Jumatano, 21 Septemba 2011

MAHITA AKUBALI AMRI YA MAHAKAMA

Bw. Omari Mahita.

 
Hatimaye, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omar Mahita amekubali kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kuhusu mtoto aliyekuwa akimkataa kwamba si wake, ambaye alizaa na mtumishi wake wa ndani, Rehema Shabani.

Jana Mahita alilipa gharama za malimbikizo ya matunzo ya kumhudumia mtoto huyo kuanzia mwaka 2003 hadi siku ya hukumu ilipotolewa Septemba mwaka juzi, ambapo alilipa Shilingi milioni 9 kupitia kwa wakili wake, Charles Semgalawe kwa kampuni ya udalali ya Nasm Auction Mart ambayo ilipewa jukumu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kufuatilia fedha hizo, na kuahidi kulipa Shilingi milioni 3 zilizobaki baada ya siku 30 kuanzia jana.
Mtoto Juma na mama yake.


Mahakama hiyo pia ilimtaka Mahita kulipa Sh 100,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto huyo baada ya kulipa Sh milioni 12 hizo.

Uamuzi wa Mahakama ulitokana na Mahita kugoma na hivyo mama wa mtoto kurudi mahakamani na kutoa taarifa. Mtoto wao, Juma Mahita kwa sasa anasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Hananasif Kinondoni.

Kampuni ya Nasm Auction Mart  ilitoa notisi ya siku 14 kwa Mahita awe amelipa fedha hizo, vinginevyo hatua ya kutumia nguvu kukamata mali zake ingetumika.  Notisi hiyo ilikuwa inamalizika jana na kwa kuwa sehemu ya fedha hizo ilitolewa na kuhidi kumaliza kiasi kilichobakia ndani ya siku 30, hatua ya kutumia nguvu iliondolewa.

Katika kesi hiyo, Mahakama ya Kinondoni ilijiridhisha kuwa mtoto huyo ni wa Mahita kutokana na ushahidi wa upande wa mlalamikaji uliowasilishwa mahakamani hapo, ukiwapo wa vipimo vya vinasaba (DNA).

Hata hivyo, Mahita alikata rufaa kupinga hukumu hiyo, rufaa ambayo nayo ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu.

Katika uamuzi wa rufaa hiyo, Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu, aliunga mkono hoja za wakili wa mlalamikaji  kuwa ingawa sheria inatamka fidia ya Shilingi 100/- lakini mahakama inaweza kuangalia hali ya maisha na uwezo wa mlalamikiwa na hivyo kuweza kuongeza kiwango hicho.  Alisisitiza kuwa katika shauri husika, kiwango kilichoamuriwa na Mahakama ya chini kilizingatia hali ya kiuchumi hususan gharama za maisha na uwezo wa mrufani kuweza kulipa na kwa mujibu wa barua kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwenda kwa Mahakama, mrufani hakuweza kufika kwa ajili ya uchunguzi mara sita kwa nyakati tofauti.

Jaji Twaib akasema Mahakama ya Kinondoni ilikuwa sahihi na hivyo kumtaka Mahita kulipa pia gharama za kesi hiyo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni