Ijumaa, 1 Julai 2011

WANAFUNZI WALIOSIMAMISHWA UDOM KUANZA KUREJEA KUANZIA KESHO.

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimetangaza kuwarejesha chuoni kuanzia kesho wanafunzi wote wa mwaka wa tatu wa Shule ya Sanaa na Sayansi ya Jamii waliosimamishwa masomo, huku 15 hatima yao ikisubiri taarifa binafsi kutoka mamlaka husika.
Majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma


Kwa mujibu wa tangazo katika tovuti ya Udom Juni 30, wanafunzi hao wanatakiwa kuripoti chuoni kesho saa nne asubuhi isipokuwa 15 wanaosubiri uamuzi wa mamlaka husika kabla ya kurejeshwa.

Aidha, katika tangazo hilo lililotolewa na Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo, wanafunzi ambao wanadaiwa ada, gharama za malazi, mitihani na gharama nyingine, hawatakubaliwa kurejea.
“Kwa taarifa hii, wanajulishwa kuwa usajili utafanyika Jumamosi tarehe 02/07/2011 na Jumapili tarehe 03/07/2011 tu.

Kila mwanafunzi anatakiwa kuja na nakala halisi za vithibitisho vya malipo ya ada na gharama nyingine ambazo alikuwa anadaiwa,” ilieleza taarifa hiyo ya Makamu Mkuu wa Chuo.

Ilieleza kuwa mwanafunzi ambaye hatatimiza masharti hayo, hatapokewa chuoni; na kwamba mitihani itaanza Jumatatu.

Awali, ilikuwa ianze Juni 20 hadi Julai 14.

Taarifa hiyo iliwataja wanafunzi 15 watakaopewa taarifa zao binafsi na mamlaka husika ni Salumu Tindo, Edwin Tairo, Pascal Ngaiza, Baraka Messo, Very Melchiory, Vincent Emmanuel, Alfred Boniface, Alex Mushi, Geofrey Msangi, Samora Julius, Romano
Baradyana, Moses Goodness, Bakari Seleman, Hassan Ally na Mustafa Shaaban.

Kwa maelezo hayo, bila shaka wanafunzi hao wanasubiri maelekezo kutoka kwa Kamati ya Nidhamu juu ya ushiriki wao katika mgomo na maandamano yaliyofanyika hivi karibuni.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa sehemu maalumu ya mapokezi na usajili, itakuwa kwenye kiwanja cha mpira wa miguu kilichoko meta 200 kutoka Ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dodoma (Duwasa), mkabala na zinapojengwa ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hivi karibuni, wanafunzi hao walisimamishwa baada ya kuanzisha maandamano na vurugu kwa siku mbili wakishinikiza malipo yao ya masomo kwa vitendo.

Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kwamba hata kabla ya kufukuzwa kwa wanafunzi hao, chuo kilishapanga kuwataka wanafunzi wote kulipa madeni wanayodaiwa na chuo, hivyo yeyote atakayekuwa anadaiwa hatapokewa hata kama hana hatia.

Akizungumzia jinsi ya kurudi chuoni, alisema Kamati ya Nidhamu ilikuwa inakutana na kuchambua wanaodaiwa kuhusika na wasiohusika katika mgomo.

Alisema wanafunzi wa mwaka wa tatu wasio na hatia watarudi mapema iwezekanavyo ili wafanye mitihani yao ya mwisho na kurejea kwao; wakati awamu ya pili, watarejea wa miaka mingine wasio na hatia kisha watakaogundulika kuwa na hatia, watapewa nafasi ya kujitetea ili haki itendeke kisha watarejea chuoni.

Alisema hatua hiyo pia itahusisha wanafunzi wa Shule ya Elimu ya Sayansi ya Habari (CIVE) waliofukuzwa chuoni miezi mitatu iliyopita, kwa kusababisha vurugu na maandamano.

Akizungumzia idadi ya wanafunzi waliofukuzwa, alisema kabla ya kufungwa kwa chuo hicho, wanafunzi 400 waligundulika kuwa vinara wa kuhamasisha migomo na maandamano huku wengine wakiomba kuondoka.

Alisema baada ya chuo kuwasimamisha wanafunzi hao, ndipo wengine walijichanganya na kuanza kufanya vurugu wakitaka hao wengine wasiondoke, hivyo kusababisha chuo kufungwa na wanafunzi zaidi ya 9,000 kusimamishwa masomo.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Udom umepokea na kuidhinisha mapendekezo ya Kamati ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu ya kupandisha vyeo watu sita wa Utawala na watatu wanataaluma.

Wanataaluma waliopandishwa vyeo ni Dk. Macheyeki kutoka Mhadhiri kuwa Mhadhiri Mwandamizi; Profesa Gesase kutoka Profesa Mshiriki kuwa Profesa kamili na Dk. Mtalikwa kutoka Mhadhiri Mwandamizi kuwa Profesa Mshiriki

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni