Ijumaa, 1 Julai 2011

YANGA YAIBANJUA ELMAN

Mshambuliaji wa Yanga Divies Mwape akiwania mpira mbele ya beki wa Elman saad Salah hasein wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana Picha na Jackson Odoyo
Clara Alphonce, Dar na Doris Maliyaga, Morogoro
"TUMERUDI, moto huu hadi ubingwa." Ni kauli ya kocha msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro alipokuwa akijitapa baada ya mchezo wa timu yake na Elma ya Somalia uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mchezo huo wa Kundi B wa Michuano ya Kagame uliofanyika kwenye Uwanja wa taifa, umeifanya Yanga kufikisha pointi nne sawa na Bunamwaya ya Uganda inayoongoza kundi hilo kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Bunamwaya iliyoifunga Elman mabao 4-0, jana ilitoka sare ya 1-1 na El Merreikh ya Sudan ambayo sasa ina pointi mbili baada ya sare ya Yanga ya 2-2 mchezo wa kwanza. Bunamwaya yenyewe ina mabao matano na imefungwa moja wakati Yanga ina mabao manne lakini imefungwa mabao mawili.

Elman haina pointi katika kundi hilo, Yanga itacheza mechi yake ya mwisho Jumapili dhidi ya Bunamwaya.

Minziro alisema kuwa moto wa Yanga hautazimika hadi fainali na hiyo ni kutokana na usongo iliyokuwa nao kuwa nje ya mashindano tangu mwaka 2008.

Ukiacha hayo, Yanga ilianza mchezo wa jana kwa kasi na kushambulia lango la Elman karibu vipindi vyote, lakini washambuliaji wake, Kenneth Asamoah, Davis Mwape na Julius Mrope walishindwa kujipanga kupachika mabao.

Yanga ingeweza kutumia nafasi zaidi kwani Elman muda mwingi walikuwa hawashambulii zaidi ya kulinda lango lao licha ya kufungw amabao hayo.

Hata hivyo, Yanga iliandika bao katika dakika ya 27, kupitia kwa Mwape baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Godfrey Taita. Dakika ya 42, Nurdin Bakari alishindwa kuunganisha wavuni krosi ya Mrope baada ya kupiga kichwa ambacho kilipaa juu na kutoka nje.

Dakika ya 44, Elman ilipeleka shambulizi kwenye lango la Yanga, ambapo Mohamed Abubakar waalikosa bao baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga na kupiga shuti ambalo lilitoka nje.

Safu ya ulinzi ya Elman ilikuwa imara kwa muda mwingi wa mchezo pamoja na Yanga kufanya mashambulizi ya mara kwa mara huku Elman ikionekana haitaki kufungwa idadi kubwa ya magoli.

Dakika ya 87, Hamis Kiza wa Yanga alikosa bao baada ya kupishana na krosi ya Mrope, na muda mfupi baadaye kocha wa Yanga, Sam Timbe alimtoa Mrope na kumuingiza Shadrack Nsajigwa aliyekuwa kwenye fungate la harusi wakati Asamoah alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Jerry Tegete.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kuongeza nguvu katika ushambuliaji na Kiza aliipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 90.

Akilizungumzia pambano hilo, kocha wa Yanga, Sam Timbe alisema wachezaji wake walicheza chini ya kiwango kwa sababu muda mwingi walikuwa wanatembea uwanjani.

Awali Bunamwaya na El Merreikh zilifungana bao 1-1, huku El Merreikh ikitangulia kupata bao katika dakika ya 32 baada ya beki wa kati wa timu hiyo, Sergi Pascal kukokota mpira kutoka katikati ya uwanja na alipofika kwenye 18 alipiga shuti lililokwenda moja kwa moja nyavuni.

El Merreikh inaonekana ina bahati mbaya ya kujifunga katika mashindano haya kwa sababu ilipigwa kona na nahodha wa Bunamwaya, Kimuli Robert akaruka juu kuucheza mpira huo, lakini beki wa El Merreikh, Mustafa alijikuta akiunganisha mpira golini kwake na kujifunga kwa kichwa katika dakika ya 38.

Mjini Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, Ulinzi ya Kenya ilipanda kileleni mwa Kundi C baada ya kutoa onyo kali kwa kuichapa mabao 9-0 Port FC ya Djibouti.

Mpaka mapumziko Ulinzi ilikuwa imeishachapa Ports mabao 4-0. Bao la kwanza la Ulinzi lilifungwa katika dakika ya 13 mfungaji akiwa Steven Waruru kwa mkwaju wa penalti baada ya Mohamed Ahmed kumchezea vibaya George Otieno.

Bao la pili lilifungwa katika dakika ya 18 mfungaji akiwa Lawrence Owino aliyemalizia krosi ya Stephen Waruru. Waruru aliifungia tena Ulinzi bao la tatu katika dakika ya 31 kwa shuti kali. Bao la nne lilifungwa na Lawrence Owino katika dakika ya 42.

Katika mechi hiyo Port waliokuwa wakicheza kichovu huku kipa wao Khalid Ally akionekana kutojiamini langoni, hata kucheza chini ya kiwango.

Ulinzi ilianza kipindi cha pili kwa kasi na katika dakika ya 49, ilipata bao la tano lililofungwa na Lawrence Owino kwa penalti tena baada ya beki wa Ports kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Dakika ya 53, Ulinzi ilipata bao la sita lililofungwa na Evance Amwoka kwa shuti kali.  Amwoka aliingia kuchukua nafasi ya Waruru.

Ulinzi ilipata bao la saba katika dakika ya 60 mfungaji akiwa Vincent Onyango aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Ismail na bao la nane la Ulinzi lilifungwa na katika dakika ya 65 na Vincent Onyango.

Wakati wa mapumziko Port walimtoa kipa wao Khalid Ally aliyekuwa amefungwa mabao manne akaingia Mohamed Said na yeye alifungwa mabao matano pia, idadi ya magoli iliendelea kuongezeka katika dakika ya 76 baada ya Mohamed Hussein kuifungia Ulinzi bao la tisa.

Kocha wa Ulinzi alisema wachezaji wake wamejituma hata kupata mabao hayo lakini kocha wa Ports, Mahmoud Ahmed alilalamikia Uwanja wa Jamhuri kuwa hauna sifa.

Katika mechi iliyofuatia ambayo ilitarajiwa kuwa na ushindani mkali St. George ya Ethiopa waliwachapa mabingwa watetezi, APR mabao 3-1.

Bao la kwanza la St. Goerge lilifungwa katika dakika ya 18 na Suleiman Mohamed, lakini katika dakika ya 23 Jean Cloud Iranzi aliisawazishia APR kwa bao murua.

Washindi walipata bao la pili lililofungwa na Prince Godwin katika dakika ya 51 baada ya mchezaji huyo kuwalamba chenga mabeki wa APR na kufunga bao hilo kirahisi.

Prince ambaye ni raia wa Ghana alifunga bao la tatu katika dakika ya 52 kwa shuti kali  lililomshinda kipa, Jean Cloud Ndoli.

Michuano hiyo inaendelea leo kwa pambano kati ya Simba ambayo itamkosa Ulimboka Mwakingwe aliyeumia itakapocheza na Etincelles ya Rwanda, pambano litakalotanguliwa na mechi kati ya Red Sea ya Eritrea na Vital'O ya Rwanda

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni