigeni EPA kutoka Benki Kuu ya Tanzania,” kilisema chanzo cha habari hii kutoka mahakamani.
Mlalamikaji Yusuph Manji.


Katika kesi hiyo ambayo tayari imefunguliwa jalada na kupewa namba 135/2011, Manji anaiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa wake, kumlipa Sh bilioni 100 kama fidia, kwa kumtapeli wakishirikiana na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Wanaoshitakiwa na Manji pamoja na mwanasheria huyo ni mmoja wa wahariri gazeti la Mwanahalisi na mwandishi wa habari wa siku nyingi.

Mwandishi huyo kwa mujibu wa chanzo chetu ndiye anadaiwa kuandaa mkutano wa Msemakweli na vyombo vya habari ambapo alitamka kwamba Manji ni mmoja wa wamiliki wa Kagoda. Msemakweli naye ni mlalamikiwa katika kesi hiyo.

Kainerugaba pia anakabiliwa na kesi kadhaa zilizofunguliwa na wabunge aliowatungia kitabu kikiwatuhumu kwamba wanatumia vyeti feki kutoka taasisi za kielimu. Wabunge hao wanamtaka athibitishe kauli yake au awalipe mamilioni ya fedha.

Wengine wanaoambatanishwa katika kesi hiyo ni pamoja na wafanyakazi wa zamani wa kampuni ya Quality Group pamoja na taasisi nyingine ya binafsi ambayo Manji anadai ina uhusiano na Kagoda.

Manji katika kesi hiyo, anadai kuwa watu hao kwa pamoja na taasisi hizo, wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha Kagoda, inajilinda na mkono wa sheria ili isilipe madeni inayodaiwa na serikali pamoja na Kampuni ya Quality Finance Corporation ambayo ni mlalamikaji wa pili na ambaye ndiyo iliyekopa fedha kutoka Kagoda.

Wakati Manji akiyafanya hayo, Msemakweli naye amesema anadhamiria kumfungulia kesi Mahakama Kuu akimdai fidia ya Sh bilioni 500 kwa alichodai ni kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari.

Akizungumza jana, Msemakweli alisema Septemba 8 vyombo vya habari viliandika na kusambaza habari za kumkashifu kutoka kwa Manji kama kukanusha shutuma zinazomkabili kuhusu kampuni ya Kagoda.

“Taarifa ya Manji imejaa matusi na kejeli dhidi yangu. Anadai mimi ni mtunzi wa vitabu vya kukashifu watu ... nitamfikisha mahakamani na kumdai fidia kwa kuwa kashfa aliyonitolea ina athari ya muda mrefu katika maisha yangu,” alisema.

Alisema ingawa Manji anadai kuwa hajasoma, ukweli ni kwamba amesoma na mwaka 2008 alitunukiwa Shahada ya Sheria na sasa anasoma Shahada ya Uzamili ya Sheria ya Matumizi ya Teknolojia ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Chanzo; HabariLeo na Mitandao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni