Jumanne, 12 Julai 2011

TAKUKURU KUINGIZA ELIMU YA RUSHWA KWENYE MTAALA WA SEKONDARI.


Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hosea
Raymond Kaminyoge
TAASISI  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Temeke, imeanza kutoa mafunzo ya rushwa kwa walimu ikiwa ni maandalizi ya kufundisha somo hilo shule za sekondari.
Hatua hiyo inafuatia mpango wa serikali kuliweka somo la rushwa kwenye mitaala ya sekondari, ili kufanya jamii kuwa na maadili mema ya kuchukia rushwa.
Hata hivyo, walimu hao walisema licha ya kufundisha somo hilo shuleni, rushwa itaendelea iwapo mishahara itaendelea kuwa midogo.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Beutoz Mbwiga, alisema mafunzo hayo yatawasaidia walimu wanaofundisha somo la uraia kuwajenga wanafunzi wao kwa maadili, hivyo kuchukia rushwa.
“Wanafunzi wakifundishwa kuhusu madhara ya rushwa wakiwa shuleni, wataichukia na kupambana nayo maishani mwao,” alisema Mbwiga.
Mbwiga alisema athari za rushwa kwa sekta ya elimu, zimekuwa zikisababisha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
“Kiwango cha elimu kinashuka kwa sababu mitihani inaweza kuvuja kutokana na watendaji kupewa rushwa,” alisema Mbwiga.
Aliongeza kuwa vurugu na migomo ya wanafunzi inayotokea kwa baadhi ya shule, ni mojawapo ya athari za rushwa.
Mbwiga alisema sababu za kuwapo rushwa ni mmomonyoko wa maadili, kupenda kuishi maisha ya kifahari, kipato duni na kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Sekondari ya Temeke, Hilde Mchomba, alisema watu hawataacha kuchukua rushwa kama mishahara itaendelea kuwa midogo.

“Hata kama tutawafundisha wanafunzi kuwa na maadili mema na kuchukia rushwa, lakini kama mishahara yao itakuwa haitoshelezi mahitaji watalazimika kuchukua ili kujikimu,” alisema mwalimu huyo.
Mwalimu Mchomba alisema mafunzo hayo yanatakiwa kwenda sanjari na serikali kupanga viwango vya mishahara itakayowezesha wafanyakazi kujikimu kwa mwezi mzima, vinginevyo mapambano  hayo hayatafanikiwa.
Naye Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Esther Mkokota, alisema wameanza kutoa mafunzo hayo kwa walimu 25.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni