Jumatatu, 4 Julai 2011

MINARA YA SIMU HAINA MADHARA-TCRA

MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA), hivi karibuni iliendesha mafunzo maalumu kwa wadau mbalimbali wa mawasiliano mkoani Ruvuma. Mafunzo yalitolewa katika wilaya za Namtumbo, Songea Mjini, Mbinga na Wilaya mpya ya Mbaba Bay.

Ili kuhakikisha kwamba kila mdau ananufaika na mafunzo hayo, Mamlaka hiyo ilitoa mafunzo
kwa watu wa kada mbalimbali kama vile maofisa wa Serikali wa ngazi ya juu wa mkoa huo, wanafunzi wa sekondari, walimu, na makundi mengine ya kijamii kama vile wakulima,
wafanyabiashara ndogo na walemavu.

Mafunzo hayo hayakuwabagua watu hata kidogo badala yake yalisababisha kuwaweka
pamoja katika suala zima la kujua haki zao za msingi katika huduma za mawasiliano nchini
zinazosimamiwa na Mamlaka hiyo.

Baadhi ya mambo waliofundishwa ni pamoja na mfumo mpya wa huduma za Posta, uitwao
Postikodi mpya zenye tarakimu tano, ambazo zitamtambulisha mtu mahali anapoishi ili
aweze kufikishiwa huduma za Posta kama vile vifurushi na barua kwa urahisi zaidi kuliko
ilivyo sasa; Jinsi ya kufikisha malalamiko ya huduma za mawasiliano pindi mteja au mdau
wa mawasiliano anapopata tatizo kama vile ukiukaji wa mikataba kati ya wateja na kampuni
za simu.
MINARA YA SIMU(Picha; John P. Mzava)

Mambo mengine yalizungumziwa katika mafunzo hayo ni haki za watumia huduma za
mawasiliano na wajibu wa watoa huduma za mawasiliano kama vile kampuni za simu. Aidha
wananchi mbalimbali waobahatika kupata mafunzo hayo walijifunza kuhusu mfumo mpya wa utangazaji uitwao Digitali badala ya ule wa zamani huitwao Analogia.

Mafunzo hayo ambayo yalitolewa na maofisa waandamizi kutoka Mamlaka hiyo kama vile Mkurugenzi wa Sheria, Elizabeth Nzagi, Meneja Mamlaka hiyo wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Deograsias Moyo na Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo anayeshughulikia masuala ya watumiaji, Richard Kayombo na mtaalamu wa masuala ya Huduma za Posta, Abel John, yaliibua mambo mengi hasa wananchi kujua umuhimu wa mawasiliano ya uhakika katika maendeleo yao.

Baada ya mafunzo hayo ambayo nitayaelezea kwa undani katika makala zijazo hivyo kwa leo
makala haya yatajikita zaidi katika suala la madhara ya mionzi ya simu na minara ambalo liliulizwa takriban katika mikutano yote ya mafunzo hayo.

Wananchi wengi walionekana kuguswa na suala hilo kutokana tetesi zilizozagaa mitaani
kuwa mionzi ya simu na minara ya mawasiliano inasababisha madhara makubwa kwa
binadamu kama vile kupunguza nguvu katika viungo vya uzazi na kusababisha magonjwa
makubwa kama vile ugonjwa wa saratani.

Kwakuwa suala hilo lilionekana kugubika mada nyingine katika mafunzo hayo, takriban maofisa wote walilazimika kulizungumzia ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaondokana na dhana hiyo potofu hatimaye waendelee kutumia huduma ya mawasiliano ya simu kwa maendeleo ya maisha yao.

Bila kutoa ufafanuzi makini kuhusu suala hilo upo wasiwasi mkubwa kuwa wananchi
wangeweza kuacha kutumia baadhi ya vifaa vya mawasiliano kutokana na kuhofia afya zao
kuathirika.

Kwa kuzingatia maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau wa mawasiliano na wananchi kwa ujumla maofisa hao walitoa ufafanuzi ufuatao: Kwa mfano Mhandisi Moyo anasema mionzi inayotoka kwenye vyombo vya mawasiliano kama simu redio, televisheni vipo kwenye kiwango cha chini sana kuweza kumdhuru binadamu.

“Kiasi cha mionzi hiyo ni sawa na kile kilichothibitishwa na mashirika mbali mbali ya kimataifa kufuatia utafiti uliochukua takriban miaka 50,” anasema Moyo na kuongeza:
“Mashirika yaliyohusika katika utafiti huo ni pamoja na: Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano ya Simu (International Telecommunications Union - ITU); Shirika la Afya Ulimwenguni (World Health organization - WHO); Tume ya Kimataifa ya Kinga Dhidi ya Mionzi (International Commission on Non-ionizing Radiation Protection - ICNIRP) Chama cha Mawasiliano ya Simu za Mkononi (GSM Association); ambapo ilithibitika kuwa mawasiliano ya simu hayana madhara kwa watumiaji.

Anasema kwa kutumia kipimo cha jinsi mionzi inavyoingia kwenye mwili wa binadamu
ambacho kwa lugha ya kitaalamu kinajulikana kama “Specific Absorption Rate (SAR)”, ilibainika wazi kuwa nguvu ya mionzi ipo chini ya kiwango fulani hivyo haina athari
kwa mwili wa binadamu tofauti na uvumi ulioenea mitaani.”

Anasema nguvu za mionzi hupungua kutoka chanzo cha mionzi hiyo. Kutokana na utafiti
uliofanywa na Taasisi za ICNIRP na ITU, SAR ni Watt 2 kwa uzito wa kilo moja kwa kichwani
na kiwiliwili) na Watt 4 kwa uzito wa kilo moja (4 W/kg kwa miguuni na mikononi).

Anaeleza kuwa bado viwango hivyo ni vikubwa kwa watumiaji wa kawaida ambao mara nyingi hawapo katika maeneo yenye mionzi mingi. Kwa upande mwingine, anasema mawimbi ya umeme na sumaku (electromagnetic waves) yako ya aina nyingi, hivyo athari zake zinatofautiana pia.

Kwa mfano,anaeleza kwamba kuna mawimbi ya radio, mawimbi ya microwave, infrared, mwanga wa kawaida, ultraviolet, Xray, gamma rays(mawimbi yatokanayo na nyuklia) na kadhalika.

Anasema nguvu ya mionzi ya redio na simu ya mkononi ni kidogo ikilinganishwa na
mwanga unaoonekana kwa macho. Vyanzo vya mionzi hii huweza kuwa ama vya asili au mitambo mbali mbali.

Anasema ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa salama zaidi licha ya udogo wa mionzi minara ya mawasiliano huwa na urefu wa mita 15 hadi 50 au kwenye majumba marefu, kwa hiyo nguvu inayomfikia binadamu ni ndogo.

Naye Kayombo anaeleza kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, (TCRA) imekuwa ikifanya
jitihada kushawishi watoa huduma za mawasiliano na utangazaji kushirikiana kutumia
Minara pamoja ili kupunguza wingi wake.

Anasema hatua mojawapo iliyochukuliwa ni kutoa mfumo mpya wa leseni ambao una
leseni nne: Leseni ya miundombinu, leseni ya kutoa huduma, leseni ya matumizi na leseni ya
utangazaji.

Vile vile anaeleza kuwa Mamlaka imetoa kanuni za mawasiliano za 2005 ambazo zinawashawishi watoa huduma kujenga minara na kukodisha wengine badala ya kila mmoja
kuwa na mnara wake mwenyewe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni