Alhamisi, 8 Septemba 2011

UANDISHI USIOFUATA MAADILI WAADHIBIWA, GAZETI LAAMULIWA KUOMBA RADHI.

KAMPUNI ya Magazeti ya New Habari Ltd kupitia magazeti yake ya Mtanzania na Rai, imeamriwa na Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), kuwaomba radhi Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib kwa kutoa machapisho ya kuwadhalilisha mbele ya jamii.
Mh. Seif Khatib.


Akitoa uamuzi Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema baada ya kupitia maelezo ya pande mbili, imejiridhisha kuwa walalamikaji wana hoja na mlalamikiwa ameshindwa kutoa vielelezo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Katika shauri hilo, Sumaye alituma malalamiko yake dhidi ya Mtanzania kwa kuandika tahariri katika toleo lake namba 5270 la Oktoba mwaka jana yenye kichwa cha habari: “Usafi wa Sumaye umeanza lini?”

“Tahariri ile imenivunjia heshima na kuniumiza sana na imeniweka katika hali ambayo watu wananishangaa na kujiuliza kuwa mimi ni mtu wa aina gani,” alisema Sumaye wakati akitoa taarifa ya malalamiko yake mbele ya Kamati hiyo ya Maadili.

Alisema katika tahariri hiyo ambayo iliandikwa baada ya kauli aliyoitoa dhidi ya mafisadi, ilimtaja Sumaye kama mchoyo, mpotoshaji na mwizi na kueleza kuwa katika kipindi chake cha uwaziri mkuu, aliwahi kuwanyang’anya wananchi mashamba na kujiwekea mfukoni zaidi ya Sh milioni 500, jambo ambalo si la kweli.

Naye Khatib alisema kupitia gazeti la Rai toleo namba 919 la Mei 5, mwaka huu lililochapisha makala yenye kichwa cha habari: “Vurugu kitatangemdemani kutakalikaje,” lilimtolea tuhuma sita zenye kumdhalilisha mbele ya jamii huku zikiwa si za kweli.

Alisema tuhuma hizo ni pamoja na madai kuwa amenuna baada ya kukosa nafasi ya uwaziri na amekuwa akimsema pembeni Rais Jakaya Kikwete baada ya kukosa nafasi hizo; huku sifa yake kuu ni kiongozi wa Hizbu katika brass bendi ya ZNP na kuuza asumin.

“Kwa Wazanzibari wanafahamu ukiitwa Hizbu maana yake, lakini mbaya zaidi ukiambiwa unauza asumin maana yake (tusi la nguoni). Waniambie nimeuza wapi na kwa bei gani, pia wamenituhumu kuwa nimejipendekeza kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na kujitoa kugombea urais, wanithibitishie lini nilichukua fomu,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Mwakilishi wa magazeti hayo, Balinagwe Mwambungu, alikiri machapisho hayo yalikuwa na makosa ya kimaadili na hakuna vielelezo vyovyote vya kusaidia utetezi wa magazeti hayo kutokana na Mhariri wa Mtanzania kuacha kazi bila kuacha vielelezo na mwandishi wa Rai aliyeandika makala hiyo kutofahamika.
Mh. Fredirick Sumaye.


Jaji Mihayo akihitimisha, alilitaka Mtanzania kumuomba radhi Sumaye katika ukurasa wa mbele ndani ya siku saba na magazeti yake mengine likiwemo la Kiingereza na Rai kumuomba Khatib radhi ndani ya siku 14.

Kamati hiyo pamoja na Jaji Mihayo, ilikuwa na Katibu wake ambaye ni Katibu Mtendaji wa MCT Kajubi Mukajanga, wajumbe ni Rose Haji, Kenneth Simbaya, Rafi Haji Makame na Usu Malya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni